Dkt CHARLES MWIJAGE aipongeza TRA kwa Jitihada za Kuelimisha Wafanyabiashara
Na
Mwandishi Wetu.
Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe.
Charles Mwijage ameipongeza na kuishukuru Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa
jitihada za kuendelea kuelimisha wafanyabiashara kutambua umuhimu wa kulipa
kodi utakaoiwezesha Serikali kusonga mbele katika suala zima na ukuzaji wa
viwanda vya ndani hapa nchini.
Mhe. Mwijage aliyasema hayo wakati wa ufunguzi wa
mkutano wa nne wa mwaka wa Taasisi isiyo ya kiserikali inayotoa Msimbomilia (Barcode) za bidhaa
(GS1); uliofanyika tarehe 29 Novemba 2016 katika ukumbi wa mikutano wa Karimjee
jijini Dar es Salaam.
Mkutano huo uliandaliwa kwa ushirikiano kati ya
GS1 na TRA kwa lengo la kujadili masuala mbalimbali yanayowahusu wadau wao,
kujadili mambo muhimu ya kodi yanayohusu umuhimu wa Namba ya Utambulisho wa
Mlipakodi (TIN) katika kuweza kupata
msimbomilia (barcodes 620) na kuweza kuzitambulisha bidhaa za Tanzania
kimataifa pamoja na kuadhimisha miaka mitano tangu kuanzishwa kwa taasisi hiyo.
Waziri Mwijage aliliagiza Shirika la Viwango
Tanzania (TBS) kuhakikisha kila mfanyabiashara anayemiliki viwanda vidogo na
vya kati kuhakikisha anakuwa na TIN na namba ya msimbomilia 620
inayotolewa na GS1 Tanzania kabla ya kuhuisha vyeti vyao vya biashara.
Aidha Waziri Mwijage amesema kuwa uchumi wa viwanda unatakiwa kukua nchini ili kuweza
kuzalisha bidhaa bora zitakazouzwa ndani na nje ya nchi na kukusanya kodi stahiki itakayoiwezesha
Serikali kutoa huduma bora za kijamii
kwa maendeleo ya wananchi wa Tanzania .
“Ifike
wakati wafanyabiashara muwaelewe vizuri TRA na kulipa kodi stahiki ya Serikali,
ili nchi iweze kusonga mbele” alisema Mhe. Mwijage.
Kwa
upande wake Afisa Mkuu wa Elimu kwa Mlipakodi kutoka TRA Bi. Rose Mahendeka
alisema kuwa wafanyabiashara wote ambao wanahitaji kutumia mfumo wa kuuza
bidhaa kwa kuweka msimbomilia (Barcode 620) wanapaswa kupitia TRA kwa ajili ya
usajili na uhakiki wa Namba ya Utambulisho wa
Mlipakodi (TIN) kabla ya kwenda kupata huduma ya msimbomilia 620.
Bi.
Mahendeka aliwasisitiza wadau hao kuhakikisha wanajisajili na TIN na wale
waliojisajili kuhakikisha wanahakiki taarifa zao ili kurahisisha upatikanaji wa
Msimbomilia 620 na kuiwezesha TRA kupata takwimu sahihi za wafanyabiashara
wazalishaji na wanaouza bidhaa zao nje ya nchi.
“Wafanyabiashara
wote ambao wanahitaji kutumia mfumo wa kuuza bidhaa kwa kuweka
Msimbomilia(Barcode 620) wanapaswa kupitia TRA kwa ajili ya usajili na uhakiki
wa Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi(TIN)
kabla ya kwenda kupata huduma” alisisitiza Bi. Mahendeka.
Aidha
Bi. Mahendeka alisema kuwa wafanyabiashara ambao wanahitaji kuuza bidhaa zao
kwa kutumia msimbomilia wanapaswa kulipa kodi bila ya kukwepa ili kuiwezesha
Tanzania kupiga hatua kufikia uchumi wa viwanda na vilevile kuweza kutoa huduma
bora kwa maendeleo ya jamii.
Naye
Mwenyekiti wa bodi ya GS1 Bw. Gideon Mazara alitoa rai kwa wafanyabiashara
wanaozalisha bidhaa kutumia Msimbomilia 620 wa Tanzania na kuweza kutangaza
bidhaa za hapa nchini ili kupata soko la kimataifa litakalowezesha nchi kufikia
uchumi wa kati .
Post a Comment