( MAKALA ) Fahamu Jinsi Fedha za Tetemeko la Ardhi Mkoani KAGERA zilivyotumika
Na Mathias Canal
Ndugu zangu kama ambavyo tunakumbuka Tarehe 10/09/2016 majira ya saa 9
na dakika 27 Alasiri maeneo ya Kanda ya ziwa hasa Mkoani Kagera
kulitokea tetemeko la ardhi linalokadiriwa kuwa na ukubwa wa 5.9 katika
vipimo vya Richter ambapo Kitovu cha tetemeko hilo ni kwenye makutano ya
latitudo 10 06’ na longitudo 31055’ eneo ambalo ni kilomita 20
kaskazini mashariki mwa kijiji cha Nsunga na kilomita 42 kaskazini
magharibi mwa mji wa Bukoba na Kitovu hicho kilikuwa kilomita 10 chini
ya ardhi kwenye eneo hilo.
Tetemeko hilo la ardhi liliacha
familia kadhaa zikiwa na huzuni kubwa kwa kuwapoteza ndugu, jamaa na
rafiki zao ambapo idadi ya watu waliofariki walikuwa ni 17 huku watu 560
wakipatiwa matibabu kutokana na majeraha waliyoyapata sambamba na
kukutikana kwa uharibifu wa makazi na miundombinu ya umma na watu
binafsi.
Kwa Mujibu wa Mtendaji Mkuu, Wakala wa Jiolojia Tanzania
(GST) alieleza sababu za kutokea kwa Tetemeko hilo la ardhi kuwa
ilikuwa ni kutokana na kitovu cha tetemeko hilo kuwa kiko chini sana ya
ardhi (Km 10) na kwa kutafasiri umbile la mawimbi ya tetemeko hilo
yaliyonakiliwa na vituo vya kupimia matetemeko ya ardhi inaonekana kuwa
tetemeko hilo limetokana na misuguano ya mapange makubwa ya ardhi
iliyopasuliwa na mipasuko ya ardhi mithili ya mipasuko kwenye bonde la
ufa.
Kwa kuwa eneo lililokumbwa na tetemeko la ardhi liko karibu
na mkondo wa magharibi wa bonde la ufa la Afrika Mashariki inakisiwa
kuwa mtetemo huo ulisababishwa na kuteleza na kusiguana kwa mapande ya
miamba juu ya mipasuko ya ardhi ya bonde hilo la ufa.
Katika siku
za karibuni kumekuwepo na taarifa mbalimbali katika mitandao ya kijamii
ikiwemo facebook, Twitter, Blogs, Instagram na Makundi mbalimbali ya
Watsup jambo ambalo lilinilazimu kufunga safari na kuweka kambi ya
takribani siku nne Mkoani Kagera ili kubaini ukweli wa namna fedha
zilizopatikana na zilivyotumika ikiwa ni pamoja na mahitaji mengine
jinsi yalivyopatikana na namna yalivyoelekezwa.
UKWELI WA MAMBO
Kufuatia tathmini zilizofanyika kupitia wataalamu mbalimbali, makadirio
ya awali yalibaini kuwa kiasi cha jumla ya shilingi Bilioni 104.9
zinahitajika katika kukabiliana na kurejesha hali katika Mkoa wa Kagera
kufuatia maafa hayo. Ambapo gharama hizi zinajumuisha:
a) Ujenzi
wa makazi ya muda kwa waathirika wa nyumba zipatazo 16,667
zilizoharibika katika viwango tofauti, ambapo kiasi cha Shilingi Bilioni
41.7 zitahitajika.
b) Kiasi cha shilingi 1.92 kwa ajili ya kodi ya miezi sita kwa wapangaji waliokuwa wakiishi kwenye nyumba zilizoharibiwa.
c) Ukarabati wa shule za msingi 163 kwa gharama ya shilingi Bilioni
12.7, sekondari 57 kwa gharama ya shilingi Bilioni 45.65, vituo vya afya
na zahanati 32 kwa gharama ya shilingi milioni 772 na Majengo ya
taasisi nyingine 20 kwa shilingi Bilioni 1.3
MISAADA ILIYOTOLEWA
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Katibu Mkuu
(WAZIRI MKUU NA BUNGE) Ndg Uledi A. Mussa ilibainisha kuwa hadi kufikia
Tarehe 13 Novemba, 2016 serikali ilikuwa imepokea misaada ya vifaa,
Chakula, Fedha na ahadi mbalimbali zenye thamani ya shilingi Bilioni
15.19 kutoka kwa wadau mbalimbali, washirika wa Maendeleo, Balozi wan
chi marafiki ambapo tayari misaada hiyo imeshagawiwa na inaendelea
kusambazwa kwa walengwa.
Msaada ya misaada iliyopokelewa ni kama ifuatavyo:
Fedha taslimu kiasi cha shilingi Bilioni 5,412,934.82 kimeshapelekwa Benki.
Kiasi cha shilingi milioni 17,579,427.00 kupitia mitandao ya simu
Ahadi za shilingi Bilioni 6,703,000,000 Hivyo jumla ya ahadi na fedha taslimu hadi sasa ni Shilingi Bilioni 12,133,564,361.82
Serikali pia imepokea misaada mingine yenye thamani ya shilingi
Bilioni 2.25 kama ifuatavyo: Unga Tani 58.12, Sukari Mifuko 1,150,
Mchele Tani 133.96, Maharagwe Tani 19.666. Mahindi Tani 70.1, Majani ya
Chai Tani 3, Maji Katoni 1,570, Mafuta lita 6,022, Sabuni Katoni 443,
Shuka 495, Blanketi 6,125, Vyandarua 2,821, Magodoro 1,146, Mahema 367 n
Turubai 6,237 vilipokelewa.
Aidha serikali ilipokea vifaa vya ujenzi
vikiwemo Saruji mifuko 24,433, Bati 20,933, Misumari kilo 1475, Nondo
vipande 725, Kofia za bati 150 na mbao 250.
Lakini ifahamike kuwa
baadhi ya waaliotoa ahadi kama serikali ya Uingereza wameahidi
kutekeleza ahadi zao kwa kujikita moja kwa moja katika ujenzi wa Shule,
Mara baada ya wakala wa majengo kuainisha viwango na gharama.
HATUA ILIYOCHUKULIWA NA SERIKALI KATIKA KUKABILIANA NA MAAFA
Katika siku za hivi karibuni kumekuwepo na juhudi za kujaribu kufanya
upotoshaji kuhusu hatua zilizochukuliwa na zinazoendelea kuchukuliwa
katika kukabiliana na maafa haya, Ukweli ni kwamba serikali kwa
kushirikiana na wadau imechukua hatua kubwa za kuwasaidia waathirika
ambapo miongoni mwao yafuatayo yameshafanyika:
Kutoa matibabu
bure kwa majeruhi wote 560, kuandaa na kugharamia mazishi ya watu 17
waliofariki ambapo Mheshimiwa Waziri Mkuu alihudhuria, Aidha serikali
kwa kushirikiana na wadau ilitoa mkono wa pole wa Shilingi Milioni 1.8
kwa kila familia iliyopatwa na msiba.
Kuendelea kutoa misaada
mbalimbali ya kibindamu ikiwemo chakula, Madawa, Nguo, Makazi ya muda,
Huduma za tiba, Vifaa vya shule na huduma ya ushauri wa kisaikolojia kwa
waathirika katika Wilaya zote za Mkoa wa Kagera zilizopata athari.
Kushirikiana na Ofisi ya Mwakilishi Mkazi mmoja wa Mataifa na wadau
mbalimbali wakiwemo Msalaba Mwekundu, Plan International (T), BRAC (T),
World Vision, CARITAS, Save the Childre, JH Piego na Benki ya Dunia
kufanya tathmini ya pamoja ya mahitaji ya haraka ya athari za Tetemeko
la ardhi ili kubaini maeneo zaidi ya kuwasaidia wananchi.
HATUA ZA KUREJESHA HALI
Tangu kutokea kwa maafa haya serikali imeendelea kufanyia kazi masuala
muhimu yaliyoainishwa katika tathmini ya Tetemeko ambapo hadi kufikia
tarehe 13 Novemba, 2016 licha ya kuendelea kuwapatia wananchi mahitaji
muhimu kama Chakula, Dawa na Misaada ya kujikimu katika makazi ya muda,
kiasi cha shilingi Milioni 969,238,326.35, Mifuko ya saruji 17,423, Bati
5,348 na Misumari Kilo 1,107 vilitumika kwa kufanya ukarabati mkubwa na
mdogo wa shule za msingi na Sekondari, Juhudi ambazo ziliwezesha
wanafunzi wa shule hizo waliokuwa katika hatari ya kukosa masomo
kuendelea na masomo yao.
Gharama hizo pia zimejumuisha ukarabati
wa zahanati katika Halmashauri za Mkoa wa Kagera na kuanza kwa ujenzi wa
kituo kipya cha afya (Ishozi/Kabyaile) kitakachojumuisha chumba cha
upasuaji wa wodi ya kina mama na watoto kwa faida ya wananchi wote wa
maeneo hayo. Pia serikali imegharamia urejeshwaji wa miundombinu ya
barabara, maji na umeme katika maeneo kadhaa yaliyoathiriwa na tetemeko.
Shirika la World Vision kwa kushirikiana na serikali mkoani Kagera,
tayari limetoa jumla ya mifuko ya saruji 2300 yenye thamani ya shilingi
milioni 39,000,000 kwa kaya 460 zilizobomolewa nyumba na zilizoonekana
kuwa na uhitaji zaidi ambapo katika awamu ya kwanza kila kaya ilipaa
mifuko mitano ya saruji na kwa sasa utekelezaji wa awamu ya pili umeanza
ambapo inatarajiwa kugawiwa mifuko ya saruji 10,645 yenye thamani ya
shilingi Milioni 164,997,000.00 kwa kaya 2,129.
Aidha tayari
serikali imeainisha kaya nyingine zilizoathirika zaidi zipatazo 370 za
watu waliomo kwenye makundi maalumu (Wazee, Wajane na Walemavu) ambao
watapatiwa vifaa vya ujenzi (Mabati 20 na mifuko 5 ya saruji kwa kila
kaya) kwa ajili ya kukarabati nyumba zao. Ugawaji kwa awamu ya kwanza
umeanza.
HITIMISHO
Haya ndio niliyoyabaini katika ziara
yangu nilipozuru Mkoani Kagera naishauri Serikali kuchukua hatua kali
dhidi ya wale wate waliokuwa wanapotosha watanzania dhidi ya matumizi ya
fedha hizi kwa makusudi kwa madai kwamba zimeliwa na serikali.
Lakini niwapongeze wananchi wote Mkoani Kagera ambao waliitikia wito wa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuitikia wito wa kuanza
ujenzi wa nyumba zao wao wenyewe huku serikali ikiunga mkono katika
maeneo baadhi kama ambavyo nimeeleza katika makala yangu.
Jamii
inapaswa kutambua kuwa hakuna serikali duniani ambayo inapanga Tetemeko
la ardhi litokee ili liwauwe wananchi wake bali ni majanga ya asili
ambayo kwa namna moja ama nyingine hayazuiliki.
Kwa wale wasomaji
wa Biblia Takatifu Ukisoma Mathayo 3:2 inasema ”Tubuni, Kwa maana
ufalme wa mbinguni umekaribi” Nami nawasihi WATUBU wale wote waliokuwa
wanapotosha kuwa hela za rambi rambi zimeliwa tena walipotosha bila kuwa
hata na Data wala Taarifa sahihi za Matumizi ya fedha hizo.
Wakati Mwema...!
Mathias Canal
0756413465
Mwanza
Post a Comment