DC Kilolo Asia Abdallah akifafanua jambo.
................................
Baada ya mradi wa maji Ipalamwa kujengwa chini ya kiwango kwa bomba kupasuka ovyo kabla ya mradi kukabidhiwa ,baraza la madiwani la Halmashauri ya wilaya ya Kilolo mkoani Iringa limempa muda wa wiki mbili mkandarasi wa kampuni ya Norcom Ltd kukamilisha mradi wa maji wa Ipalamwa kwa ubora unaotakiwa zinginevyo mkataba wake utavunjwa.
Huku mkuu wa wilaya ya Kilolo Asia Abdalaha akiagiza Halmashauri hiyo kutomlipa fedha yeyote mkandarasi huyo hadi hapo atakapokamilisha mradi kwa kiwango kinachotakiwa vinginevyo kama kuna pesa alilipwa awali basi pindi mkataba wake utakapovunjwa atapaswa kuzirudisha fedha hizo.
Wakitoa maadhimio hayo katika kikao cha baraza la madiwani kilichofanyika juzi katika ukumbi wa Halmashauri ya Kilolo na kuhudhuriwa na mkuu wa wilaya ya Kilolo ,madiwani hao walisema kuwa wamechoshwa na mkandarasi huyo kuendelea kuchelewesha mradi huo wa maji na kuwa sasa wanaona suala hilo la kero ya maji kijiji cha Ipalamwa lifike mwisho kwa kumpa muda wa mwisho kwa ajili ya kukamilisha mradi huo .
Mhandisi wa maji wa wilaya ya Kilolo Enock Basyagile akijibu hoja za baraza la madiwani juu ya ucheleweshwaji wa mradi huo alisema kuwa sababu ya kuchelewa kwa kazi hiyo ni kutokana na kukosekana kwa fedha kati ya Halmashauri na mkandarasi ila kwa sasa fedha zimeingia na mchakato wa kufanya kazi hiyo kwa kununua vifaa vya mradi huo ikiwa ni pamoja na mchakato wa malipo kwa mkandarasi huyo.
Mkuu wa wilaya ya Kilolo Asia Abdalah alisema hakubaliani na uamuzi wa mhandisi wa maji wilaya kutenga fedha ama kufanya mchakato wa malipo ya Tsh milioni 19 kwa mkandarasi huyo aliyejenga mradi huo chini ya kiwango ila alitegemea kuona mkandarasi huyo anachukuliwa hatua kwa kufanya kazi chini ya kiwango.
" Sikubaliani hata kidogo na uamuzi wa kumlipa fedha mkandarasi huyo ama Halmashauri kununua mabomba kwa ajili ya kukarabati mradi ambao haujakabidhiwa kwa wananchi .....naagiza mkandarasi huyo afanye kazi hiyo kwa gharama zake na asilipwe pesa yoyote hadi mradi utakapokabidhiwa "
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kilolo Bw Vellance Kihwaga alisema sababu kubwa ya mradi huo kuendelea kusumbua kwa mabomba kupasuka ni baada ya mkandarasi huyo kwenda kinyume na mkataba wa kazi hiyo kwa kuweza mabomba membamba zaidi kuliko nguvu ya maji hivyo pindi maji yakifunguliwa mabomba hayo hupasuka .
Alisema kutokana na ubovu huo wa mabomba kamati ya fedha ilifanya ziara ya ukaguzi wa mradi huo toka mwaka jana na kumwagiza mkandarasi huyo kufanya marekebisho kwa kutoka mabomba yote yasiyo na ubora na kufunga mabomba yenye ubora na alikubali kuifanya kazi hiyo ndani ya wiki mmoja na kamati ilimpa mwezi mmoja ila hadi sasa ni zaidi ya miezi 4 kazi hiyo haijafanyika .
Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Kilolo Bw Aloyce Kwezi alisema kuwa mkanadarasi huyo bado hajalipwa fedha yoyote na kuwa Halmashauri haitamlipa fedha hadi hapo mradi utakapokamilika na anapaswa kufanya kazi hiyo kwa gharama zake na iwapo atashindwa kwa muda uliotolewa basi halmashauri itavunja mkataba huo.
Wakati huo huo serikali ya wilaya ya Kilolo imepiga marufuku wageni kuingia katika vijiji ama kata na kuendesha miradi mbali mbali pasipo kushiriisha viongozi wa ngazi zote za vijiji ama Halmashauri .
|
Post a Comment