( VIDEO ) Tanzania Imeahidi Kushirikiana na Afrika Kusini Kwenye Sekta ya Utamaduni na Sanaa
.....................................................
Na Genofeva Matemu -
WHSUM
Serikali ya Tanzania
itaendelea kuweka historia ya Ukombozi wa Bara la Afrika kwa kuhifadhi
kumbukumbu zote huku ikitunza na kuweka alama maeneo ambayo yalitumika wakati
wa kupigania Uhuru wa Bara la Afrika na kutunza makaburi ya wapigania uhuru hao
pamoja na kuyafanya kuwa ya kihistoria.
Hayo yamesemwa leo
Jijini Dar es Salaam na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Nape
Moses Nnauye alipokutana na Waziri wa Utamaduni na Sanaa wa Afrika ya Kusini
Mhe.Nathi Mthehwa aliyeko nchini kwa ziara ya siku tatu kwa lengo la kuimarisha
uhusiano wa nchi hizo mbili katika sekta ya Utamaduni na Sanaa.
“Tumeanza kuandika historia ya Ukombozi wa
Bara la Afrika kwa kuhoji baadhi ya wanaharakati walioshiriki katika kuwasaidia
wapigania uhuru kuanzisha vyama vyao vya ukombozi ambapo historia hii
itahifadhiwa kwa njia ya sauti na picha lakini pia tutaendelea kutunza kumbukumbu
zote tutakazozipata na kuwekea alama maeneo ambayo yalitumika wakati wa kupigania
uhuru” amesema Mhe. Nnauye.
Aidha, Mhe. Nnauye
amesema kuwa makubaliano yaliyosainiwa mwaka 2011 kati ya Tanzania na Afrika ya
Kusini kufuta Visa ya kusafiria kati ya nchi hizo mbili yameleta mabadiliko makubwa katika eneo la Sanaa
nchini kwani wasanii wamekua wakitumia fursa hiyo kwenda Afrika ya Kusini
kuandaa kazi zao na kuzifanya kuwa na ubora zaidi.
Kwa upande wake
Waziri wa Utamaduni na Sanaa wa Afrika Kusini Mhe. Nathi Mthehwa ameishukuru
Serikali ya Tanzania kwa kuendeleza ushirikiano uliopo baina ya nchi hizo mbili
na kuthamini mchango uliofanywa na Tanzania katika kukomboa nchi ya Afrika ya
Kusini.
Pamoja na hayo Mhe.
Mthethwa ameahidi kuendeleza ushirikiano ulipo na kuthamini maendeleo yaliyopo
kwenye maeneo ya Utamaduni na Sanaa kwa kuhakikisha kuwa mafanikio ya Sekta za
Ubunifu ndani ya Afrika ya Kusini yanakua sehemu ya mafanikio ndani ya nchi ya
Tanzania.
Ziara hii inaangalia
namna nchi hizi mbili zinaweza kuimarisha makubaliano ya mwaka 2011, katika maeneo
mengine ya mashirikiano kama vile upande wa tasnia ya filamu ambapo Afrika ya
Kusini imekua ikifanya vizuri ikiwemo kusimamia haki za wasanii kwa kutengeneza
mifumo ya kisheria ya kulinda haki za ubunifu na kuongeza mahusiano ya nchi hizo mbili.
Waziri huyo atatembelea Mkoa wa Morogoro kwenye kambi ya
wapigania Uhuru wa Afrika ya Kusini Mazimbu, Dakawa pamoja na Bagamoyo ambapo
kulikua na kambi yao,pamoja na baadhi ya maeneo Jijini Dar es Salaam.
Post a Comment