Waziri
wa Habari,Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Nape Moses Nnauye (wa tatu kushoto)
akiwa na ujumbe wa Serikali ya China wakati wa mazungumzo ya kuimarisha sekta
ya habari nchini yaliyofanyika jana Jijini Dar es Salaam.Wa kwanza kulia ni
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC).
...........................................
Na Shamimu Nyaki-WHUSM
Serikali imeahidi kuendeleza ushirikiano na Serikali ya China katika kuimarisha sekta ya habari ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia ya utoaji wa habari.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Habari,Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Nape Moses Nnauye jana Jijini Dar es Salaam katika mazungumzo na Naibu Waziri wa Uenezi wa China Ndg. Sun Zhijun yaliyolenga kuimarisha sekta ya habari nchini.
“Tunashukuru kwa uhusiano mzuri uliopo baina ya serikali zetu ikiwemo hii ya kuendeleza sekta ya habari ambayo ni muhimu na inamchango mkubwa katika kuleta maendeleo na kutoa ajira kwa watanzania”.Alisema Mhe Nape.
Mhe. Nape anaongeza kuwa ushirikiano huo utasaidia nchi zote mbili kuwa na uwezo wa kuwafikia wananchi kwa ukaribu zaidi kupitia vipindi mbalimbali vinatakavyokuwa vikirushwa na vyombo vya habari vya nchi hizo kwa lugha zote mbili.
Kwa upande wake Mhe. Naibu Waziri wa Uenezi wa China Mhe.Sun Zhijun ameahidi kufanya mageuzi katika soko la habari kupitia radio na Luninga ambazo zitatoa fursa ya kuonyesha vipindi mbalimbali vya Kiswahili na hivyo kusaidia katika kukuza na kueneza lugha hiyo.
“Ushirikiano wetu ni wa tangu enzi na enzi hivyo ni budi kuutunza na kuulinda umoja wetu ndo maana tukaona kuna umuhimu wa kuimarisha sekta ya habari ambapo Serikali yetu ya China itakuwa ikirusha vipindi vya radio na luninga kama vile muziki na filamu za kiswahili katika vyombo vyetu vya habari ”.Alisema Mhe.Zhijun.
Vyombo vya Habari vya Tanzania na China vimekuwa vikishirikiana katika kubadilishana Habari na vipindi mbalimbali kupitia Chaneli zao na hivyo kusaidia ushirikiano kati ya nchi hizi mbili kuendelea kuimarika na kustawi zaidi.
|
Post a Comment