TAWLA yasisitiza Mabadiliko ya Sheria za Usalama Barabarani
Jonas
Kamaleki-Maelezo
Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini,
Kamanda Mohamed Mpinga amesema mabadiliko ya sheria ya usalama barabarani
hayaepukiki ili kupunguza vifo na majeruhi vitokanavyo na ajali za barabarani.
Kamanda Mpinga amayesema hayo leo jijini Dar es
Salaam wakati wa Uzinduzi wa Programu ya Usalama Barabarani inayoratibiwa na Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA)
kwa kushirikiana na wadau mbali mbali wa Usalama Barabarani.
“Sheria zinazohusu masuala ya Usalama barabarani
inabidi zifanyiwe marekebisho ili ziweze kusaidia kupunguza vifo na majeruhi
kwani zilivyo sasa hazitoi adhabu kali kwa wanaokiuka sheria hizo”alisema
Kamanda Mpinga.
Aidha Kamanda huyo alisisitiza kuwa suala la
Usalama Barabarani ni la kila mmoja hivyo inabidi litiwe mkazo na watu wote.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa TAWLA, Bi Tike
Mwambipile amesema chama hicho kwa kuzingatia umuhimu wa kushughulikia masuala
ya Usalama Barabarani kimeona ni vyema kikafanya kikao hicho ili kupata mawazo
ya wadau.
Bi Mwambipile amesema vifo vingi vinavyotokana na
ajali za barabarani vinawaacha wanawake wengi wakiwa wajane na watoto yatima
wanaongezeka.
Ameongeza
kuwa fedha nyingi zinatumika kuwahudumia majeruhi badala ya kufanya shughuli
nyingine za maendeleo ya jamii.
Naye Mwenyekiti wa TAWLA, Bi Aisha Bade amesema
mabadiliko makubwa ya sera na sheria za usalama barabarani ni lazima yafanyike ili kupunguza athari
zitokanazo na ajali za barabarani.
Bi Bade amesema TAWLA kwa kushirikiana na wadau
wengine inafanya juhudi za makusudi ili kuhakikisha sheria hizi zinabadilishwa
ili kukabiliana na janga hili.
Visababishi vya ajali kwa hapa nchini vimetajwa na
Mratibu wa Mradi Bloomberg wa Usalama Barabarani, Bi Mary Kessy kuwa ni ulevi,
kutofunga mkanda, kutoweka vizuizi vya watoto kwenye magari, mwendo kasi na
kutovaa kofia ngumu kwa waendesha pikipiki.
Post a Comment