Header Ads

Watanzania Tumuunge Mkono Rais Magufuli Kujenga Uchumi wa Viwanda

Na. Lilian Lundo - MAELEZO

Katika hotuba yake ya kwanza Mhe.  Rais  wa Awamu ya Tano Dkt. John Pombe Magufuli alipokuwa akifungua Rasmi Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alisema kwamba Serikali yake itaweka mkazo mkubwa katika ujenzi wa Viwanda.

“Viwanda tunavyovikusudia ni vile ambavyo sehemu kubwa ya malighafi yake itatoka ndani, hususani kwenye sekta za kilimo, mifugo, uvuvi, madini na maliasili nyingine,” alifafanua Rais Magufuli

Viwanda hivyo  vitatakiwa kuzalisha bidhaa ambazo zitatumiwa na watu wengi nchini kama vile nguo, viatu, mafuta ya kupikia ili kuwa na uhakika wa soko la ndani kabla ya kufikiria soko la nje. 

Licha ya Serikali kuweka mkazo katika uanzishwaji wa viwanda nchini lakini bado watanzania wamekuwa na fikra potofu juu ya bidhaa zinazotengenezwa ndani ya nchi, wengi wao wanashusha thamani ya  bidhaa hizo na kuziweka katika  kundi la bidhaa zisizo na ubora huku wakikimbilia bidhaa za nje ya Tanzania.

Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango alipotembelea maonyesho ya Viwanda yaliyofanyika  kuanzia tarehe 07  hadi 11 Desemba 2016 alisema kwamba Tanzania haitaweza kuwa Tanzania ya Viwanda ikiwa watanzania wenyewe hawathamini bidhaa zinazotengenezwa ndani ya nchi.

Dkt. Mpango alitoa mfano wa mashine zinazotengenezwa na SIDO ambazo zimekuwa zikidharaulika kwamba hazina ubora wakati huo huo mashine hizo zimetengenezwa kwa kuzingatia mazingira ya nchi yetu na gharama yake ni ya chini ukilinganisha na zile zinazotengenezwa nje ya nchi.

“Haiwezekani hata jembe la mkono liagizwe toka nje wakati kuna viwanda ndani ambavyo vinauwezo wa kutengeneza majembe katika kiwango cha juu.” Alisema Dkt. Mpango.

Ni muda wa watanzania kubadilika na kuunga mkono Serikali ya Awamu ya Tano kwa kununua bidhaa zinazotengenezwa ndani ya nchi ili kuipeleka nchi kuwa na uchumi wa viwanda hatimaye kufikia uchumi wa kati.

Kamwe Tanzania haitaweza kufikia uchumi wa viwanda ikiwa sisi wenyewe tunakimbilia bidhaa zinazotoka nje ya Tanzania.

Ifike hatua tuone bidhaa zetu ni bora zaidi kuliko bidhaa kutoka nje ya nchi. Nchi nyingi zimeendelea kutokana na kuthamini bidhaa ambazo zimekuwa zikitengenezwa ndani ya nchi.

Mfano ni Nchi ya Japan, ambayo imekuwa ikifanya vizuri katika uchumi wa viwanda, mafanikio hayo yametokana na wajapani wenyewe kutokana na imani ambayo wamejiwekea kwamba hakuna bidhaa inayotengenezwa Dunia yenye ubora zaidi ya bidhaa zinazotengenezwa nchini kwao. 

Kwa kupenda bidhaa zinazotengenezwa ndani kutaamsha morali kwa uanzishwaji wa viwanda vingi hapa nchini, kwani watu wengi wamekuwa wakihofia kuanzisha viwanda vidogo vidogo kwa hofu ya kukosa masoko ya bidhaa zao na wengine wakihofia gharama ya uanzishwaji wa viwanda.

Ambapo wengi wetu tumekuwa tukitafsiri kiwanda kama ni kuwa na mashine kubwa, zenye gharama kwa ajili ya uzalishaji wa bidhaa mbalimbali, na kusahau kuwa kiwanda kinaweza kuundwa kwa kuwa na cherehani nne tu.

Hivyo basi, kwa kuwa na cherehani nne peke yake, tayari watu wanne wanakuwa wamepata ajira na kujikomboa kiuchumi.

Hivyo uchumi huu wa viwanda ni fursa kubwa kwa vijana katika kutengeneza ajira badala ya kusubiri ajira kutoka Serikalini au Mashirika Binafsi.

Ambapo Mhe. Rais katika hotuba yake ya kufungua Bunge la 11 alisema kuwa ifikapo mwaka 2020 idadi ya ajira itokanayo na viwanda ifikie asilimia 40 ya ajira zote zitakazokuwepo nchini wakati huo.

No comments

Powered by Blogger.