( MAKALA ) Heko SMZ kwa kufanya utekelezaji wa Mpango wa Matumizi ya Ardhi ya Mwaka 1968
Na. Lilian Lundo - MAELEZO.
Nichukue nafasi kuipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kwa kutekeleza Mpango wa Matumizi ya Ardhi ya Mwaka 1968 ambao ulikuwepo kwa muda mrefu lakini utekelezaji wake ulikuwa ukienda taratibu.
Zanzibar ni moja ya kitovu kikubwa cha utalii nchini, kikiwa na vivutio mbalimbali kama vileJumba la Maajabu, Mji Mkongwe (stone town) ambao upo katika orodha ya UNESCO ya "Urithi wa Dunia" (World Heritage), fukwe zinazozunguka Kisiwa hicho pamoja na bustani maarufu ya Forodhani.
Vivutio hivyo vimepelekea Zanzibar kupokea wageni mbalimbali wanaotoka ndani na nje ya nchi kwa ajili ya utalii na mapumziko ya kawaida, mwisho wa mwaka na hata mwisho wa wiki.
Licha ya uwepo wa vivutio hivyo vya kila namna katika mji huo, bado kulikuwa kunahitajika kuwepo na mpangilio mzuri wa mji huo ambao utaweza kutofautisha maeneo kutokana na shughuli ambazo zitakuwa zinafanywa katika eneo husika.
“Tangu mwaka 1964, ni awamu hii ya saba ndiyo imetoa kipaumbelle katika masuala ya upangaji wa miji, kwanza taasisi maalum ya miji imeundwa.
Sheria ya Mipango Mji iliyotungwa mwaka 1955 imefanyiwa kazi katika awamu hii na rasimu ya Sheria mpya “Planning and Development” imepatikana,” alifafanua Waziri wa Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira, Mhe. Salama Aboud Talibkatika taarifa yake ya mafanikio ya mpango wa ardhi kuanzia 1964.
Aliendelea kusema kuwa ndani ya Awamu ya Saba ya SMZ utekelezaji wa Mpango wa Matumizi ya Ardhi wa mwaka 1968 umepata nguvu zaidi kwa kurudisha tena dhana adhimu iliyotungwa baada ya Mapinduzi ya kuwa na kitovu cha mji “Ngambo tuitakayo”.
Mhe. Salama alitaja maeneo mapya ya starehe, biashara na utamaduni ambayo yatapangwa katika kipindi cha Awamu hii ya Saba kuwa ni Mji wa kibiashara ambao utakuwa Kinazini, Kitovu cha biashara kitakuwa Mkunazini-Kariakoo, kitovu cha michezo na utamaduni ambacho kitakuwa Maisara-Mnazimmoja, Kitovu cha kijamii ambacho kitakuwa Michenzani-Rahaleo-Miembeni pamoja na Kitovu cha makumbusho ambacho kitakuwa Mnazimmoja Maisara.
Kwa mpangilio huu wa maeneo kutokana na shughuli mbalimbali itaipandisha Zanzibar katika hadhi ya ngazi za kimataifa katika shughuli za kitalii na kiuchumi, kwani hata idadi ya watalii itaongezeka mara dufu ya wale ambao waikuwa wakija kipindi cha nyuma.
Ni wakati sasa wa kuiona Zanzibar Mpya ikiwa katika muonekano wa kibiashara hasa katika kipindi hiki ambacho Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inataka kukimbia kufikia uchumi wa kati.
Kupitia Zanzibar Mpya, vivutio vingine vinavyopatikana ndani ya Tanzania kama Mlima Kilimanjaro, Mbuga za Wanyama, Nyumba mbalimbali za Makumbusho pamoja na tamaduni za watanzania zitafahamika zaidi.
Hongera SMZ kwa kuona umuhimu wa utekelezaji wa mpango huo ambao umechukua miaka mingi hadi kutekelezwa kwake.
Post a Comment