Header Ads

KASSIM MAJALIWA : Hakuna Kiongozi wa Serikali anayepinga Zoezi la Uhifadhi


Na Hamza Temba - WMU
Kufuatia malalamiko ya wahifadhi juu ya kauli na vitendo mbalimbali za baadhi ya wananchi na viongozi wa kisiasa vyenye lengo la kukwamisha shughuli za uhifadhi nchini kwa maslahi yao binafsi kwa visingizio kuwa ni maagizo kutoka juu, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ametoa tamko na kusema kuwa hakuna kiongozi wa juu wa Serikali anayepinga zoezi la uhifadhi wa maliasili nchini.
Majaliwa ameyasema hayo juzi wakati akizungumza na viongozi na watendaji wakuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, wakuu wa taasisi za uhifadhi zilizopo chini ya wizara hiyo na wakuu wa hifadhi za taifa pamoja na mapori ya akiba katika kikao alichokiitisha kwenye ukumbi wa ofisi ya Waziri Mkuu mjini Dodoma.
“Wapo watu wanaotumia majina ya viongozi wakuu kukwamisha mazoezi yanayoendeshwa na wahifadhi nchini. Hakuna kiongozi wa juu anaeweza kuzuia zoezi muhimu kama hili. Na Kama kuna mtu anakuja kukuambia wewe fulani kasema, mwambie niunganishe na yeye mwenyewe.  Tumeona maeneo mengi sana, watu wanafanya madudu wanasema huyu kaagizwa kutoka juu, juu ni wapi, kwa Mkurugenzi wako? kwa Katibu Mkuu?  Naibu Waziri au Waziri? Au huku kwa Waziri mkuu? Makamu wa Rais au Rais?,” alihoji.
“Fanyeni, bora ukosee halafu tuseme hapo umekosea utarekebisha, kuliko kuogopa kufanya kwa sababu mtu kakukwamisha, kwani ulivokuwa unaimplement (unafanya) alikuambia nani? si kutokana na na sheria na taratibu, muhimu zaidi ni kuzingatia sheria na taratibu, usije ukafanya mambo ya ajabu,” aliongeza.
Ili kufanikisha zoezi hilo aliwaagiza pia kuhakikisha wanaweka alama za mipaka (beacons) katika hifadhi zao hadi kufikia januari 31, 2017 ili kuepusha migogoro na wananchi wanaovamia maeneo hayo kwa makusudi au kwa kutokujua maeneo ya mipaka husika.
“Nendeni mkawaambie mwisho ni hapa weka na beacon kabisa, na sheria zitachukua mkondo wake kwa yeyote ambaye hatafata maelekezo yenu. Tatizo la migogo iliyozungumzwa kati wa wafugaji na wahifadhi au wafugaji na kamati za ulinzi na usalama za wilaya na mikoa ni lazma likafanyiwe kazi, lazima tuendelee kudhibiti kuingia mifugo ndani ya mapori,” alisisitiza.
Aliwaagiza pia kusimama kwenye majukwaa na kutoa elimu ya uhifadhi kwa wananchi wanaozunguka maeneo yao ya hifadhi. “Namba moja wa utoaji elimu ni wewe mkuu wa pori, ni lazma utoe maelezo ya pori lako ni wapi linakoishia, kama mpaka huo ni wa kisheria muwaambie, nini umuhimu wa kutoingia, wananchi wapate elimu namna ya kuhifadhi pori na faida zake,” alisema.
Akizungumzia changamoto iliyoibuliwa katika kikao hicho kuhusu mgongano uliopo katika usimamizi wa misitu baina Wakala wa Huduma za misitu Tanzania na Serikali za Mitaa alisema Serikali inaenda kuliangalia upya suala hilo ili ione namna bora ya kutoa majukumu ya kusimamia rasilimali zote za misitu kwa chombo kimoja tofauti na ilivyo hivi sasa, hatua ambayo inaelezwa kuwa itasaidia kwa kiasi kikubwa kuondoa changamoto za uharibifu wa misitu nchini.
“Kama ilivyoelezwa kuwa kuna mgongano wa majukumu kwenye kitengo cha misitu, baina ya TFS na DFO (Ofisa misitu wa Wilaya), DFO anauza bila hata kumconsult (kumtaarifu) TFS na anagonga na nyundo…, kwa hiyo tutaliangalia tuone majukumu yale na namna ambavyo tunaweza tukayapa chombo kimoja ili kisimamie lakini TFS mmeperform (mmefanya) vizuri endeleeni kufanya hivyo vizuri kwa sasa,” alisema huku akipigiwa makofi na watendaji hao.
Changamoto nyingine iliyoibuliwa katika kikao hicho ni matukio ya kuingizwa kwa mifugo katika maeneo ya hifadhi yaliyoko mpakani huku asilimia kubwa ya mifugo hiyo ikielezwa kutoka nje ya nchi, Waziri Mkuu Majaliwa amekemea kitendo hicho na kuagiza mifugo hiyo iondolewe mara moja. “Hatutaki ng'ombe wa nje ya nchi kuingia ndani ya nchi, mifugo ya ndani imetutosha,” alisema.
Aidha ameutaka uongozi wa Wizara kuimarisha doria za mara kwa mara, kuongeza ajira za makamanda (askari wa wanyamapori) na vitendea kazi muhimu vya kuimarisha doria ikiwemo magari.
Kwa upende wake Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe alisema ipo changamoto kubwa ya tishio la kutoweka kwa mvua na kukauka kwa vyanzo muhimu vya maji nchini kutokana na uharibifu wa maeneo yaliyohifadhiwa pamoja na mlipuko wa magonjwa mbalimbali yanayosababishwa na muingiliano wa mifugo na wanyamapori kama vile kimeta na homa ya bonde la ufa.
Naye Mkurugenzi wa Idara ya Utalii wa Wizara hiyo, Zahoro Kimwaga alisema, umuhimu wa uhifadhi una faida mtambuka  ambapo sekta ya utalii pekee inachangia asilimia 17 ya pato la taifa huku ikitoa ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja takriban milioni 1.5. Alisema sekta hiyo pia inachangia asilimia 25 ya mapato yote ya fedha za kigeni ikiwa ni sekta kiongozi kwa muda wa miaka mitatu mfululizo.
Aliongeza kuwa hadi kufikia Novemba 20 mwaka huu takwimu zinaonyesha kuwa maendeleo ya sekta ya utalii yameongezeka kwa asilimia 5 licha ya malalamiko mbalimbali kuhusu sekta hiyo baada ya Serikali kuweka kodi ya VAT katika huduma za kitalii nchini.

No comments

Powered by Blogger.