Viongozi wa CHADEMA Jimbo la Singida Mashariki wajiuzulu
Katibu mwenezi wa Chama hicho Theotimi Mughanga na mwenyekiti wa Bawacha Bibianna Benedicto wakizungumza na waandishi wa habari leo wilayani Ikungi.
...........................................
CHAMA cha Demokrasi na Maendeleo(CHADEMA)jimbo la Singida Mashariki wilayani Ikungi mkoani Singida kimepata pigo baada ya viongozi wake wa wawili kujiuzulu uongozi kwa madai ya kutothaminiwa na kuongozwa kidikteta na mbunge wa jimbo hilo Tundu Lissu.
Viongozi hao waliojiuzulu ni Katibu mwenezi wa Chama hicho Theotimi Mughanga na mwenyekiti wa Bawacha Bibianna Benedicto.
Wakizungumza na waandishi wa habari leo jimboni humo viongozi hao wamesema uamuzi huo wameufikia wenyewe bila ya kushinikizwa na mtu huku wakidai chama hicho kukosa muelekeo na kupoteza imani na matumaini kwa wananchi waliowapigia kura.
"Tunapenda kuwaambia wana CHADEMA wa jimbo la singida mashariki huu ni uamuzi wetu wenyewe na hatujashawishiwa na mtu yoyote"wamesisitiza.
Wametaja sababu nyingine kuwa ni kuminywa kwa demokrasia ,kutotekelezwa kwa ahadi mbalimbali za mbunge wao Lissu.
"Katika kipindi cha uchaguzi mkuu wa mwaka 2010-2015 Lissu alitoa ahadi nyingi ambazo hajazitekeleza hali inayotufanya sisi kuona aibu na kusutwa na dhamira zetu kwa wananchi tuliowaomba ridhaa ya kuwatumikia jimboni", wamesema.
Aidha wamesema wamechoshwa na tabia ya mbunge kuzuia wananchi kuchangia shughuli za kimaendeleo na kupora madaraka ya viongozi wa chama jimboni.
Katika hatua nyingine, Mughanga na Benedicto wamesema wanamuunga mkono rais Dk. John Magufuli kwa dhamira yake ya dhati ya kupambana na rushwa,ufisadi na kuleta uwajibikaji kwa watumishi wa umma na kutekeleza kwa vitendo sera ya elimu bure.
Post a Comment