Naibu Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Anastazia Wambura akizungumza na waandishi wa habari wadau wa harakati za upatikanaji wa lishe bora nchini na wahariri wa vyombo vya habari katika hafla ya kuwatunuku tuzo waandishi bora wa masuala ya lishe nchini iliyofanyika Jijini Dar es Salaam Novemba 22,2016.
.......................................
Na Raymond Mushumbusi WHUSM
Serikali imeahidi kutenga jumla ya Dola za kimarekani Millioni 115 kwa ajili ya kuboresha lishe ikiwa ni mpango wa maendeleo wa miaka mitano 2016/2021 na mkakati wa kuboresha lishe kwa mwaka 2016/2021.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Anastazia Wambura alipokuwa akizungumza katika halfa ya kuwatunuku tuzo waandishi bora wa habari zinazohusu lishe iliyofanyika leo Jijini Dar es Salaam.
Mhe. Anastazia Wambura ameongeza kuwa bado kumekuwa na changamoto katika upatikanaji wa lishe bora nchini ikiwemo kuwepo kwa tamaduni mbalimbali zinazonyima fursa kwa watoto na wakina mama kupata lishe iliyo bora.
“Serikali imeingiza suala la lishe katika mpango wa maendeleo wa taifa wa miaka mitano na katika kulitekeleza hili Serikali ya awamu ya Tano itatenga dola million 115 kwa ajili ya mkakati wa kuboresha lishe nchini” alisisitiza Mhe. Anastazia.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Jukwaa la Lishe Tanzania(PANITA) Bw. Tumaini Mkindo amesema kuwa hali ya lishe imeendelea kuimarika hasa kwa miaka mitano iliyopita hili linadhihilisha kuwa mikakati thabiti iliyopo imesaidia kwa asilimia kubwa kupambana na tatizo la ukosefu wa lishe bora nchini.
Bw. Mkindo ameipongeza Serikali kwa juhudu inazozichukua katika kupanga mikakati na kuitekeleza katika suala la upatikanaji wa lishe bora nchini ili kuondokana na suala la udumavu linaloleta athari kubwa katika ukuaji wa Binadamu.
Ameongeza kuwa Jukwaa la Lishe Tanzania litaendelea kushirikiana na Serikali na wadau wengine katika harakati za upatikanaji wa lishe bora na kufikia malengo ya Shirika la Afya Dunia (WHO) yaliyosainiwa na Tanzania yahusuyo masuala ya lishe pamoja na kupunguza udumavu kwa asilimia 40 ifikapo mwaka 2025.
|
Post a Comment