Header Ads

Mradi wa GREEN VOICES Wafanikisha Ujenzi wa Jiko la Umeme Jua

Mgeni rasmi katika uzinduzi wa jiko la umeme-jua, Robert George, ambaye ni Ofisa Ushirika wa Manispaa ya Moshi, akisikiliza maelezo ya namna jiko hilo linavyofanya kazi kutoka kwa Mkurugenzi wa Uhawilishaji Teknolojia wa Kituo cha Zana za Kilimo na Teknolojia Vijijini – CAMARTEC, Mhandisi Noela Byabachwezi, Kushoto kwa Noela ni mshiriki kiongozi wa mradi wa Green Voices Moshi, Farida Makame, Wengine pichani ni washiriki wa kikundi hicho. 
........................

Viunga vya ukumbi wa Aroma mjini Moshi vimesheheni akinamama wengi katika siku hii ya Jumamosi, kama ilivyo kawaida kwa siku kama hiyo, ambapo wote wanaonekana kuwa na nyuso za furaha kutokana na mijadala inayoendelea.

Lakini tofauti na Jumamosi nyingine ambapo akinamama wa kikundi cha Wamama wa Kahawa ambao ni wanachama wa Tanzania Women Coffee Association - TAWOCA mjini humo kujadili masuala mbalimbali ya ujasiriamali, siku hii inaonekana kuwa ya tofauti kwa sababu licha ya idadi ya akinamama kuongezeka, lakini kuna tukio kubwa na muhimu ambalo limewakutanisha.

"Leo tunazindua rasmi jiko la umeme-jua, yaani parabolic solar cooker, ambalo kupitia udhamini wa mradi wa akinamama wa Green Voices, hatimaye limeweza kupatikana baada ya jithada za miezi kadhaa," ndivyo anavyoanza kuelezea Farida Makame, mshiriki kiongozi wa mradi wa Green Voices wa kikundi hicho, huku akionyesha kifaa kinachofanana na dish kama la satellite ambacho katikati yake kumewekwa sufuria inayong’aa kama taa kubwa ya umeme.

Anasema kwamba, jiko hilo linaweza kupika kila aina ya chakula kwa kutumia mionzi ya jua ya moja kwa moja bila kuathiri mazingira.

"Kwa kutumia jiko hili maana yake huhitaji kutafuta mkaa wala kuni, hivyo kuokoa misitu ambayo inateketea kila siku kutokana na ukataji wa miti kwa ajili ya kutafuta nishati ya kupikia," anaongeza.

Farida, ambaye pamoja na akinamama wengine 14 – wakiwemo wanahabari watano wanawake – walipatiwa mafunzo ya takriban miezi miwili jijini Madrid, Hispania mapema mwaka huu wa 2016, anasema kwamba lengo la kubuni na kutengeneza jiko hilo la umeme-jua ni kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi pamoja na kupambana na uharibifu wa mazingira.


Jiko la umeme-jua ambalo limetengenezwa na CAMARTEC kwa ufadhili wa mradi wa Green Voices Tanzania kwa ajili ya kikundi cha akinamama wa TAWOCA Moshi. 


Wanakikundi wa TAWOCA Green Voices Moshi wakihakikisha jinsi joto la jua linavyosaidia kupika kwa kutumia jiko la umeme-jua. Kushoto ni mgeni rasmi katika uzinduzi wa jiko hilo, Robert George, ambaye ni Ofisa Ushirika wa Manispaa ya Moshi.

Mhandisi Noela Byabachwezi, mwenye kofia kulia, akionyesha kwa vitendo jinsi jiko la umeme-jua linavyofanya kazi.

No comments

Powered by Blogger.