Header Ads

TPDC " Zaidi ya asilimia 50 ya Umeme wa Gridi ni Gesi "

Wataalam kutoka Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) Mamlaka ya Udhibiti wa Shughuli za Mkondo wa Juu wa Mafuta (PURA) na Wizara ya Nishati na Madini wakijadiliana jambo kabla ya kukutana na kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini mjini Dodoma.
...................................

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) Mhandisi Kapuulya Musomba ameileza Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuwa, hivi sasa zaidi ya asilimia 50 ya umeme uliopo katika Gridi ya Taifa unatokana na gesi asilia.

Mhandisi Musomba aliyasema hayo hivi karibuni mjini Dodoma, wakati akiwasilisha Taarifa ya Utekelezaji wa Miradi ya TPDC kwa kipindi cha mwezi Julai hadi Disemba, 2016 na kuongeza kuwa, mipango ya Serikali ni kulifanya Shirika hilo kuchangia zaidi mapato Serikalini yanayotokana na rasilimali hiyo.

Aidha, alieleza kuwa, kwa kuwa Tanzania imeingia kwenye uchumi wa Gesi asilia, shirika linajipanga kuwekeza kwenye shughuli za utafutaji, uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa gesi ili Taifa linufaike na rasilimali hiyo.

Akifafanua shughuli ya usambazaji gesi asilia kwa kuzalisha umeme, alisema kuwa, TPDC inaendelea kuhakikisha kwamba mitambo ya kuzalisha umeme inaunganishwa na miundombinu ya usambazaji gesi asilia ili iweze kutumia gesi asilia kuzalisha umeme.

“Mheshimiwa Mwenyekiti, TPDC kwa kushirikiana na TANESCO iliendelea kusimamia ujenzi wa miundombinu ya Kudumu ya usambazaji gesi asilia kwenye mitambo ya Kinyerezi I, Ubungo II,Tegeta na IPTL,”alisema Musomba.

Kaimu Mkurugenzi   Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Mhandisi Kapuulya Musomba, akiwasilisha Taarifa ya Utekelezaji wa Miradi ya TPDC kwa kipindi cha kuanzia Mwezi Julai hadi Disemba, 2016 kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini. Wengine wanaofuatilia ni Watendaji kutoka Wizarani na TPDC.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Doto Biteko (aliyesimama), akieleza jambo wakati wa kikao kati ya Kamati hiyo na Wizara ya Nishati na Madini na Watendaji kutoka Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).

No comments

Powered by Blogger.