Wananchi Watakiwa Kupima Afya Zao
Mkurugenzi wa Ufuatiliaji na Tathmini wa TACAIDS Dkt. Jerome Kamwela akiwaonesha waandishi wa Habari Bango lenye Takwimu za Hali ya Maambukizi ya VVU nchini Tanzania. | |
Na. Nyakongo Manyama - MAELEZO
Wito umetolewa kwa
wananchi kote nchini kuyatumia maadhimisho ya Siku ya UKIMWI duniani ambayo
huadhimishwa kila ifikapo Desemba 1 ya kila mwaka kupima afya zao ili kudhibiti
maambukizi mapya ya VVU.
Akizungumza na
waandishi wa Habari leo jijini Dar es salaam Mwenyekiti Mtendaji wa Tume ya Taifa ya
Kudhibiti UKIMWI nchini Tanzania Dkt. Fatma Mrisho amesema Siku ya Ukimwi Duniani nchini itaadhimishwa
kwa kuwahimiza wananchi kujitokeza kwa
wingi kupima afya zao na kupata elimu ya
kujikinga na maambukizi ya ugonjwa huo.
Ameeleza kuwa maadhimisho ya mwaka huu yataambatana na
shughuli mbalimbali zikiwemo za Utoaji wa Elimu ya Afya na Upimaji wa hiari wa
VVU katika maeneo mbalimbali kote nchini kupitia vituo vitakavyowekwa, Kufungua
kituo cha maarifa cha udhibiti UKIMWI eneo la Manyoni mkoani Singida ambayo ni
njia kuu kuelekea mikoa ya Kanda ya Ziwa na nchi za Jirani za Burundi na
Rwanda.
Ameongeza kuwa Tume kwa
kushirikiana na wadau mbalimbali itaendesha mikutano ya kitaalam kuhusu UKIMWI,
Zoezi la upimaji wa hiari wa VVU kwa wananchi, Kupokea tamko litakalotolewa na
Baraza la Watu wanaoishi na VVU pamoja na Uzinduzi wa taarifa ya tathmini ya
Sheria zinazotumika zinazohitaji
kurekebishwa zinazozuia malengo ya sifuri 3.
Aidha Tume itapokea taarifa ya hali ya
maambukizi ya VVU duniani itakayotolewa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban
Ki Moon kuhusu dunia na mapambano dhidi ya VVU.
Dkt. Fatma amefafanua kuwa
mgeni rasmi katika maadhimisho hayo anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.
John Pombe Joseph Magufuli ambapo pamoja na mambo mengine atazindua Mfuko wa
UKIMWI ambao utakuwa chachu ya kupunguza maambukizi ya VVU nchini.
Kwa upande wake
Mkurugenzi wa ufuatiliaji na tathmini kuhusu UKIMWI wa TACAIDS Dkt.Jerome Kamwela
amesema kuwa kiwango cha maambukizi ya UKIMWI kwa mujibu wa takwimu za mwaka
2011/2012 kimepungua na kufikia asilimia 5.3 huku mikoa ya nyanda za juu kusini
ya Njombe, Iringa na Mbeya ikiongoza kwa
kuwa na maambukizi zaidi na mikoa ya
Manyara, Tanga na Lindi ikiwa na maambukizi
ya chini ya asilimia mbili.
Dkt. Kamwela amesema
kuwa maambukizi ya VVU ni mengi hasa kwa kundi la watu wenye umri wa miaka
19-24 huku makundi ya wanaojidunga, wanaume wanaofanya mapenzi ya jinsia moja,
wanawake wanaofanya biashara ya ngono yakiendelea kuwa katika hatari ya
kuathiriwa zaidi na maambukizi ya VVU.
Post a Comment