Serikali yafuta Leseni za Makandarasi 4572
Bodi ya Usajili wa Makandarasi imefuta usajili wa jumla ya
makandarasi 4572 kwa kushindwa kutimiza matakwa ya Sheria ya Usajili wa
Makandarasi ya mwaka 1997.
Hayo yamebainishwa na Kaimu Msajili wa Bodi ya Usajili wa
Makandarasi (CRB), Bw. Rhoben Nkhori wakati wa Mkutano wa Mashauriano wa CRB
uliofanyika jijini Dar es Salaam na kufunguliwa na Mhe. Dkt. John Pombe
Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Bw. Nkhori amesema kuwa katika jukumu la kuratibu mwenendo
wa kazi za makandarasi, Bodi ilikagua miradi 2735. Katika miradi hiyo
iliyokaguliwa, miradi 1873 sawa na asilimia 68.5 haikuwa na kasoro.
Ameongeza kuwa miradi mingine ilikuwa na kasoro za
kutofanywa na makandarasi waliosajiliwa, kutozingatia usalama wa wafanyakazi,
kutokuwa na bango wala uzio na miradi kutosajiliwa. Kwa mujibu wa Bw. Nkhori
miradi yote iliyopatikana na upungufu wahusika walichukuliwa hatua mbali mbali
kwa mujibu wa sheria.
Aidha, Bwana Nkhori amesema kuwa kwa mwaka jana, Bodi
ilisajili miradi 3,172 yenye thamani ya shilingi trilioni4.23. Katika miradi
hii asilimia 44.4 ilifanywa na Makandarasi wazawa na asilimia 55.6 ilifanywa na
makandarasi wa kigeni.
Licha ya mafanikio hayo CRD ilikumbana changamoto kadhaa
ikiwemo kuwasilisha nyaraka za kugushi wakati wa usajili hususani kadi za
magari na mitambo, vyeti vya wataalam, kutumia majina ya makandarasi kwa
udanganyifu kwa kuuza vibao, waendelezaji kutotoa taarifa sahihi za umiliki kwa
Bodi na baadhi ya makandarasi kushindwa kuwalipa wafanyakazi na vifaa vya
ujenzi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa
Makandarasi, Bi Consolata Ngimbwa amemwomba Mhe. Rais John Pombe Magufuli
kuwapa kipaumbele Makandarasi wa humu nchini ili kuwawezesha kiuchumi. “Mhe.
Rais tunaomba utupe kipaumbele kwani sisi tukipata hiyo miradi tutawekeza hapa
nchi na kuongeza soko la ajira,”alisema Bi Ngimbwa.
Katika hotuba yake ya ufunguzi, Mhe. Dkt. John Pombe
Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amesema serikali yake itawapa
kipaumbele makandarasi wazawa lakini akawataka wajipange na kufanya kazi kwa
weledi na kuzingatia maadili ikiwemo kujiepusha na vitendo vya rushwa.
Mkutano huu pamoja na mamabo mengine utajadili jinsi ya
kuwajengea uwezo makandarasi nchini. Kauli mbiu ya Mkutano huo ni “Juhudi za
Makusudi za kukuza uwezo wa makandarasi wazawa, changamoto na mustakhabali.”
Post a Comment