( MAKALA ) Profesa NDALICHAKO ondoa Pamba Masikioni Kuhusu Mikopo ya Elimu ya Juu
Na BARAKA NGOFIRA
Tatizo la mikopo kwa
wanafunzi wa elimu juu limekuwa likipigiwa kelele kila siku na wadau mbalimbali
wa elimu, huku wanafunzi wa vyuo vikuu wakiwa wahanga wakubwa wa mikopo.
Hata
wale wanaonufaika na mkop huo ambao hutolewa na bodi ya mikopo ya elimu ya juu
HESLB. Kwa uzoefu wangu mdogo wa kwenda kuangalia ofisi za bodi ya mikopo
zilizopo Mwenge jijini Dar es salaam hakuna siku hata moja ambayo sikukuta
wanafunzi kutoka vyuo mbalimbali wakifuatilia mikopo yao.
Wengi wao ni watoto wa
maskini na wakulima ambao wametoka mikoani na kuchaguliwa vyuo vilivyo Dar es salaam
na maeneo ya jirani. Lakini pia wapo wale ambao huingia gharama za kuja Dar es
salaam kufuatilia mikopo lakini kwa masikitiko huambulia kupoteza nauli na muda
wao bure na kuamua kusitisha masomo ambayo ndiyo njia pekee ya kuishi ndoto
zao.
Tangu serikali itoe
majina ya wanufaika wa mkopo wa elimu ya juu ambayo mpaka sasa ni zaidi ya
wanafunzi elfu ishrini na moja wa mwaka wa kwanza ambao wamepewa mkopo kati ya
waombaji zaidi 58000 walikuwa wameomba mkopo. Huku lengo la serikali kwa mwaka
huu likuwa kuwapa mkopo wanafunzi 25,500 tu kwa mwaka huu wa fedha.
Kwa idadi
hiyo ni sawa na asilimia kama 38 hivi za waombaji wote wa mwaka huu wa masomo
2016/17.
Nimekuwa nikipokea simu
na jumbe nyingi kwenye simu yangu za wanafunzi, wazazi pamoja na walezi wa
wanafunzi mbalimbali wakilia mizigo mizito na msongo wa mawazo walionao kwa
kukosa mkopo wa elimu ya juu huku sifa zote wakiwa nazo. Lakini mkopo wamenyima
hivyo kuwalazimu watoto wao kusiotisha masomo na kurudi nyumbani kulima na
kuchunga ng’ombe maana ndizo kazi pekee ambazo zimewakuza na kuwasomesha.
Kwa taarifa zisizo
rasmi zaidi ya wanafunzi 10,000 wa mwaka wa kwanza kwa mwaka huu pekee bado
hawajaripoti kwenye vyuo walivyopangiwa. Idadi hii ni kubwa sana kwa taifa na
ni aibu kwa taifa ambalo serikali inajigamba kuwa ni tajiri kwa kuwa na
maliasili nyingi, madini ya kila aina, gesi na mbuga na hifadhi nyingi za
wanyama wa kila aina. Lakini cha ajabu imeshindwa kutoa elimu bure au kuchangia pesa
ya kujikimu kwa kila mwanafunzi wa elimu ya juu.
Kwa muda sasa nimekuwa
nikitiwa kichefuchefu na kauli za viongozi wa serikali hasa walionufaika
kusomeshwa na serikali. Bila hata ya aibu husubutu kusema hadharani hata bila
ya aibukuwa enzi wao wanasoma serikali ilikuwa ikiwahudumia kila kitu, kazii
yao ilikuwa ni kusoma tu.
Na cha kushangaza hadi
magari walikuwa wakipanda bure, kalamu, sabuni, chakula, malazi, posho, yaaani
kila kitu kwao kilikuwa ni bure. Lakini leo baada ya kupata elimu wamesahau
yote ambayo serikali iliwatendea badala yake wameondoa kila kitu na kuweka
elimu ya kujitegemea ili wao na wanao waendelee kufaidi matunda ya nchi hii.
Inasikitisha sana
pamoja na vilio vyote vya wanafunzi maskini na hoe hae ambao kwa sasa hawana
mbele wala nyuma lakini kwa sasa wako vyuo vikuu wamebaki njia panda. Na hivyo
kuamua kufanya ofisi za bodi ya mikopo kuwa shule yao ambapo kila kukicha wao
huenda na kurudi lakini bado serikali imeziba masikio.
Haisikii haioni na wala
hata haijali maana watoto wao wanasoma vyuo vikuu vya nje na kama wapo vyuo
vikuu vya ndani mkopo wamepewa kwa asilimia mia moja maana wao ni watoto wa
mabosi.
Agness Leonard
mwanafunzi aliyechaguliwa kujiunga na shahada ya kwanza ya ualimu Chuo Kikuu
cha Dar es salaam na kupewa namba ya usajili ya 2016-04-00782. Ni miongoni mwa
maelfu ya wanafunzi waliokosa mkopo kwa
mwaka huu huku akiwa anatokea familia maskini.
Ambao wanandoto ya kupata elimu
ya chuo kikuu lakini kwa sababu ya kukosa mkopo huku wakiwa na ufaulu mzuri
ameamua kusitisha masomo yake huku hata nauli ya kurudi nyumbani kwao Tabora
hakiwa hana.
Amesoma kwa shida sana
na kwa bidii huku akiamini kuwa akifaulu na kujiunga na elimu ya chuo kikuu
walau uchungu wa maisha utapungua. Lakini zilikuwa ni ndoto za mchana kwake
ambazo kwa sasa hana tena matumaini na kubaki kufutwa machozi na rafiki zake.
Maisha ya kushindia
mkate wa shilingi mia tano kila siku yamemshinda maana kwa sasa hata hiyo 500
ya kununulia mkate hana. Haya ndiyo maisha ya watoto wengi wa maskini na
makabwela wanaosoma vyuo vikuu.
Inatia hasira sana
kuona serikali inaweka vipaumbele vya mikopo kwa wanafunzi wa masomo ya sayansi
na mengine yakiachwa bila kipaumbele huku wanaosoma masomo ya biashara na sanaa
wakiachwa.
Na cha kushangaza zaidi wanaosoma masomo ya sayansi wenyewe mara
baada ya kumaliza vyuo hawathaminiwi na serikali yao.
Ndiyo ni jambo zuri
kuwekeza kwenye masomo ya sayansi lakini mbona hata wanasayansi waliosomeshwa
na serikali tena kwa gharama kubwa faida yao haionekani. Nasema haionekani kwa
sababu hatuna unachokitengeneza cha kwetu, viberiti, chumvi, kalamu, pamba za
kutolea uchafu maskioni na hata njiti za kutolea mabaki ya chakula tunaagiza
nje?
Japo sera na mikakati
ipo ya kuboresha viwanda vya ndani ili nasi tuwe na vya kujivunia, ni bora
serikali ikaweka mipango mikakati ya mikopo kwa wanafunzi wote wa elimu ya juu
pasipo kuwa na ubaguzi.
Rais Magufuli
alisisitiza kuwa mikopo ya elimu ya juu itakuwa kipaumbele ikiwa atachaguliwa.
Lakini leo imekuwa danganya toto kwa wanafunzi wa vyuo vikuu na kuongeza
uchungu zaidi kwao kwa kuwacheleweshea mkopo ambapo hadi waandamane na kupiga
kelele kwenye vyombo vya habari ndipo wapewe.
Cha kushangaza zaidi ni
baadhi ya watu ambao hata hawakuwahi kusoma au kunufaika na fedha za mkopo wa
elimu ya juu majina yao kuonekana kwenye orodha ya wadaiwa sugu. Jambo ambalo
linatia shaka kwa utendaji na usahihi wa taarifa na utunzwaji wa kumbukumbuku za
wanafuika wa mikopo kwa elimu ya juu.
Chonde chonde waziri wa
elimu wasaidie watoto wa maskini wapate mkopo wasome elimu ya juu kama wewe na
wenzako mlivyonufaika na elimu ya bure mliyopewa na serikali kwa kipindi chenu.
Ni haki yao kupata mkopo maana ni kodi za wazazi wao na babu zao waliowawekea
ninyi mazingira mazuri ya kusoma na kushikia nyazifa mlizonazo.
Lakini kama mmeamua
kuendelea kuweka pamba maskioni ili watoto wenu waendelee kusoma ili waje
kuongoza taifa ili haina shida lakini tambueni kuwa ipo siku Mungu atajibu
maombi yao. Maana machozi yao hayapotei bure.
Makala
hii imeandikwa na mwanafunzi wa mwaka wa tatu wa shahada ya kwanza ya
mawasiliano kwa Umma katika Chuo Kikuu cha Dar es salaam. Anapatikana kwa
mawasiliano ya barua pepe ya barakangofira@gmail.com au 0763580901.
Post a Comment