Mbunge wa Namtumbo
Eng. Edwin Ngonyani akitoa maelekezo kwa mwenyekiti wa kamati ya ujenzi wa
zahanati ya Mchomoro mara baada ya kukagua ujenzi wa zahanati hiyo.
...................................
Mbunge wa Jimbo la
Namtumbo ambae pia ni Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng.
Edwin Ngonyani amewahakikishia wananchi wa Kata ya Mchomoro Wilayani humo kuwa
jengo la Zahanati ya kijiji hicho litakamilika na kuanza kutoa huduma mwezi Machi
mwakani kama ilivyopangwa.
Jengo hilo ambalo
ujenzi wake unatokana na kuharibika kwa jengo la zamani kulikosababishwa na
ujenzi wa barabara ya Songea- Tunduru linatarajiwa kuendelezwa ili kuwa kituo
cha afya na hivyo kuhudumia idadi kubwa ya wananchi wa Kata hiyo.
Akizungumza mara baada
ya kukagua ujenzi wa jengo hilo Eng. Ngonyani amewakabidhi wasimamizi wa ujenzi
huo fedha kwa ajili ya kukamilisha hatua upauaji wa jengo hilo na kusisitiza
umuhimu wa matumizi sahihi ya fedha hizo
ili ziwiane na ubora wa kazi.
“Hakikisheni mnazingatia
makubaliano ili zoezi la kuezeka jengo hili la Zahanati likamilike kabla ya
Januari na hivyo kuwezesha zahanati hii kuanza kazi mapema mwezi Machi”.
Amesema Eng.Ngonyani.
Zahanati hiyo ambayo
ujenzi wake unagharamiwa na Mbunge wa Namtumbo akishirikiana na kampuni ya Mantra
Tanzania LTD na nguvu za wananchi wa kata hiyo inatarajiwa kupandishwa hadhi
kuwa kituo cha afya cha kata hiyo mara zoezi la ujenzi wa majengo mengine utakapokamilika.
Naye msimamizi wa
ujenzi wa zahanati hiyo Bw, Yasini Languka amemhakikishia Mbunge huyo wa
Nmatumbo kwamba fedha zinazopelekwa kwaajili ya ujenzi huo zinatumika kama
ilivyokusudiwa ili kufikia lengo la kuifungua upya zahanati hiyo ifikapo mwezi Machi
mwakani na hivyo kuwaondolea usumbufu wananchi wa Kata hiyo.
Katika hatua nyingine
Naibu Waziri huyo amekagua barabara ya Mangaka –Tunduru- Matemanga –Namtumbo hadi
Songea na kuwataka wananchi kutoa taarifa kwa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS)
pale wanapoona vitendo vya hujuma katika barabara hiyo ikiwemo utengenezaji na
uegeshaji wa magari mabovu katika barabara hiyo.
Naibu Waziri Ngonyani
yupo katika ziara ya kukagua Miundombinu ya barabara, Bandari na Mawasiliano
katika mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma.
|
Post a Comment