Wizara ya Afya yatoa Tathmini Kuhusu Hali ya Kipindupindu Nchini
Waziri wa Afya, UMMY MWALIMU |
TAMKO KUHUSU MWENENDO WA UGONJWA WA KIPINDUPINDU
NCHINI LILILOTOLEWA NA MHE. UMMY MWALIMU (MB); WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO
YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO, TAREHE 9
MEI, 2016.
Ndugu
wanahabari,
Serikali kupitia Wizara yangu inaendelea na utaratibu wa
kutoa taarifa ya mwenendo wa
mlipuko wa ugonjwa wa Kipindupindu nchini kila wiki kama tulivyoahidi. Takwimu
za ugonjwa huu zinaonyesha kuwa hadi kufikia tarehe 08 Mei 2016, kulikuwa na jumla ya wagonjwa
21,262 ambao wametolewa taarifa ya kuwa na ugonjwa huu, na kati ya hao,
watu 333
wamepoteza maisha.
Katika kipindi cha mwezi mmoja yaani mwezi wa Aprili
2016, idadi ya wagonjwa imekuwa ikipungua kwa kiasi kikubwa lakini katika
kipindi cha mwezi Mei, 2016 kasi ya maambukizi imeanza tena kuongezeka.
. Takwimu za wiki
iliyopita kuanzia tarehe 2
hadi 8 Mei 2016 zinaonyesha kuwa, kasi ya
ugonjwa wa kipindupindu imeongezeka,
ambapo idadi ya wagonjwa wapya walioripotiwa ni 138 na vifo 2,
ikilinganishwa na wagonjwa wapya
104 walioripotiwa wiki
iliyotangulia, sawa na ongezeko la 32%. Takwimu hizi ni zinaonesha kuwa juhudi zaidi ziahitajika katika
mapambano dhidi ya ugonjwa huu.
Mikoa ambayo
imeendelea kuongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya wagonjwa wiki hii ni Kilimanjaro (58, kifo 1), Dar es Salaam (29) na Morogoro (22, kifo 1), Pwani
(16) na Mara (15). Halmashauri zilizoongoza kutoa wagonjwa
wengi ni Same), Kinondoni, Mvomero), Mbulu, Tarime vijijini, Ilala, Tarime mjini,
Temeke, Morogoro vijijini Kilolo Morogoro mjini, Bagamoyo, Kisarawe.
Katika wiki iliyopita, mikoa ambayo haikuwa na wagonjwa
wa kipindupindu ni Kigoma, Dodoma, Mwanza, Geita, Singida, Shinyanga, Arusha,
Tanga, Tabora, Lindi, Kagera, Rukwa, Katavi, Mbeya, Simiyu na Mtwara.
Ndugu
wanahabari,
Kama nilivyoeleza hapo juu, takwimu zinaonyesha kuwa ugonjwa
unaongezeka, hivyo tunahitaji kuchukua tahadhari kubwa,
hususan wakati wa huu wa mvua, ambapo kuna uwezekano mkubwa wa maji ya mvua
kusambaza vimelea vya ugonjwa huu. Tujitahidi
kuzuia maambukizi, na pia
kuendelea kutoa taarifa za ugonjwa kila siku, hata kama hakuna wagonjwa, na
kusimamia kikamilifu hatua mbalimbali za udhibiti wa mlipuko huo.
Ndugu wanahabari,
Wizara inaendelea kutoa rai kwa wananchi wote
kuzingatia kanuni za usafi binafsi na usafi wa mazingira. Aidha wananchi
wanashauriwa kutumia maji safi na salama na hii ni pamoja na kuhakikisha maji ya kunywa yanachemshwa au kutibiwa kwa dawa
kama maagizo ya wataalam yanavyoelekeza. Napenda pia kusisitiza kwa wananchi
wanaokaa kandokando ya Mto Pangani hususani mikoa ya Tanga na Kilimanjaro, kuwa
maji ya mto huo si salama, kwa kuwa yamechafuliwa na vimelea vya kipindupindu. Ni
muhimu sana kuyachemsha au kuyatibu kwa dawa maji hayo kabla ya kuyatumia
nyumbani. Napenda kusisitiza
tena kwamba ni marufuku kwa watu
kutitirisha maji taka ovyo,
hasa katika kipindi hiki cha mvua na mamlaka husika zinatakiwa kuchukua hatua za
kisheria kwa wale wote watakaokiuka agizo hili. Aidha tunawasihi viongozi
mbalimbali wa ngazi zote; za vitongoji, vijiji, kata na tarafa kusimamia
kikamilifu suala hili, hususan wakati
huu wa mvua za masika
Ndugu
wanahabari,
Tunaendelea kuisihi jamii kuungana na Halmashauri, Mikoa
pamoja na Wizara katika juhudi za kupambana na kuenea kwa ugonjwa wa
kipindupindu kwa kuzingatia yafuatayo:
§ Kujenga na kutumia vyoo bora katika maeneo tunamoishi
ili kupunguza hatari ya kuenea kwa ugonjwa huu.
§ Kunawa mikono kwa maji yanayotiririka na sabuni kabla ya
kula, baada ya kutumia choo na baada ya kumsafisha motto aliyejisaidia.
§ Mamlaka za maji zilizopo nchini zihakikishe upatikanaji
wa maji safi na salama kwa wananchi.
§ Kuzingatia ushauri na elimu sahihi kuhusu ugonjwa wa
kipindupindu, ili jamii iondokane na imani potofu kuhusu kipindupindu. Viongozi
wa dini, watu mashuhuri na waganga wa tiba mbadala wasaidie kuhamasisha jamii
zao kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huu,
§ .
§ Kufikisha wagonjwa wa Kipindupindu mapema katika vituo
vya kutolea huduma ili wawahi kupata matibabu.
§ Kuzingatia matumizi sahihi ya ORS kwa wagonjwa walioanza
kuonesha dalili ili kupunguza athari za ugonjwa.
§ Watumishi wa afya kutoa takwimu sahihi na kamili za
ugonjwa kwa kuzingatia miongozo inayotolewa na Wizara.
Hitimisho
Wizara inawapongeza na
kuwashukuru wadau wote kwa jitihada za dhati zinazoendelea kutekelezwa na
katika kusimamia kikamilifu miongozo
inayotolewa na Wizara ili kuutokomeza ugonjwa huu, wakiwemo wataalamu wa sekta
mbalimbali, Mashirika ya Kimataifa,
Watumishi, Mikoa na Halmashauri pamoja na waandishi wa habari na wananchi
kwa ujumla.
Asanteni sana
Post a Comment