Serikali yawezesha Vikundi 1,200 vya Wakulima kupata Masoko
Na Raymond Mushumbusi MAELEZO
Serikali imefanikiwa kuwezesha vikundi 1200 vya wakulima wadogo wadogo nchini ili kupata masoko ya uhakika ya mazao yao wanayozalisha.
Akizungumza kuhusu mradi wa kuboresha miundombinu ya masoko,uongezaji wa thamani na huduma za kifedha vijijini (MIVARF) Mratibu wa Taifa wa Mradi huo Bw. Walter Swai amesema malengo ya mradi huo ni kuongeza kipato cha wakulima na uhakika wa chakula kwa kutengeneza miundombinu ya upatikanaji wa masoko kwa wakulima kwa kuboresha barabara za kutoka mashambani kuelekea sokoni na kuwapa taarifa sahihi kuhusu masoko na mahitaji yake.
Bw Walter Swai ameongeza kuwa lengo la mradi ni kufikia vikundi 1,600 kwa nchi nzima katika kutoa elimu ya kuwezesha wakulima kupata masoko ya mazao yao ikiwa ni jitihada za Serikali kuwawezesha wakulima hao kujikwamua kiuchumi.
“Nia yetu ni kufikia vikundi 1,600 katika mikoa yote Tanzania Bara na Visiwani na hadi sasa tumefika asilimia 75 ya lengo tulilojiwekea la kuwawezesha wakulima wadogo kupata masoko ya mazao yao” alisema Bw.Swai.
Naye Mtaalamu wa Masoko ya mazao ya kilimo wa MIVARF Bw. Muhoni Leonard amesema kuwa mradi huo utasaidia kuwapa wakulima taarifa sahihi juu ya masoko na mahitaji yake na kupunguza gharama ambazo zilikuwa zinatumika kwa ajili ya kupata taarifa hizo kutoka kwa madalali.
“Azma ya mradi huu ni kubadili muundo na utendaji wa wakulima wadogo kuongeza ufanisi katika uzalishaji na upatikanaji wa masoko ya mazao husika” alisistiza Bw Leonard.
Aidha, mmoja wa wakulima na msindikaji wa mchele kutoka Wilaya ya Chato mkoani Geita Bw.Joseph Nchimani amesema kuwa elimu aliyoipata kutoka MIVARF imemuwezesha kuendesha kilimo cha mpunga kwa njia ya kisasa ambayo imemuwezesha kuongeza thamani ya mchele kwa kuufunga kwenye mifuko iliyo katika hali ya
ubora unaokubalika kwenye soko.
“Kabla ya kuanza kufunga mchele kwenye mifuko nilikuwa nauza jumla ya tani mbili mpaka kumi kwa mwaka ila baada ya MIVARF kuja na kunipa elimu hii nimeweza kuuza mpaka kufikia tani 50 kwa mwaka” alisistiza Bw.Nchimani.
Program hiyo ya MIVARF inajushughulisha pia na kutoa huduma za kifedha vijijini ambayo ni ya miaka saba inayotekelezwa kwa mikoa 30 ya Tanzania Bara na Visiwani na inasimamiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu.
Post a Comment