Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter
Muhongo (katikati) akizungumza wakati wa Kikao cha kujadili taarifa ya Kamati iliyoundwa na Profesa Sospeter Muhongo mwezi Februari mwaka
huu ili kutathmini migogoro kati mgodi wa Acacia NorthMara na wananchi
wanaozunguka mgodi huo, kilichofanyika
wilayani Tarime. Kushoto kwake ni Mkuu
wa wilaya ya Tarime, Glorious Luoga na wa Pili kushoto ni Mbunge wa Tarime
Vijijini, John Heche.
Awali Katibu wa Kamati hiyo, Mhandisi John Shija kutoka
Wizara ya Nishati na Madini, alisema kuwa Kamati hiyo ilikuwa na wajumbe
27 ambapo wataalam wa Serikali walikuwa 19, wawakilishi wa mgodi 4 na wawakilishi wa wananchi kupitia Ofisi ya
Mbunge wa Tarime vijijini wakiwa 4.
Mhandisi Shija alisema kuwa Kamati ilipewa hadidu
za rejea 16 ambapo baadhi ya hadidu hizo zinahusu masuala ya fidia ya ardhi,
athari za mgodi kwa mazingira, binadamu na mifugo, uvamizi wa mgodi unaofanywa
na vijana, askari wanaolinda mgodi kunyanyasa wananchi na wachimbaji wadogo kupatiwa
maeneo ya kuchimba madini.
“Katika kuyachunguza masuala yaliyomo kwenye
hadidu za rejea, Kamati ilipitia taarifa mbalimbali na kuwahoji wananchi, pia
ilikutana na viongozi wa mgodi wa NorthMara, Wilaya, Watendaji wa Halmashauri,
Kata, Vijiji na kukagua shughuli za Mgodi na maeneo yanayozunguka Mgodi,”alisema
Mhandisi Shija.
kuhusu maeneo ambayo Mgodi uliwaambia wananchi
wasiyaendeleze huku maeneo hayo yakifyekwa wakati wa uthamini, Kamati
ilipendekeza kuwa Mgodi ulipe fidia ya mazao yaliyofyekwa na fidia ya usumbufu.
“ Kwa kuwa kwa mujibu wa sheria, fidia ya usumbufu
ni asilimia 8 ya fidia kuu (Fidia ya mazao),
Kamati inapendekeza mgodi ulipe fidia hiyo kwa kiwango cha asilimia
50 badala ya Nane,” alisema mmoja wa
Wajumbe wa Kamati hiyo.
Kuhusu wananchi ambao walikataa kufanyiwa uthamini
katika maeneo ya MjiniKati na Nyabichune wilayani Tarime, Kamati ilipendekeza
kuwa mgodi ufanye tathmini ndani ya wiki Tatu kwa mujibu wa hali ya mwaka 2012,
na wananchi hao wakiendelea kukataa, Serikali itawafanyia uthamini na kuutaka
Mgodi uwalipe kwa mujibu wa viwango vya serikali.
|
Post a Comment