Serikali Imesema Itaendelea Kuvifutia Usajili Vyuo ambayo Havina Sifa
Na Dotto Mwaibale
Serikali imesema itaendelea kuvifutia usajili vyuo vyote vya taaluma mbalimbali ambavyo havikidhi viwango nchini.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia Dk. Leonard Akwilapo wakati akihutubia katika mahafali ya 11 ya Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Dar es Salaam jana.
"Wizara kupitia Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) na Baraza la Taifa la Mafunzo ya Ufundi (NACTE) inaendelea na mchakato wa tathmini ya vyuo vyote kuanzia vyuo vikuu hadi vyuo vya ngazi ya kati ili kubaini ubora wake" alisema Dk. Akwilapo.
Alisema Serikali inaangalia ubora wa Wahadhiri na Wakufunzi, miundombinu ya chuo husika kama inakidhi utoaji wa elimu bora na usimamizi na utaratibu wa masomo katika vyuo hivyo na kila kitu kilicho katika mahitaji ya kufanya chuo kitoe elimu bora.
Alisema kwa lengo la kusimamia utoaji bora wa elimu serikali haitasita kukiondolea usajili chuo chochote ambacho kitadhihirika kutokuwa na sifa za kukifanya kiwe chuo na kuwa mchakato huo utafanyika kwa kufuata taratibu za kisheria na kwa uwazi.
Dk. Akwilapo alisema uamuzi huo wa Wizara utakuwa endelevu na hautaishia katika Vyuo tu bali utateremka mpaka kufikia katika ngazi ya shule za msingi lengo likiwa ni kuhakikisha kuwa katika miaka michache ijayo tunaondokana na suala la kuwa na taasisi uchwara katika mlolongo mzima wa utoaji elimu hapa nchini.
Alisema katika suala hilo Baraza la Taifa la Mafunzo ya Ufundi wiki chache zilizopita ilifuta baadhi ya vyuo ambavyo vilikuwa havikidhi matakwa ya usajili wao.
"Napenda kutamka wazi kwamba kama unaona huwezi kuendesha taasisi inayotoa elimu kwa ubora unaotakiwa basi nenda kawekeze fedha zako kwenye sekta nyingine sio elimu kwani imetosha sasa. Na huko kwingine uwe makini vilevile kwa sababu nako huko utatimuliwa pia" alisema Akwilapo.
Aliongeza kuwa mchakato huo hautaishia kwa vyuo pekee badi na kuangalia udahili wa wanafunzi katika vyuo vya ngazi ya kati na vyuo vikuu na sifa zao na kuwa mchakato huo utafanyika na kwa wakufunzi.
Mkuu wa chuo hicho, Profesa Shadrack Mwakalila alisema idadi ya wahitimu imeongezeka kutoka wahitimu 567 mwaka jana hadi kufikia wahitimu 1013 mwaka huu abapo katika kampasi ya Kivukoni idadi ya wanafunzi imeongezeka sana katika kipindi cha mwaka wa masomo 2016/2017 na kufikia wanafunzi 5,000 ukilinganisha na wanafunzi 1517 katika mwaka 2014/2015.
Akizungumzia katika kampasi ya Zanzibar alisema idadi imeongezeka hadi kufikia wanafunzi 900 ukilinganisha na wanafunzi 22 katika mwaka wa masomo 2014/2015 na kuwa hali hiyo inaonesha dalili njema kwa chuo jinsi gani wananchi walivyo na imani na ubora wa mafunzo yanayotolewa na chuo hicho.
Picha mbalimbali zikichukuliwa.
Maandamano ya wanafunzi kuelekea eneo maalumu la mahafali hayo yakifanyika.
Maandamano yakiendelea.
Mkuu wa Idara ya Uchumi wa chuo hicho, DK. Venance Mutayoba akizungumza katika mahafali hayo.
Mkuu wa Idara ya Ualimu Dk. Bertha Losioki akizungumza.
Mkuu wa Idara ya Jinsia katika chuo hicho, Dk. Patricia Mwesiga akizungumza.
Post a Comment