Milioni 10 za Ujenzi wa Choo Zayeyuka Manispaa ya Temeke, Dar es Salaam
Choo cha Soko la Madenge katika Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam kikiwa kimeng'olewa milango kutokana na kutokamilika ujenzi wake licha ya manispaa hiyo kutenga sh.milioni 10 za ujenzi.
Mkazi wa Temeke akipita mbele ya choo hicho.
Mwonekano wa moja ya tundu la choo hicho ambacho hakina miundombinu ya mifereji.
Na Dotto Mwaibale
SHILINGI milioni 10 zinazodaiwa kutolewa na Halmshauri ya Manisaa ya Temeke kwa ajili ya ujenzi wa choo katika Soko la Madenge hazijulikani zilipo hivyo kuzua tafrani kwa wananchi.
Wananchi hao wamelalamikia kukosa choo katika soko hilo kwa zaidi ya miaka mitano licha ya kutengwa kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya ujenzi wa choo hicho.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na mtandao huu, wananchi hao walisema wanalazimika kutumia choo cha kulipia baada ya choo cha soko hilo kilichoanza kujengwa kushindwa kumalizika.
Mmoja wa wafanyabiashara wa soko hilo ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe alisema Manispaa ya Temeke ilitenga fedha hizo kwa ajili ya ujenzi wa choo hicho lakini kwa muda wa miaka mitano ujenzi wake haujakamilika.
Hali hiyo inaleta adha kwa wafanyabiashara kwa kuendelea kulipia huduma za choo kilichopo sokoni hapo kinyume cha matarajio yao.
" Hii ni hujuma au matumizi mabaya ya fedha kwa nini ujenzi wa choo umeishia njiani licha ya fedha kutolewa na Manispaa na kibaya zaidi baadhi ya miundombinu kama milango imeng'olewa hivyo kubaki kama gofu" alihoji.
Akitoa ufafanuzi wa malalamiko hayo Ofisa Masoko wa Wilaya ya Temeke, Johnson Makalanga alikiri kuwepo kwa jambo hilo na kuwa limetokana na mkandarasi aliyepewa tenda ya ujenzi wa choo hicho kukomea njiani kwa kuwa fedha zake hakumaliziwa.
"Ninachofahamu mimi Changamoto kubwa iliyosababisha kutokamilika kwa ujenzi huo ni mkandarasi kucheleweshewa fedha zake kwani anadai sh.milioni 4" alisema Makalanga.
Makalanga aliongeza kuwa ujenzi wa vyoo hivyo ilikuwa ni kwa baadhi ya masoko ya wilaya hiyo ambapo yeye alisimamia kujenga choo kilichopo kwa Urasa Kigamboni ambacho kinatoa huduma na kuingiza mapato yanayotokana na wananchi kuchangia fedha baada ya kupata huduma za choo hicho.
Makalanga alisema hawezi kulizungumzia suala hilo kwa mapana kwa vile ni hayupo kwa muda mrefu katika kata hiyo badala yake aliomba atafutwe ofisa Mtendaji au Diwani wa Kata ya Temeke kwa ufafanuzi zaidi.
Jitihada za gazeti hili kumpata mtendaji wa kata hiyo ziligonga mwamba baada ya kufika ofisini kwake jana na kuambiwa alikuwa kwenye kikao na watendaji wake.
Post a Comment