Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Yustino Ndugai (Mb) akizungumza na Balozi wa Jamhuri ya Kiislam ya Iran Nchini Tanzania Mhe. Mohammad Dehghani aliefika Ofisini kwake Dodoma kwa ajili ya kuwasilisha salaam na mualiko rasmi kutoka kwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Kiislam ya Iran ukimualika Mheshimiwa Ndugai kutembelea Bunge la Iran kwa lengo la kuimarisha uhusiano wa mabunge haya mawili.
.................................
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Yustino Ndugai (Mb) amesema Bunge la Tanzania litaendelea kudumisha mahusiano yaliyopo na Bunge Irani ili kubadilishana uzoefu katika maeneo mbalimbali.
Mhe. Ndugai ameyasema hayo Mjini Dodoma leo alipokutana na Balozi wa Jamhuri ya Kiislam ya Iran Nchini Tanzania Mhe. Mohammad Dehghani aliefika Ofisini kwake Dodoma kwa ajili ya kuwasilisha salaam na mualiko rasmi kutoka kwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Kiislam ya Iran ukimualika Mheshimiwa ndugai kutembelea Bunge la Iran kwa lengo likiwa ni kuimarisha uhusiano wa nchi zetu mbili.
Nashukuru kwa Salaam hizi kutoka kwa Spika wa Bunge la Iran na naahidi kuzifikisha salaam hizi kwa Waheshimiwa Wabunge na pia Ofisi yangu itatolea taarifa juu ya mwaliko huu na kujipanga kutembelea Bunge la Irani kwa kadri muda utakavyoruhusu. Alisema Mhe. Ndugai
Pamoja na mwaliko huo wa Kibunge kutoka kwa Spika wa Bunge la Iran, Balozi huyo Irani pia alitumia fursa hiyo kuwasilisha ombi la Rais wa Iran Mhe. Hassan Rouhani la kumwalika Mhe. Ndugai ili aweze pia kuhudhuria Mkutano wa Kimataifa wa kusaidia kutatua mgogoro wa muda mrefu kati ya Palestina na Israel uliopangwa kufanyika tarehe 22 Februari, 2017 Jijini Tehran jambo ambalo pia aliahidi kulitolea majibu hivi karibuni.
Akizungumzia namna ya kuimarisha mahusiano ya Mabunge haya mawili, Mhe. Ndugai alisisitiza umuhimu wa kuanzisha Chama Rafiki cha Kibunge (Parliamentary Friendship Group) baina ya Bunge la Tanzania na Bunge la Iran kwa kuwa kitasaidia sana Wabunge wa Mabunge yote mawili kubadilishana uzoefu na kuimaisha uhusiano uliodumu kwa muda mrefu baina ya Tanzania na Iran.
Kwa upande wa Mhe. Mohammad Dehghani aliipongeza Tanzania kwa kuendelea kuimarisha demokrasia ambayo kwa kiasi kikubwa nchi yake ya Iran imekuwa ikithamini na kuheshimu misingi imara iliyowekwa na Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere.
Nchi yenu imekuwa na historia kubwa sana ya kimahusiano na Iran, pamoja na mambo yote napongeza sana jitihada mnazozichukua kuimarisha demokrasia ikiwa ni pamoja na kuongeza idadi ya Wabunge wanawake Bungeni na nimatumaini yetu kuwa mtayafikia malengo mliyojiwekea ya kufikia idadi ya 50 kwa 50. Alisema Bolozi Dehghani
|
Post a Comment