Mzazi Azuiliwa Kuondoka Hospitali ya Muhimbili Kwa Kushindwa Kulipa Shilingi 338,257
Mzazi Sakina Lembo |
Na Dotto Mwaibale
MZAZI Sakina Mohamed Lembo (26) pichani mkazi wa Mbagala Kibonde Maji amezuiliwa kuondoka wodi ya wazazi katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), kutokana na deni la sh. 338,257 baada ya kufanyiwa oparesheni ya uzazi.
Akizungumza na mtandao huu wodini hapo Dar es Salaam leo, Lembo alisema hajui hatma yake kwani yeye na ndugu zake hawana uwezo wa kulipa fedha hiyo ambayo kila siku imekuwa ikiongezeka kama riba.
Mama mzazi wa Salome, Edith Chausa akizungumza na mtandao huu alisema mwanaye alifikishwa katika hospitali hiyo Novemba 15, 2016 akitokea Hospitali ya Serikali ya Zakhem ambapo walimuandikia rufaa kwenda MNH baada ya kubaini alikuwa na dalili za kifafa cha mimba.
Lembo alisema baada ya kufika MNH alichunguzwa na kufanyiwa upasuaji wa uzazi ambapo juzi aliambiwa alipe sh.3000 ili mwanaye aweze kuletewa wodini.
Aliongeza kuwa siku ya Ijumaa Daktari ajulikanaye kwa jina la Julieth Kileo alimruhusu kuondoka lakini wauguzi waliokuwa zamu walimzuia na kumwambia hawezi kuondoka mpaka alipe kiasi hicho cha fedha ambacho hawana uwezo wa kulipa.
"Mpaka leo hii hatujui cha kufanya kwani hatuna fedha hizo na kibaya zaidi kadri siku zinavyoongeza na fedha hizo zinaongezeka kwani tumeona kwa mwenzetu mmoja ambaye alilipa sh.600,000 tunaomba serikali kuliangalia jambo ili kwa karibu kwani tusiokuwa na uwezo wa kifedha tunachangamoto kubwa" alisema Chausa.
Jitihada za gazeti za kumpata Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Umma na Huduma kwa Wateja wa Hospitalini hiyo, Aminiel Eligaesha ili kulitoa ufafanuzi suala hilo hazikuzaa matunda baada ya kupigiwa simu kwa muda mrefu lakini ikawa imefungwa.
Post a Comment