Tigo yatoa Kompyuta 20 Zilizounganishwa na Intaneti kwa Sekondari 3 Mtwara
Wanafunzi wakishuhudia makabidhiano hayo. |
Kampuni inayoongoza kwa maisha ya kidijitali ya Tigo Tanzania leo
imetoa kompyuta 20 zenye thamani ya shilingi milioni 33 zikiwa na huduma ya
bure ya intaneti iliyogharimu 22m/- kwa shule tatu za sekondari mkoani
Mtwara. Msaada huo uko katika mkondo wa malengo ya kampuni ya kuleta
mabadiliko ya kidijitali katika sekta ya elimu nchini.
Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano
yaliyofanyika Shule ya Sekondari Sino mkoani Mtwara Mkurugenzi wa Tigo Kanda ya
Pwani, Goodluck Charles alisema, “Msaada huu kwa shule hizi tatu ni sehemu ya
mkakati wa kampuni wa kuleta mageuzi katika mtindo wa maisha ya kidijitali.
Msaada huu wa leo umekuja baada ya kukabidhi kompyuta 10 kwa Shule ya Msingi
Chuda mkoani Tanga na kompyuta 25 zilizounganishwa na intaneti kwa
Hospitali ya Rufaa ya Sekou Toure mkoani Mwanza mwaka jana.
“Msaada kwa shule ya Sekondari ya Masasi,
Tandahimba na Sino ni kielelezo cha kweli cha uwekezaji wa Tigo katika miradi
tofauti yenye mchango kijamii kupitia mkakati wetu wa kuwekeza kijamii
unaowezesha jamii kupokea zana za kisasa za Teknolojia ya Habari na Mawasiliano
katikanyanja zote za kijamii ikiwemo sekta ya elimu,” alisema Charles.
Tukio hilo ambalo lilihudhuriwa na Mkuu wa
Mkoa wa Mtwara, Halima Dendego ambaye alizitaka sekta binafsi kuisaidia
serikali katika mikakati yake katika kuboresha mazingira ya kujifunzia katika
shule zilizopo nchini.
Dendego alisema, “Naipongeza Tigo kwa
ukarimu wao wa kuzisaidia shule hizi natoa wito kwa watu binafsi kampuni za
biashara na wadau wengine kujitokeza katika kuunga mkono juhudi za kuboresha
sekta ya elimu.”
Akipokea msaada huo kwa niaba ya wakuu
wenzake wa shule za sekondari, Mkuu wa Shule ya Sekondari Sino Riyadh Kadhi
alisema kwamba kompyuta hizo zitawawezesha wanafunzi kuwa na uelewa wa kiteknolojia
na kuwawezesha kuipata teknolojia ya habari mapema katika elimu yao.
“Tunafurahi kwa hatua hii ya Tigo; tuna
matumaini kwamba kompyuta hizi zitawaweka wanafunzi wetu katika ngazi
moja na wenzao katika mashule mengine yaliyo maeneo ya mjini na duniani kwa
ujumla,” alisema Kadhi.
Post a Comment