Naibu Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani amewahakikishia wananchi wa
Wilaya za Kibiti, Rufiji na Mafia kuwa ujenzi wa gati la kisasa katika eneo la
Nyamisati utaanza wakati wowote baadaye mwakani na kukamilika ifikapo Machi
2018.
Akizungumza mara baada
ya kukagua eneo litakapojengwa gati hilo katika pwani ya Nyamisati wilayani
Kibiti Eng.Ngonyani amewataka viongozi na wananchi wa wilaya hizo kuwa na
uvumilivu katika kipindi hiki ambacho Serikali inatafuta ufumbuzi wa kudumu.
“Endeleeni kutunza
mazingira ya eneo hili na kutunza mazingira ya bahari ili kudhibiti mabadiliko
ya tabia nchi katika eneo lenu, Serikali imejipanga kukabiliana na changamoto
inayowakabili sasa hivyo toeni ushirikiano unaohitajika ili kuiwezesha Mamlaka
ya Bandari nchini(TPA) kutekeleza ujenzi wa gati hili”. Amesisitiza Eng.
Ngonyani.
Naye Mbunge wa Mafia
Mhe. Mbaraka Dau amemhakikishia Naibu Waziri Ngonyani kuwa kukamilika kwa gati
la kisasa katika pwani ya Nyamisati kutahuisha shughuli za kiuchumi kwa
wakazi wa Mafia na Mkoa wa pwani kwa
ujumla.
“Kukamilika kwa gati
hili kutavutia wasafirishaji wengine kuleta vyombo vya usafiri na hivyo
kushusha gharama za usafiri kati ya Kibiti na Mafia ambapo sasa ni zaidi ya
shilingi elfu kumi na tatu kwa safari”. Amesema Mhe. Dau.
Katika hatua nyingine
Naibu Waziri Ngonyani amekagua barabara ya Ikwiriri-Lindi, Nanyumbu
–Masugulu-Mtambaswala na Mangaka -Tunduru na kumtaka Meneja wa Wakala wa
barabara Mkoa wa Mtwara Eng.Dotto Chacha kuhakikisha barabara inakuwa salama
wakati wote kwa kudhibiti madereva wanaoegesha magari barabarani isivyostahili.
Naibu Waziri Ngonyani
yupo katika ziara ya kukagua Miundombinu ya barabara, Bandari na Mawasiliano
katika mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma.
|
Post a Comment