Makamu wa Rais SAMIA SULUHU Akutana na Uongozi wa Mtandao wa Wanawake TANZANIA
TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
Makamu wa Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan leo amekutana na uongozi wa
Mtandao wa Wanawake na Katiba Tanzania (WFT) ambapo amezungumzia dhamira ya
serikali katika kuyatafutia ufumbuzi matatizo mbali mbali yanayowakabili
wanawake na watoto wa kike nchini.
Katika mazungumzo hayo
Makamu wa Rais aliueleza ujumbe huo kuwa wakati wa kampeni aliahidi pamoja na
kazi za kumsaidia Mhe. Rais bado kama mama atafuatilia kwa karibu utekelezaji
wa ahadi ya kupatikana kwa maji safi na salama, kuboresha afya ya mama na
mtoto, elimu na mazingira.
“Nilipokuwa kwenye kampeni
nimejionea shida ya maji na wanawake ndiyo wanaopata tabu ya kutembea mwendo
mrefu kutafuta maji.
Kwa hiyo, pamoja na kazi zangu za kumsaidia Mhe. Rais
nitasimamia miradi yote ya maji, alau tuhakikishe maji yanapatikana umbali wa
mita 400 kutoka eneo wananchi wanakoishi au karibu zaidi”.
Alisema kinachofurahisha
zaidi suala la maji liko kwenye Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) na miradi
mingi ikiwemo ya kuchimba visima virefu katika mikoa kama vile ya Singida na
Dodoma iko kwenye mchakato na cha msingi ni kusimamia fedha zinatumika kuleta
maji kama ilivyokusudiwa.
Kuhusu afya ya mama na mtoto
alisema kazi hiyo ataianza hivi karibuni kwa kushirikiana na Mashirika yasiyo
ya kiserikali yanayotetea haki za wanawake ili kupunguza vifo vinavyosababishwa
na mimba za utotoni.
“Hili tutajitahidi
kulipunguza kwa kiasi kikubwa na hasa baada ya serikali ya Awamu ya Nne kusema
kwamba shule ya msingi ya lazima ni kutoka darasa la kwanza hadi kidato cha
nne”, alisema na kuongeza.
“Katika kipindi hicho binti
atakuwa amefikisha miaka 17, atakuwa tayari kukabiliana na mambo ya uzazi
tofauti na ilivyo sasa ambapo anamaliza darasa la akiwa mdogo na matokeo yake
anapata mimba katika umri mdogo. Mtusaidie kupiga debe huko nje utekelezaji
uweze kufanikiwa.”
Hata hivyo, alisisitiza
kusimamia suala la kuhakikisha zahanati, vituo vya afya na hospitali nchini
zinakuwa na dawa na vifaa tiba vya kutosha katika wodi za wazazi kwa ajili ya
kuhudumia akina mama na wananchi kwa ujumla ambao wengi wanaonekana ni watiifu
kwa serikali yao.
Kwa upande wa elimu Mhe.
Samia alisema atasimamia ujenzi wa mabweni kwa watoto wa kike na kuhakikisha
mazingira yanatunzwa kwa sababu uharibifu wa mazingira ndiyo umekuwa chanzo cha
upungufu wa maji nchini.
Aidha aliuambia ujumbe huo
kuwa hivi sasa tuna mpango wa kuimarisha utendaji serikalini kuanzia serikali
kuu hadi serikali za mitaa ili kinachopatikana kidogo kimfikie kila mwananchi.
“Tutaendelea kuaihirisha
sherehe ili fedha hizo ziweze kutumika kwa mambo ya kijamii. Kwa msimamo huu
amabao Mhe. Rais ameanza nao labda watu wote tushirikiane kwa kutatua matatizo
yetu kwa gharama nafuu kwa ufanisi mkubwa.”
Mapema akizungumza kwa
niaba ya wenzake Mwenyekiti wa Mtandao huo Prof Ruth Meena alimpongeza Mhe.
Samia kwa kushika nafasi ya juu ya uongozi akiwa mwanamke wa kwanza kuweka
historia katika Tanzania.
Alimweleza Mhe. Makamu wa
Rais matarajio yao kwa serikali ya Awamu ya Tano kuwa itatetea misingi ya haki
na usawa katika Nyanja zote.
Imetolewa na Ofisi ya
Makamu wa Rais
Dar es salaam
24/11/2015
Post a Comment