Jamii yatakiwa Kudumisha na Kuenzi Utamaduni
Na Shamimu Nyaki WHUSM
Katika kuelekea kilele cha maadhimisho ya siku ya Uanuwai wa Utamaduni Duniani Serikali imeitaka jamii kuhifadhi kulinda na kuheshimu utamaduni wa nchi kwa vile ndio kitambulisho cha Taifa letu ili kuweza kutambulika ndani na nje ya nchi.
Wito huo umetolewa leo Jijini Dar es Salaam na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Utamaduni kutoka Wizara ya Habari,utamadunu,Sanaa na Michezo Bi.Lily Beleko wakati akizungumza na Waandishi wa habari kuhusu cha maadhimisho ya siku ya Uanuwai wa Utamaduni Duniani ambapo kauli mbiu ya madhimisho ya mwaka huu ni” Utamaduni wa Uadilifu na Nidhamu ya Kazi Huleta Maendeleo”, “Sasa Kazi Tu”
.
Kaimu Mkurugenzi wa Utamaduni Bi.Lily Beleko amesema kuwa ni wajibu kwa kila mtanzania kuheshimu Utamaduni wetu na kushiriki kikamilifu katika kuutambua, kuujenga, kuuendeleza na kuurithisha kwa vizazi vingine.
“Siku hii ni maalumu kwa kila mtanzaniana na kila mmoja hana budi kukubaliana na harakati hizi za kulinda, kuhifadhi na kuendeleza Utamaduni wetu kwa ajili ya vizazi vijavyo”Alisema Bi Lily.
Bi.Lily Beleko ameongeza kuwa nchi haiwezi kutambulika na kuheshimika kama Taifa huru bila kuwa na Utamaduni wake hivyo kuwepo kwa maadhimisho haya kunaipatia jamii fursa ya kuendelea kukumbushana ,kuhamasishana na kuhimizana katika kuuenzi utamaduni wa nchi.
Siku ya Uanuwai wa Utamaduni Duniani huadhimishwa kila ifikapo tarehe 21 Mei, ambapo siku hiyo imeteuliwa na Baraza kuu la Umoja wa Mataifa kuona umuhimu wa kuhifadhi na kuendeleza Utamaduni na hivyo kupitisha Azimio Na 57/249 mnamo mwaka 2002.
Post a Comment