Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(Tamisemi), Selemani Jafo akikagua ujenzi wa barabara ya lami ya Sango katika eneo la Soko kuu la majengo, Manispaa ya Dodoma. ...........................................................
Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(Tamisemi), Selemani Jafo amefanya ziara katika manispaa ya Dodoma huku akipiga marufuku wafanyabiashara kupanga bidhaa zao kwenye barabara na kuwataka wafanye biashara zao kwenye masoko au maeneo rasmi yaliyotengwa na Manispaa hiyo.
Akizungumza leo mara baada ya kukagua ujenzi wa barabara ya Sango iliyopo katika soko kuu la majengo na ujenzi wa dampo la kisasa,Jafo amesema serikali inawekeza fedha nyingi kwenye barabara lakini mwisho wa siku barabara haionekani kutokana na watu kupanga bidhaa zao.
Naibu Waziri huyo amesema kupangwa kwa bidhaa za nyanya au vitunguu barabarani kumekuwa kukichafua barabara na wakati mwingine kusababisha zisipitike kiurahisi na watumiaji wengine.
Ameagiza Manispaa hiyo kuhakikisha malengo ya barabara hiyo yanafuatwa na kuwazuia wafanyabiashara hao ili barabara hizo zitunzwe ziweze kudumu na kufikia malengo.
“Hivi karibuni nilitembelea barabara hii na ilikuwa ni mbaya na ni eneo la kibiashara niliagiza Manispaa kuhakikisha barabara hii inajengwa, nimefarijika sasa agizo limetekelezwa,”amesema Jafo
Hata hivyo amesema kwa kuwa vikao vimeanza vya kupendekeza Dodoma iwe jiji ni lazima ibaki maana yake na thamani ya jiji ipatikane kwa watu kuweka bidhaa zao kwenye masoko yanayotakiwa.
Kuhusu Dampo la kisasa lililopo eneo la Chidaye mjini Dodoma, Jafo ameitaka manispaa kuhakikisha eneo hilo halivamiwi na watu kwa kuwa kumekuwepo na tabia ya wananchi kuvamia maeneo yanayojengwa miundombinu.
Naye, Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma, Godwin Kunambi amemuahidi Jafo kuwa atasimamia sheria ndogo ndogo za manispaa kuhakikisha wafanyabishara wanafanya biashara zao kwenye maeneo yaliyopangwa.
|
Post a Comment