Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimshukuru
mwenyeji wake Rais wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni jijini Kampala mara baada
ya kumaliza mazungumzo yao nchini Uganda.
........................
Viongozi hao pia
wamezungumzia mradi mkubwa wa ujenzi wa bomba la mafuta la kutoka Hoima (Ziwa
Albert) nchini Uganda hadi bandari ya Tanga nchini Tanzania ambapo pamoja na
kuishukuru Uganda kwa uamuzi wake wa kuamua bomba hilo lipitie Tanzania, Rais
Magufuli amemshauri Rais Museveni kufupisha muda wa ujenzi wa mradi huo, kwa
kutumia mbinu inayojumuisha usanifu na ujenzi (Design and Construct method) na kutumia wakandarasi wengi
watakaogawanywa katika vipande tofauti badala ya kutumia mkandalasi mmoja.
"Nashauri
tutumie mbinu ya usanifu na ujenzi pamoja, hii ni njia ya haraka zaidi, na pia
tugawe vipande vya ujenzi kwa njia yote ya bomba la mafuta yenye urefu wa
kilometa 1,410 tunaweza kuwa na Wakandarasi watano mpaka sita ambao watatumia
njia hiyo mpya ya usanifu na ujenzi.
"Kwa kufanya
hivyo tutakuwa tumepunguza muda utakaotumika kwa ajili ya ujenzi wa bomba la
mafuta, inaweza hata kuchukua mwaka mmoja tu" Amesema
Rais Magufuli.
Rais Magufuli
amebainisha kuwa kwa kufanya hivyo faida za mradi huo wa mafuta zitaanza
kupatikana mapema badala ya kusubiri miaka miwili au mitatu ijayo, na kwamba
hiyo itakuwa inaendana na kauli mbiu yake ya "Hapa Kazi Tu"
Pia Rais Magufuli
amemshukuru Rais Museveni kwa uamuzi wa nchi hiyo wa kuipa Tanzania umiliki wa
asilimia 8 katika mradi huo wa bomba la mafuta.
Kwa upande wake
Rais Museveni amesema amefurahishwa na hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa
mradi huo, na pia amempongeza Rais Magufuli kwa juhudi zake kubwa ambazo
amezifanya katika mapambano dhidi ya rushwa nchini Tanzania.
"Napenda kasi
yako ya uongozi, napenda jinsi unavyopambana na rushwa, kwa sababu rushwa
ilikuwa inazaa matatizo mengine kama vile ucheleweshaji wa mizigo bandarini na
vikwazo vya mpakani, hivyo nakupongeza sana kwa hilo"
Amesema Rais Museveni.
Katika sherehe ya
kuapishwa kwa Rais Museveni iliyofanyika kabla ya mazungumzo hayo, pamoja na
Rais Magufuli viongozi wengine kutoka Tanzania waliohudhuria ni Rais Mstaafu wa
awamu ya pili Mhe. Ali Hassan Mwinyi, Rais Mstaafu wa awamu ya nne Mhe. Jakaya
Mrisho Kikwete aliyekuwa na Mkewe Mama Salma Kikwete na Naibu Waziri wa Mambo
ya Nje Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa Dkt. Suzan
Kolimba.
|
Post a Comment