Viongozi wa KIMILA wapitisha Azimio la Kumlinda Mtoto wa KIKE
Pichani
juu na chini ni baadhi ya viongozi wa mila (Laigwanan na Laiboni) na
akina mama mashuhuri (Ngaigwanan) wilayani Lolilondo wakisoma na
kujadili azimio la pamoja la kumlinda mtoto wa kike kabla ya kulipitisha
na kusaini wakati wa kongamano kubwa la siku mbili lililofanyika katika
ofisi za halmashauri ya wilaya Ngorongoro, jijini Arusha.
VIONGOZI
wa kimila wa jamii ya Kimaasai na wanawake mashahuri wamepitisha Azimio
la Loliondo lenye lengo la kumlinda mtoto wa kike na kuhakikisha
maendeleo yake kiafya, kielimu na kitamaduni.
Azimio
hilo ambalo limetiwa saini na viongozi hao mwishoni mwa kongamano kubwa
la siku mbili lililofanyika, katika ofisi za halmashauri wilayani
Ngorongoro, linapinga mila na desturi zinazomkandamiza mtoto wa kike.
Mila na desturi ambazo zimepitwa na wakati.
Kabla
ya kupitishwa na kusaini maazimio hayo viongozi hao wa kimila na
mashuhuri walipatiwa mafunzo ya kuwajengea uwezo ili kuendeleza mijadala
na uelewa na hatimae kuamini kwamba baadhi ya mila na desturi
zinachangia na kuchochea athari za kiafya na kijamii hasa kwa watoto wa
kike na kina mama.
Viongozi
hao wamepitisha azimio hilo baada ya kupitia kifungu hadi kifungu na
kuridhia yaliyomo kwa kuzingatia wajibu wao ndani ya jamii na uwezo
mkubwa wa ushawishi kama viongozi wa mila (Laigwanan na Laiboni) na
akina mama mashuhuri (Ngaigwanan) .
Aidha
walisema kwamba watatumia nafasi zao kuelimisha jamii juu ya malezi
bora ikiwa ni pamoja na mahali salama pa kulala watoto wa kike na kiume
na kuelimisha jamii umuhimu wa elimu kwa kuwapeleka shuleni hasa kwa
watoto wa kike.
“Naomba
viongozi wenzangu twende tukaelimishe jamii juu ya madhara ya tohara
kama tulivyoazimia na kuanzisha mchakato utakaosaidia kupunguza au
kumaliza kabisa matendo ya tohara ndani ya jamii yetu,” alisema
Mwenyekiti wa Baraza la Malaigwanan wilaya ya Ngorongoro, Joseph
Oletiripai.
Viongozi
hao pia wamesema ni vyema jamii ya kifugaji kuacha kuendelea na vitendo
vya kuwaoza watoto wa kike wakiwa bado wadogo na wakati mwingine kwa
kuwakatisha masomo na kuwalazimisha kuolewa.
......................................
“Sisi
kama viongozi tusiendelee kuwa chanzo cha kuendeleza matukio haya kwani
ni ya ukatili kwa watoto wetu wa kike na tutumie nafasi hii kwenda
kuwaelimisha viongozi wenzetu wengine mashuhuri ili kusambaza ujumbe na
jamii ijue athari zinazotokana na ukeketaji pamoja na kuozesha watoto
wetu wakiwa katika umri mdogo,” alisema Laanoi Munge.
Viongozi
hao pia wamedhihirisha kuwa matukio ya vitendo vya ukeketaji na ndoa za
utotoni vimechangia utoro nyumbani na kwenda kuishi kwa muda kwenye
vituo maalum kwa kuogopa kufanyiwa tohara.
Watoto
hao wamekuwa na hali ya kutoroka baada ya kugundua kwamba kuna matukio
ya ulemavu na athari nyinginezo za kiafya zinazotokana na ukeketaji na
salama yao ni kujitoa katika jamii hiyo na kutafuta hifadhi kwingine.
Azimio
hilo la Loliondo ambalo pia lilitiwa saini na waganga wa tiba asilia
limetoa mwelekeo wa kuboresha afya ya uzazi, elimu na malezi kwa watoto
wa kike katika jamii ya Kimaasai.
Aidha
limetoa namna bora ya utekelezaji na kupitisha taratibu zitakazosaidia
watoto wa kike wanaokimbia tishio la ukeketaji na kuhakikisha kwamba
watasoma na kupata huduma zote za afya.
Katika
maeneo yao baada ya kutia saini viongozi hao wameahidi kuonyesha
ushirikiano wa karibu kwa viongozi wa serikali katika ngazi zote,
viongozi wa dini, vyombo vya habari, walimu, wataalamu wa afya na wadau
wa maendeleo katika maeneo yote ndani ya wilaya ili kuboresha afya ya
uzazi, elimu na malezi bora kwa watoto.
Pamoja
utiaji saini wa Azimio la Loliondo,viongozi hao wameliomba shirika la
UNESCO na halmashauri ya wilaya ya Ngorongoro kushirikisha viongozi
wengi zaidi, kuendelea kutoa elimu kwa viongozi wa kimila na kuendelea
kuwasaidia katika majukumu yao ikiwa ni pamoja na kuwapa elimu na
kuwasaidia uratibu wa shughuli zote za kupingana na unyanyasaji na
ukatili wa kijinsia.
Katibu
wa Baraza la Mila (W) Ngorongoro, Laanoi Munge akisoma azimio la
kumlinda mtoto wake baada ya kulifanyia marekebisho ya pamoja mbele ya
viongozi wa mila wa wilaya ya Ngorongoro.
.........................................
Kongamano
hilo lililozaa Azimio la Loliondo ni mwendelezo wa warsha zinazotolewa
na UNESCO kwa ajili ya kutoa elimu ya kuwajengea uwezo na kugawa
majukumu kwa viongozi wa kimila, wamama mashuhuri, viongozi wa dini,
wakunga wa jadi pamoja na waandishi wa habari ili kutekeleza vizuri
ufuatiliaji wa afya ya uzazi na malezi bora kwa watoto katika jamii ya
Kimaasai.
Utiaji
saini wa Azimio la Loliondo ulishuhudiwa na Katibu Tawala Wilaya ya
Ngorongoro Bw. Lemuel Kileo, maafisa wa Shirika la Umoja wa Mataifa
linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) Bw.Herman Mathias
na Bi.Rose Haji Mwalimu.
Kongamano
hilo la siku mbili lililofanyika katika ukumbi wa halmashauri ya wilaya
ya Ngorongoro limeendeshwa na Shirika la Umoja wa Mataifa
linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kwa kushirikiana
na Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro.
Katibu
wa Baraza la Mila wilayani Ngorongoro, Laanoi Munge (kushoto
aliyesimama) akimsomea baadhi ya maboresho ya vipengele vilivyomo ndani
ya azimio hilo Ofisa Elimu ya Uzazi na UKIMWI kutoka UNESCO, Mathias
Herman (kulia).
Laigwanan wa kata ya Pinyinyi, Moses Mollel akiwasilisha maboresho ya azimio hilo baada ya kulijadili kabla ya kusaini.
Ofisa
Elimu ya Uzazi na UKIMWI kutoka UNESCO, Mathias Herman akifafanua jambo
kwa viongozi hao baada ya kuridhishwa na maboresho ya azimio hilo
katika kongamano kubwa la siku mbili lililofanyika katika ofisi za
halmashauri ya wilaya Ngorongoro, jijini Arusha. Kutoka kushoto
ni Mkalimani wa kwenye kongamano hilo Mchungaji, Mark Murenga, Katibu
Tawala wa Wilaya ya Ngorongoro, Lemuel Kileo, Mwenyekiti wa Baraza la
Malaigwanan wilaya ya Ngorongoro, Joseph Oletiripai pamoja na Kiongozi
wa Malaiboni wilaya ya Ngorongoro Bw. Sangau Naimodu.
Baadhi
ya waandishi wa habari kutoka redio ya jamii Loliondo FM nao walikuwepo
kuhudhuria tukio hilo la utiaji saini wa azimio la kumlinda mtoto wa
kike.
Baadhi ya maafisa wa halmashauri ya wilaya ya Ngorongoro na waandishi wa habari waliokuwepo ukumbini kushuhudia tukio hilo.
Mwenyekiti
wa Baraza la Malaigwanan wilaya ya Ngorongoro, Joseph Oletiripai
(kushoto), Kiongozi wa Malaiboni wilaya ya Ngorongoro Bw. Sangau Naimodu
(wa pili kushoto) Laigwanan wa kata ya Pinyinyi, Moses Mollel (wa pili
kulia) pamoja na Ngaigwanan wa Malambo, Miriam Lembirika wakisaini kwa
niaba ya viongozi wengine wa mila wa Wilaya ya Ngorongoro, Azimio la
Liliondo.Wanaoshuhudia (waliosimama) ni KatibuTawala wa Wilaya ya
Ngorongoro, Lemuel Kileo (kulia), Ofisa Ustawi wa Jamii wa halmashauri
ya wilaya ya Ngorongoro, Benezeth Bwikizo (wa pili kulia), Mtaalamu wa
masuala ya vyombo vya habari vya kijamii na Mkufunzi kutoka UNESCO,
Rose Haji Mwalimu (wa tatu kulia) pamoja na Ofisa Elimu ya Uzazi na
UKIMWI wa UNESCO, Mathias Herman.
Walioshuhudia tukio hilo wakipiga makofi baada ya zoezi hilo.
Baadhi ya viongozi wa kimila na waandishi wa habari wakishuhudia tukio hilo la kusainiwa kwa azimio la kumlinda mtoto wa kike.
Zoezi
la utiaji saini likiendelea kwa kila kiongozi aliyeshiriki kongamano
kubwa la siku mbili lililoandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa
linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) ambalo
limefanyika katika ofisi za halmashauri ya wilaya Ngorongoro, jijini
Arusha.
Picha ya pamoja baada ya zeozi kukamilika.
Post a Comment