Serikali yamfuta Kazi Kamishna mkuu wa TRA Rished Bade
.............................
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amemsimamisha kazi Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania Bw Rished Bade kufuatia kasoro kubwa za kiutendaji zilizobaini katika Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA.
Kasoro hizo ni pamoja na kuingizwa nchini kwa makontena zaidi ya 300 ambayo
hayajalipiwa ushuru na hivyo kusababisha upotevu wa zaidi ya shilingi bilioni
80 za mapato ya serikali.
Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue, amesema kufuatia kusimamishwa kazi
kwa Bw Bade, Rais Magufuli amemteua Dkt. Philip Mpango kuwa Kaimu Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato (TRA).
Kabla ya Uteuzi huo, Dkt. Mpango alikua Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango.
Pamoja na hatua hizo Balozi Sefue amesema Rais Magufuli ameagiza watu wote
ambao wanajijua kuwa wameingiza nchini makontena ya bidhaa mbalimbali pasipo
kulipa ushuru na kodi kama inavyopaswa waende wenyewe katika mamlaka ya Mapato Tanzania na kulipa ushuru unaopaswa.
Wakati huohuo Balozi Sefue amesema safari zote za wafanyakazi wa TRA nje ya
nchi zimefutwa kuanzia leo na badala yake amewataka wafanyakazi hao kutoa
ushirikiano wakati uchunguzi zaidi katika mamlaka hiyo ukiendelea.
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano,
IKULU
IKULU
27 Novemba, 2015
Post a Comment