Serikali yatoa Tamko Siku ya Kupiga Vita Matumizi ya Tumbaku
Ndugu Wananchi,
Siku ya kupinga matumizi ya Tumbaku Duniani, huadhimishwa duniani kote kila mwaka tarehe 31 Mei.
Kaulimbiu ya Maadhimisho ya Siku ya kupinga matumizi ya tumbaku mwaka 2016 ni “jiandae kwa pakiti zisizo na matangazo wala vivutio”.
Kauli mbiu hii inalenga kuhamasisha jamii juu ya kujiepusha au kujikinga na vivutio mbalimbali vya matangazo yanayo hamasisha matumizi ya sigara ambayo ina madhara mengi kiafya.
Tanzania kama zilivyo nchi nyingine duniani inaadhimisha siku hii, kwa Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kutoa elimu ya umuhimu wa kuzuia na kujikinga na matumizi ya sigara na bidhaa za tumbaku.
Ndugu Wananchi
Tafiti nyingi zinathibitisha madhara yatokanayo na matumizi ya tumbaku ni pamoja na magonjwa yasiyoambukiza kama vile saratani, magonjwa ya mishipa ya damu na moyo, kiharusi, magonjwa ya njia ya hewa.
Tafiti pia zinaonyesha takriban watu 6,000,000 hupoteza maisha duniani kwa mwaka kwa utumiaji wa tumbaku na bidhaa zake.
Ndugu Wananchi,
Kauli mbiu ya maadhimisho ya siku ya kupinga matumizi ya tumbaku duniani kwa mwaka 2016, inalenga kuelimisha na kuhamasisha jamii kuachana na matumizi ya tumbaku na kusisitiza kwa wazalishaji kutokuweka maandishi au nembo zinazovutia ili kuishawishi jamii kutumia bidhaa hizo. Aidha tumbaku imekuwa ikisababisha madhara kiafya kama vile magonjwa mbalimbali yasiyoambukiza. Magonjwa hayo ni magonjwa ya moyo na mishipa ya damu, saratani, ugonjwa wa kisukari na magonjwa ya njia ya hewa.
Mambo mengine yanayoongeza uwezekano wa kupata magonjwa yasiyoambukiza ni pamoja na ulaji usiofaa hasa matumizi ya chumvi kupita kiasi, kutofanya mazoezi, unywaji pombe kupita kiasi na msongo wa mawazo.
Ndugu Wananchi,
Ili kuzuia maradhi yasiyoambukiza yatokanayo na matumizi ya tumbaku na bidhaa zake ni muhimu kufuata kanuni za afya ambazo ni kutovuta sigara na kama wewe ni mvutaji, kutovuta sigara hadharani maana madhara yake ni sawa hata kwa mtu asiyevuta ambaye anapata moshi kutoka kwa mvutaji, kuendelea kuielimisha jamii juu ya madhara mbalimbali yatokanayo na utumiaji wa tumbaku hususani kwa vijana.
Ndugu Wananchi,
Serikali inaendelea na mkakati wa tiba kwa watu wenye uraibu wa matumizi ya tumbaku, ikiwa na lengo kupunguza matumizi hayo miongoni mwa jamii. Kuhakikisha pakiti za tumbaku na bidhaa zake ziwe na tahadhari ya madhara ya utumiaji wa tumbaku na bidhaa zake. Aidha, serikali, inaendelea kurekebisha sheria, kanuni na taratibu za udhibiti wa magonjwa yasiyo ya kuambukiza.
Serikali kupitia Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inatumia maadhimisho haya kuwa sehemu ya uhamasishaji kwa jamii kama ilivyo kwenye nchi zote duniani.
ASANTENI KWA KUNISIKILIZA
Post a Comment