Header Ads

TTCL kuanza kutoa Huduma za Kifedha Hapa Nchini

Mhandisi wa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL), Paul Magembe akitoa maelezo kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa, kuhusu mitambo ya kutolea huduma za kifedha iliyopo katika ofisi za Kampuni hiyo mkoani Dodoma.
...............................

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa ameitaka Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) kujipanga na kuanza mkakati wa kutangaza huduma za fedha ambazo zitatolewa na kampuni hiyo mwanzoni mwa mwaka ujao.

Prof. Mbarawa ametoa agizo hilo baada ya kukagua mitambo itakayotumika kwa huduma hiyo ambayo itaongeza ushindani wa biashara kwenye huduma za simu nchini mkoani Dodoma.

"Lazima mjipange kwenye idara ya masoko kwa kuanza kutangaza huduma hiyo kupitia njia zote zikiwemo mitandao ya kijamii, ili wananchi warahisishiwe huduma za fedha kupitia TTCL", amesema Waziri Prof. Mbarawa.

Aidha, ameiagiza kampuni hiyo kupitia idara ya masoko kujipanga kuona fursa zilizopo kwa kufahamu mahitaji ya wateja wao na  kuhakikisha inaongeza wateja katika mkoa huo ili kuteka soko la ushindani  ambapo Serikali inajipanga kuhamia huko.

Waziri Prof.Mbarawa ametaja baadhi ya maeneo ambayo TTCL inahitaji kuboresha zaidi ni upande wa Simu (Voice) na Data (video) ili kuweza  kurahisisha mawasiliano kwa njia ya video conference  kwa kuwa kuna baadhi ya watendaji wengine watabaki Dar es salaam.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa, akitoa maelekezo  kwa Meneja wa Shirika la Posta Nchini, kanda ya Dodoma Bw. Laurent Thobias (kulia), kuhusu utoaji wa matangazo ya huduma ya Posta mlangoni katika ofisi za Shirika hilo mkoani humo.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa, akizungumza na watumishi wa taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo (hawapo pichani), alipokutana nao Mkoani Dodoma.

Baadhi ya Watumishi wa Taasisi za Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, wakimsikiliza Waziri wa Wizara hiyo (hayupo pichani), alipokutana nao kuwapa mikakati ya utendaji wa Wizara hiyo, Mkoani Dodoma.

No comments

Powered by Blogger.