Header Ads

RBA yaandaa Mashindano ya Mpira wa Kikapu


Na BEATRICE LYIMO

Chama cha mpira wa Kikapu Dar es salaam (RBA) kimeanzaa mashindano ya ligi ya mpira huo yatakayoshirikisha timu 16 kutoka kwa wananume na timu nane za wanawake.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam Mwenyekiti wa chama hicho Okare Emesu alisema kuwa ligi hiyo inatarajiwa kuanza Januari 28 mpaka julai 30  mwaka huu.

Alisema kuwa viongozi wa RBA wamekuja na mikakati hiyo ili kuleta chachu kwenye maeneo mengine ya mkoa, ligi ya watoto chini ya miaka 14, ligi ya daraja la kwanza, ligi ya vyuo, ligi ya mashirika, ligi ya mashule, program maalumu kwa ajili ya kukuza vipaji kwa mpira wa kikapu nchini.

“Tangu kuanzishwa kwa chama hiki, kumekuwa na mafanikio ya muda mfupi ikiwemo ushiriki kwenye mashindano ya Taifa na kushika nafasi ya pili kwa wanaume na wanawake jambo ambalo halikuweza kufanyika kwa takribani miaka mitatu sasa” Alisema Mwenyekiti huyo.

Aidha akizungumzia kuhusu mfumo wa ligi utakaotumika kwenye mashindano hayo, Mkurugenzi wa Mawasiliano na Masoko RBA Peter Mpangala alisema kuwa mfumo utakaotumika ni mfumo wa nyumbani na ugenini katika hatua za awali na timu nane za wananume za nafasi za juu zitacheza mtoano hadi kupata bingwa.

Mbali na hayo alisema kuwa kutakuwa na maonyesho ya awali ya ligi ya RBA (Pre RBA Show case) siku ya Mapinduzi januari 12, mwaka huu kwenye viwanja vya mpira wa kikapu vya Gymkhana yakilenga kukaribisha wadau mbalinmbali kuona mfano wa ligi ya RBA itakavyokuwa.

Timu zinazotarajiwa kushiriki kwenye ligi hiyo kwa upande wa wanaume ni JKT, Mgulani, Ukonga Kings, Magereza, Savio, Pazi, DB Youngstars, Magnet, ABC, Mabibo Bullets, Outsiders, Kurasini heat, Oilers, Vijana, Chui na Jogoo na kwa upande wa wanawake ni JKT Stars Jeshi  Stars, Vijana Queens, DonBosco Lioness, Ukonga Queens, Kurasini Divas na Oilers Princess.

No comments

Powered by Blogger.