Na Teresia Mhagama
Watendaji
kutoka Chuo cha Ukamanda na Unadhimu cha nchini India (NDC) wameupongeza Wakala
wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA) kwa umakini wake katika Usimamizi na Ukaguzi
wa Shughuli za uzalishaji na Biashara ya Madini nchini, ambazo zimeifanya Serikali kupata mapato stahiki kutokana na
rasilimali hiyo.
Pongezi
hizo zimetolewa na Kiongozi wa Ujumbe kutoka Chuo hicho Admiral D. M Sudan, katika kikao
kilichofanyika Makao Makuu ya Wizara ya Nishati na Madini jijini Dar es Salaam
ambapo Ujumbe huo ulikutana na watendaji wa Wizara na TMAA wakiongozwa na
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa Justin Ntalikwa.
Ujumbe
huo kutoka nchini India uliofika Wizara ya Nishati na Madini ili kujifunza
namna Wakala huo unavyosimamia shughuli za uzalishaji na biashara ya madini nchini,
ulieleza kuwa TMAA inafanya kazi nzuri
kwani imekuwa ni mwangalizi wa madini nchini hasa katika juhudi zake za
udhibiti wa utoroshaji wa madini kwenda nje
ya nchi.
|
Kaimu Mkurugenzi wa Ukaguzi na Udhibiti wa Uzalishaji na Biashara ya Madini, Mhandisi Godfrey Kasekenya Kutoka Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA),( aliyesimama), akifafanua jambo katika Kikao kilichohudhuriwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa Justin Ntalikwa (wa kwanza kushoto) na Ujumbe kutoka Chuo cha Ukamanda na Unadhimu cha nchiniIndia (NDC) ulioongozwa na Admiral DM Sudan
(hayupo pichani). Kushoto kwa Katibu Mkuu ni Kaimu Kamishna wa Madini, Mhandisi
John Shija. |
|
Katibu
Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa Justin Ntalikwa (kulia) akikabidhiwa
Ngao ya Chuo cha Ukamanda na Unadhimu cha nchini India ambayo alikabidhiwa na
Admiral DM Sudan (kushoto). Ujumbe kutoka Chuo hicho ulifika katika Wizara ya
Nishati na Madini ili kujifunza masuala ya ukaguzi wa madini.
|
|
Katibu
Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa Justin Ntalikwa (katikati) akiwa
katika kikao na Ujumbe Chuo cha Ukamanda na Unadhimu cha nchini India
(NDC)ulioongozwa na Admiral DM Sudan (Kulia kwa Katibu Mkuu). Ujumbe huo
ulifika katika Wizara ya Nishati na Madini ili kujifunza masuala ya ukaguzi wa
madini. Kushoto kwa Katibu Mkuu ni Kaimu Kamishna wa Madini, Mhandisi John Shija.
|
|
Meneja
wa Mipango na Utafiti Kutoka Wakala wa
Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA), Julius Moshi, (aliyesimama), akielezea shughuli za Wakala huo mbele ya
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa Justin Ntalikwa (katikati)
na Ujumbe kutoka Chuo cha Ukamanda na Unadhimu cha nchini India (NDC)
ulioongozwa na Admiral DM Sudan (hayupo pichani). Kushoto kwa Katibu Mkuu ni
Kaimu Kamishna wa Madini, Mhandisi John Shija.
|
|
Mkurugenzi
wa Usimamizi wa Mazingira na Ukaguzi wa Mazingira Migodini, Emanuel Sumay
Kutoka Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA),(aliyesimama), akifafanua
jambo katika Kikao kilichohudhuriwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na
Madini, Profesa Justin Ntalikwa (wa kwanza kushoto) na Ujumbe kutoka Chuo cha
Ukamanda na Unadhimu cha nchini India (NDC) ulioongozwa na Admiral DM Sudan
(hayupo pichani). Kushoto kwa Katibu Mkuu ni Kaimu Kamishna wa Madini, Mhandisi
John Shija.
..................................
|
Awali, Meneja wa Mipango na Utafiti wa TMAA, Julius
Moshi aliueleza Ujumbe huo kuhusu shughuli mbalimbali zinazofanywa na Wakala
huo ikiwemo ukaguzi wa shughuli za
uzalishaji na mauzo ya dhahabu kutoka kwa wazalishaji wanaotumia teknolojia ya
“vat leaching” katika kuchenjua
marudio ya dhahabu katika mikoa ya Mbeya, Mwanza na Geita.
Alisema
kuwa katika kipindi cha Julai 2015 hadi Machi 2016, jumla ya kilo 1,114.49 za
dhahabu zenye thamani ya Shilingi Bilioni 73.5 zilizalishwa na Mrabaha wa Shilingi Bilioni 2.9 kulipwa serikalini kutokana na shughuli hizo za
uchenjuaji madini.
“Siyo hivyo tu, TMAA pia tumejikita katika kudhibiti Utoroshaji na
Biashara Haramu ya Madini ambapo kazi hii tunatekeleza kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi, Mamlaka ya
Mapato Tanzania (TRA), Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA), Idara ya Madini na
Usalama wa Taifa kwa kufanya ukaguzi kupitia madawati maalum yaliyopo katika
viwanja vya ndege vya Julius Nyerere (Dar es Salaam), Kilimanjaro, Mwanza,
Songwe (Mbeya) na Arusha,”,” alisema Moshi.
Alisema kuwa
katika kipindi cha mwezi Julai 2015 hadi
Januari 2016, ukaguzi uliofanyika kupitia madawati yaliyopo katika viwanja
hivyo vya ndege, umewezesha kukamatwa
kwa watoroshaji wa madini katika matukio 16 yaliyoripotiwa ambayo yalihusisha madini yenye thamani ya Shilingi bilioni 3.2.
Aidha
Moshi alisema kuwa Wakala huo pia umeweka Wakaguzi katika migodi yote mikubwa
nchini ambapo juhudi hizo zimezaa matunda kwani Ukaguzi uliofanywa na TMAA kwa
kushirikiana na TRA umewezesha baadhi ya kampuni za uchimbaji madini kuanza
kulipa kodi ya mapato ambapo katika kipindi cha mwaka 2009 hadi Machi 2016,
kampuni mbalimbali zimelipa jumla ya Shilingi bilioni 680.5 kama kodi ya
mapato.
Vilevile,
alisema kuwa Wakala huo umekuwa ukifanya ukaguzi wa mara kwa mara wa shughuli
za ukarabati na utunzaji wa mazingira katika maeneo ya migodi mikubwa, ya kati
na midogo ambapo Wahusika wamekuwa wakipewa maelekezo yenye lengo la kuboresha
hali ya mazingira kwenye maeneo yao, suala lililopelekea kuimarika kwa shughuli za utunzaji wa
mazingira nchini katika maeneo ya migodi mikubwa, na baadhi ya migodi ya kati
na midogo nchini.
Awali, Katibu
Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa Justin Ntalikwa aliukaribisha
Ujumbe huo kutoka nchini India na kukishukuru Chuo hicho kwa kuamua kujifunza
masuala ya ukaguzi wa madini nchini kwani suala hilo limepelekea pande zote
mbili kujadiliana na kutoa maoni yatakayoboresha Sekta ya Madini katika nchi za
India na Tanzania.
Aidha, alitumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji
mbalimbali kutoka nchini India kuwekeza katika uzalishaji umeme nchini kwa
kutumia vyanzo mbalimbali kama gesi asilia na Nishati jadidifu ili kuweza kuwa
na umeme wa kiasi cha megawati 10,000 ifikapo mwaka 2025.
Post a Comment