Header Ads

Mahusiano CUP yahamasisha Wananchi Kujitokeza Kupima VVU wilayani Kahama

  Mgeni rasmi katika fainali za Mahusiano Cup, katibu tawala wa wilaya ya Kahama, Timoth Ndanya (Katikati) akipokea maelezo kutoka kwa mwamuzi wa mchezo wa fainali kati ya timu za kata ya Mhungula, Kushoto ni Kaimu Meneja Mkuu wa Mgodi wa Buzwagi George Mkanza, wengine katika picha ni Solomon Rwangabwoba- Meneja Ufanisi na raslimali watu (katikati ya mwamuzi na katibu tawala) wengine ni mwenyekiti wa KDFA Bwana Ibrahim Khan na Bwana Magesa Magesa Afisa Mawasiliano Mgodi wa Buzwagi.
...............................................

Watu zaidi ya 400 wakazi wa mji wa Kahama na viunga vyake wamejitokeza kupima VVU wakati wa mashindano ya Mahusiano Cup ambayo huusisha michezo ya mpira wa miguu na mpira wa pete.



Mashindano hayo ambayo huandaliwa na Kampuni ya Uchimbaji wa madini ya Acacia kupitia Mgodi wa Buzwagi yalizinduliwa tarehe moja desemba, yakiwa na lengo la kuhamasisha Jamii kupima afya zao na kuimarisha uhusiano baina ya wenyeji na Mgodi wa Buzwagi.



Akizungumza wakati wa Kuhitimisha fainali za michezo hiyo pamoja na kampeni ya upimaji VVU katika uwanja wa mpira wa Kahama Mji, Katibu Tawala wa Wilaya ya Kahama Timothy Ndanya amesema wao kama uongozi wa wilaya ya Kahama wanafarijika na jitihada zinazofanywa na Kampuni ya Acacia kupitia Mgodi wa Buzwagi katika harakati za kuhakikisha Jamii inajua afya zao kwa kupima afya na kupanga maisha yao vizuri.



Ameongeza pia jitihada hizo zimekuwa zikionekana kupitia katika sekta ya michezo na hii imekuwa ikijidhihirisha kupitia programu mbalimbali za michezo ambazo zimekuwa zikiendeshwa na Kampuni ya Acacia.



Akizungumzia Mashindano ya Mahusiano Cup ya mwaka huu ambayo yamehusisha timu nyingi zaidi ukilinganisha na miaka iliyopita, Katibu Tawala huyo amesema mashindano ya mwaka huu yamesaidia kuonyesha vipaji vingi vya wanamichezo ambao hapo awali hawakuwa na fursa ya kuweza kuonyesha uwezo wao kupitia michezo.

  Katibu tawala Wilaya ya Kahama Timoth Ndanya akisalimiana na wachezaji wa timu ya kata ya Mhungula.

  Kaimu Meneja Mkuu wa Mgodi wa Buzwagi George Mkanza akisalimiana na wachezaji wa timu ya kata ya Mhungula, nyuma yake ni Meneja Ufanisi na raslimali watu wa Mgodi wa Buzwagi,Solomon Rwangabwoba.

Katibu tawala wa wilaya ya Kahama Timoth Ndanya (Mwenye track suit nyekundu) akijianda kupiga mpira kuashiria kuanza kwa mchezo wa fainali ya Mahusiano Cup baina ya timu ya Kahama Mji na timu ya Mhungula.

  Wachezaji wa timu za Kahama Mji na Timu ya kata ya Mhungula wakiendelea na mchezo wa fainali za Mahusiano Cup mchezo ulioisha kwa timu ya Mhungula kuibuka kidedea kwa kuwachapa vijana wa mjini timu ya Kahama Mji jumla ya magoli matatu kwa mawili (3-2).

  Katibu Tawala wa Wilaya Kahama Timoth Ndanya akiwahutubia wachezaji na wananchi wa mji wa Kahama mara baada ya kumalizika kwa michezo wa fainali za Mahusiano Cup.

  Nahodha wa timu ya mpira wa pete ya Kahama Mji akipokea kombe la mshindi wa kwanza pamoja na kitita cha shilingi milioni moja baada ya kuibuka kidedea katika michezo hiyo.

Nahodha wa timu ya Kahama Mji akinyanyua kikombe cha mshindi wa pili kwa upande wa mpira wa miguu baada ya timu hiyo kujinyakulia ushindi wa pili, timu hiyo pia ilijinyakulia kitita cha shilingi laki saba na nusu.

No comments

Powered by Blogger.