Na FATMA SALUM -MAELEZO
Jumla ya wadaiwa wapya 21,721
wa mikopo ya elimu ya juu wamejitokeza ili kuanza kulipa madeni yao kufuatia
agizo la siku 60 lililotolewa na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu
(HESLB) mnamo Machi 14 mwaka huu.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi
wa Urejeshaji Mikopo kutoka Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB)
Bw. Robert Kibona wakati akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam kuhusu
tathmini ya agizo lililotolewa na bodi
hiyo kwa wanufaika wa mikopo na waajiri ili kutimiza wajibu wao kisheria.
Bw. Kibona alifafanua kuwa
jumla ya Shilingi bilioni 151.5 zinatarajiwa kurejeshwa na wadaiwa hao ambao
walikopeshwa ili kuwawezesha kupata elimu yao ya juu katika vyuo mbalimbali
ndani na nje ya nchi kuanzia mwaka 1994.
|
Mkurugenzi wa Urejeshaji Mikopo
kutoka Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) Bw. Robert
Kibona akiongea na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu utekelezaji wa
agizo la siku 60 kwa wadaiwa wa Bodi hiyo na waajiri, ambapo takribani asilimia
72 ya wadaiwa wote wameshawasilisha taarifa zao. Kulia ni Meneja Habari, Elimu
na Mawasiliano wa Bodi hiyo.
|
|
Mkurugenzi Msaidizi Habari, Elimu na
Mawasiliano kutoka Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB)
Bw. Cosmas Mwaisobwa (kushoto) akieleza kwa
waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu utaratibu wa urejeshaji wa
mikopo kwa wadaiwa ambao mikopo yao imeshaiva. Kulia ni Mkurugenzi wa
Urejeshaji Mikopo kutoka Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu
(HESLB) Bw. Robert Kibona.
|
|
Baadhi
wa waandishi wa habari wakifuatiliaa mkutano huo. ...........
“Lengo la agizo lilikuwa ni kuhahakisha madeni yote
yaliyoiva yanakusanywa ili kuongeza uwezo wa kukopesha watanzania wengi zaidi
na agizo hili limeisha Mei 13 mwaka huu.” alisema Bw. Kibona.
Kwa mujibu wa Bw. Kibona, kati ya wadaiwa
waliopatikana, wadaiwa 19,528 walipatikana baada ya Bodi kuchambua taarifa za
waajiriwa zilizowasilishwa na waajiiri na wadaiwa wengine wapatao 2,007
walijitokeza kwa hiari.
“Waajiri wana wajibu wa kisheria wa kuwasilisha
taarifa za waajiriwa wao, baadhi yao walifanya hivyo katika siku hizo sitini na
tukawabaini wadaiwa hao, tunawapongeza waajiri kwa ushirikiano walioutoa na
wanufaika wote waliojitokeza kwa hiari” alisema Bw. Kibona.
Aidha Bw.
Kibona aliongeza kuwa Bodi imeongeza siku 30 za ziada kuanzia Mei 20, 2016 kwa
wadaiwa waliobaki kujitokeza na uamuzi huo umetokana na tathmini iliyoonyesha
kuwa kuna idadi kubwa ya waajiri na wanufaika wanaoendelea kujitokeza.
Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi Habari, Elimu na
Mawasiliano wa Bodi ya Mikopo Bw. Cosmas Mwaisobwa alisema kuwa kiwango cha
ukusanyaji wa madeni kwa mwezi kinatarajiwa kuongezeka kutoka shilingi bilioni
2.7 zinazokusanywa hivi sasa na kufikia shilingi bilioni 8 ifikapo mwezi Juni
2016.
Katika kipindi cha mwaka 1994/1995 hadi sasa, kiasi cha shilingi
trilioni 2.44 kimetolewa kwa wanufaika 378,504 wakiwemo wanafunzi wanaoendelea
na masomo yao hivi sasa ambao kwa sasa hawana wajibu wa kulipa hadi pale
watakapomaliza au kusitisha masomo yao.
|
Post a Comment