Header Ads

Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga " Ni Aibu Mwanamke Kutafuta Kuni Wakati Mume Umelala "


Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Luteni mstaafu Abdallah Kihato, akipanda mti katika Ofisi ya Kijiji cha Magoza kama sehemu ya utunzaji wa mazingira pamoja na uzinduzi wa mradi wa Majiko Banifu uliofadhiliwa na Green Voices. 

“NI aibu mwanamke anatoka alfajiri kwenda kutafuta kuni wakati mume amelala, tena ni mateso makubwa kwa wanawake,” ndivyo anavyoanza kueleza Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Luteni mstaafu Abdallah Kihato, wakati akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Magoza.

DC Kihato alisema hayo hivi karibuni alipokuwa anazindua mradi wa Majiko Banifu wa kikundi cha ‘Moto Moto’ unaotekelezwa na wanawake wa kijiji hicho kupitia mradi wa Green Voices.

Mkuu huyo wa Wilaya alisema kwamba, kitendo cha mwanamke kuamka alfajiri kwenda vichakani kutafuta kuni kinaitia doa hata ndoa yenyewe kwa maana kinaongeza mateso kwa upande mmoja hasa mama anapokosa usingizi wa alfajiri.

Alisema mradi huo wa majiko banifu ni wa msingi hasa katika kipindi hiki ambapo mazingira yameharibiwa kutokana na ukataji ovyo wa miti kwa ajili ya mkaa na kuni, hali ambayo inawawia vigumu hata wanawake kupata kuni za kupikia.

Majiko hayo banifu yanajengwa kwa kutumia udongo wa kawaida wa kwenye vichuguu na gharama pekee ni sukari na vibao vya kufyatulia matofali.

“Misitu yote imekatwa, tena wanaume ndio wanaoongoza kwa ukataji wa miti huku wanawake wakiwa ndio waathirika wakubwa.

“Kila siku ukisimama barabarani utaona malori na baiskeli zimebeba mkaa na kuni kupeleka mjini (Dar es Salaam), wanaume wanaona fahari kukata kuni na mkaa kwenda kuuza lakini hawako tayari kutafuta kuni za kupikia nyumbani, ni aibu kubwa,” alisema DC Kihato.

Aidha, alisema kuni bora zinapelekwa kuuzwa mjini Dar es Salaam wakati wanawake wanabaki kuokoteza kuni ndogo ndogo ambazo zinakwisha baada ya muda mfupi, hivyo kulazimika tena kurudi vichakani.
Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Luteni mstaafu Abdallah Kihato, akiwasili katika Kijiji cha Magoza, Kata ya Kiparang’anda kuzindua mradi wa Majiko Banifu uliofadhiliwa na Green Voices ambao unalenga wanawake kupaza sauti zao katika kupambana na mabadiliko ya tabianchi. 


Majiko Banifu yaliyotengenezwa na kikundi cha akinamama cha ‘Moto Moto’ katika Kijiji cha Magoza. Majiko hayo ni rafiki wa mazingira kwani yanatumia kuni chache na hivyo kusaidia kupambana na  mabadiliko ya tabianchi. Mradi huo umefadhiliwa na Green Voices.


DC Abdallah Kihato akisikiliza maelezo ya namna ya utengenezaji wa majiko hayo.


Mratibu wa Mradi wa Majiko Banifu, Bi. Regina Kamuli, akionyesha mojawapo ya majiko yaliyotengenezwa na akinamama wa Kijiji cha Magoza.


Mkuu huyo wa wilaya alisisitiza kwamba ni vyema wanawake wa kikundi hicho cha ‘Moto Moto’ wakawa waalimu kwa wenzao ili kusambaza teknolojia hiyo ya majiko banifu ambayo ni rafiki wa mazingira kwani yanatumia kuni kidogo.

Hata hivyo, alihimiza kikundi hicho kisajiliwe rasmi ili kitambulike katika Halmashauri ya Wilaya na kipate fursa mbalimbali za mitaji kutoka halmashauri pamoja na taasisi za fedha.

“Jisajilini rasmi ili Idara ya Maendeleo ya Jamii iwatambue ili fedha  zinapokuja kwa ajili ya akinamama na vijana muweze kunufaika, kila mwaka kuna fedha zinazokuja wilayani kwa ajili ya wanawake na vijana, lakini wanaonufaika ni wachache kutokana na wananchi kushindwa kuunda vikundi na kuvisajili,” alisema.

Aidha, alisema kwamba, pindi watakapojisajili wanaweza kuanzisha hata karakana ya kutengeneza majiko hayo na kuyauza katika vijijini vingi wilayani humo ili kukuza kipato pamoja na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

“Elimu mliyoipata ni mtaji, badala ya kutengeneza majiko yenu wenyewe, mnaweza kutengeneza mengi na kuyasambaza katika vijiji vingine, lakini ninyi pia ni walimu tayari mnaweza kuitwa mahali popote kuwafundisha wanawake wenzenu na mkapata fedha,” alisema.

DC Kihato akikaribishwa na baadhi ya viongozi na wananchi wa Kijiji cha Magoza tayari kuzindua mradi wa Majiko Banifu yaliyotengenezwa na kikundi cha akinamama wa kikundi cha ‘Moto Moto’ kijijini hapo. Mradi huo umefadhiliwa na Green Voices.


Bi. Regina Kamuli akitoa neno la shukrani kwa mgeni rasmi Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga Luteni mstaafu Abdallah Kihato (hayuko pichani) wakati wa uzinduzi huo. Wengine pichani ni akinamama wanaounda kikundi cha ‘Moto Moto’ ambao ndio wametengeneza majiko banifu kwa lengo ya kupambana na mabadiliko ya tabianchi. Mradi huo umefadhiliwa na Green Voices.

Katika kuunga mkono jitihada hizo, DC Kihato alimuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya kuwaweka katika orodha wanawake hao ili wakaonyeshe bidhaa hiyo ya majiko wakati wa mkesha wa Mwenge wa Uhuru katika Kijiji cha Mwalusembe jana Mei 23.

Wanawake hao wameshawezeshwa na uongozi wa Halmashauri na wamehudhuria na kuonesha majiko yao katika sherehe za Mwenge kijijini hapo.

Ofisa Maendeleo ya Jamii wa Wilaya ya Mkuranga, Bw. Nambunga, ambaye alimwakilisha Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya kwenye uzinduzi huo, alisema atatoa ushirikiano wa kutosha kwa akinamama hao kuhakikisha wanasajili kikundi chao pamoja na kuzitumia fursa mbalimbali zilizopo.

“Mimi ndiye ninayeshughulikia maendeleo ya jamii, hivyo nawaahidi kwamba nitakuwa nanyi bega kwa bega ili hata fedha hizo zinazokuja wilayani kwa ajili ya vikundi vya kijamii ziweze kuwafikia,” alisema.  

Mratibu wa mradi huo wa majiko banifu, Regina Kamuli, amesema licha ya kuwafunza akinamama hao kutengeneza majiko, lakini pia wameazimia kupanda miti kwa ajili ya kukabiliana na Tatio la uhaba wa kuni katika kijiji hapo.

DC Kihato aliunga mkono jitihada za upandaji miti na yeye mwenyewe alipanda miti mitatu kama sehemu ya uzinduzi wa upandaji miti kijijini hapo huku akiagiza kila kaya ipande miti 10.

“Kila kaya ikipanda miti walau kumi tu tutabadilisha hata mazingira, naomba ninyi akinamama wa kikundi hiki ndio muwe mfano wa upandaji miti na wanakijiji wote lazima wachukue hatua,” alisema mkuu wa wilaya.

DC Abdallah Kihato akiwahutubia wananchi kuhusu umuhimu wa kutunza mazingira na kupambana na mabadiliko ya tabianchi  na kuzindua rasmi mradi wa Majiko Banifu kijijini Magoza. Wa pili kutoka kushoto ni Mratibu wa Mradi wa Green Voices nchini Tanzania, Bi. Secelela Balisidya.

DC Kihato katika picha ya pamoja.


DC Kihato akifanya mazungumzo na baadhi ya akinamama wanaotekeleza mradi wa Green Voices nchini Tanzania  walipomtembelea ofisini kwake kabla ya kwenda kuzindua mradi wa Majiko Banifu.

Akinamama wanaotekeleza mradi wa Green Voices nchini Tanzania wakiwa katika picha ya pamoja na DC Abdallah Kihato. Kutoka kushoto ni Siddy Abubakar Mgumia, Tukuswiga Mwaisumbe, Secelela Balisidya, Judica Losai, Farida Hamisi na Regina Kamuli.

Idara ya Misitu ilitoa jumla ya miti 500 ya kuanzia ambapo iliahidi kuendelea kushirikiana na kikundi hicho katika kampeni ya upandaji miti.

Regina ni mmoja kati ya akinamama 15 wanaotekeleza mradi wa Green Voices waliopatiwa mafunzi nchini Hispania mapema mwaka huu kwa nia ya kuwawezesha akinamama kupaza sauti zao kuhusu mabadiliko ya tabianchi kwa kufanya miradi ambayo itahamasisha mapambano dhidi ya uharibifu wa mazingira.

Akizungumzia mradi wa Green Voices, mratibu wa mradi huo unaotekelezwa nchini Tanzania, Secelela Balisidya, alisema mradi wa majiko banifu ni sehemu ya miradi 10 inayotekelezwa chini ya Green Voices ambapo Tanzania ndiyo pekee iliyopendekezwa kutekeleza mradi huo unaofadhiliwa na taasisi ya Foundation for Women of Africa.

Taasisi hiyo inaongozwa na Makamu wa Rais wa zamani wa Hispania, María Teresa Fernández de la Vega.

Mradi wa Green Voices unatekelezwa katika mikoa sita ya Tanzania Bara ambayo ni Dar es Salaam, Pwani, Mwanza, Kigoma, Morogoro na Kilimanjaro.

“Miradi hiyo ni kilimo cha miti ya matunda mkoani Kigoma, kilimo cha viazi lishe visiwani Ukerewe mkoani Mwanza, Ufugaji Nyuki mkoani Morogoro na Pwani, ukaushaji wa mbogamboga kwa kutumia nishati ya jua mkoani Morogoro, usindikaji wa vyakula mbalimbali kutokana na muhogo mkoani Pwani, kilimo hai cha mbogamboga, kilimo cha uyoga mkoani Dar es Salaam, mradi huu wa majiko banifu mkoani Pwani na mradi wa utafiti wa jiko linalotumia nishati ya jua mkoani Kilimanajro,” alifafanua Secelela.

Alisema, lengo kubwa la mradi wa Green Voices ni kupaza sauti za akinamama kueneza ujuzi wao wa kupambana na mabadiliko ya tabianchi ili jamii nzima ya Kitanzania iweze kujifunza zaidi na kuzitumia mbinu hizo katika kupambana na mabadiliko ya tabianchi.

Mradi huo unatarajiwa kutelekezwa kwa mwaka mmoja ili kutoa fursa kwa akinamama kutumia ujuzi wao kupambana na mabadiliko ya tabianchi na sauti zao kusikika, kwa sababu kazi wanazozifanya kila siku za utunzaji wa familia zinahusiana moja kwa moja na mazingira.

Serikali kupitia taasisi na idara zake zilizo chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara pamoja na Wizara ya Maendeleo ya Jamii imekuwa ikiendesha program mbalimbali za mafunzo ya ufundi ikiwemo utengenezaji wa majiko banifu na sanifu kama inayoendelea katika Chuo cha Maendeleo ya Jamii Malampaka wilayani Maswa.

Hata hivyo, bajeti ndogo imekuwa changamoto kubwa kwa wananchi wengi kushindwa kufikiwa na elimu ya aina hiyo.

No comments

Powered by Blogger.