Hili Hapa Tamko la Wizara ya Afya Kuhusu Matumizi na Usambazaji wa Vilainishi
Wizara ya Afya, Maendeleo
ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imekuwa ikitekeleza afua mbalimbali za
mapambano dhidi ya maambukizi ya VVU nchini ambazo zimepelekea kupungua kwa
viwango vya maambukizi ya VVU kitaifa kutoka wastani wa asilimia 7 mwaka
2007-2008 hadi kufikia asilimia 5.1 mwaka 2011-2012.
Mafanikio haya yamefikiwa
kutokana na ushirikiano wa karibu kati ya Wizara na wadau mbalimbali wa maendeleo
pamoja na wale wa utekelezaji wa moja kwa moja wanaofanya kazi na mikoa yote
Tanzania bara.
Aidha kumekuwa na uitikiaji mzuri kutoka kwa wananchi katika
utekelezaji wa afua hizo.
Sambamba na mafanikio
haya, tafiti mbalimbali hapa nchini zimethibitisha kuwepo kwa kiwango cha juu cha
maambukizi ya VVU miongoni mwa makundi maalum yaliyo katika hatari zaidi ya
maambukizi kuliko kiwango kilichopo miongoni mwa jamii ya kawaida. Makundi haya
ni pamoja na Wanawake wanaofanya biashara ya ngono ambayo maambukizi ya VVU ni
asilimia 26, Watu wanaojidunga sindano za madawa ya kulevya (asilimia 36) na
Wanaume wanaoshiriki ngono baina yao (asilimia 25). Aidha, makundi haya
yamekuwa na muingiliano wa karibu sana na wana jamii ya kawaida, na hivyo
kupelekea hatari ya kutofanya vizuri katika udhibiti wa maambukizi ya VVU
nchini.
Hali hii ilisababisha
kuwepo na umuhimu wa kuongeza nguvu katika afua mbalimbali za kukabiliana na
ongezeko la maambukizi ya VVU miongoni mwa makundi haya, pamoja na jamii ya
kawaida ili kudhibiti VVU. Kwa mantiki hiyo, Wizara kwa kushirikiana na wadau mbali
mbali walikubaliana mikakati mahsusi ya kutoa huduma bora na rafiki kwa watu wa
makundi maalum kwa kuzingatia sheria, taratibu, mila na desturi za taifa letu.
Pamoja na nia njema na
jitihada za pamoja baina ya Wizara na wadau katika mapambano dhidi ya UKIMWI, imebainika
kwamba baadhi ya wadau wanaotekeleza shughuli za makundi maalum wamekuwa
wakikiuka taratibu za kiutendaji hasa suala la kuihusisha Wizara na Mikoa
husika wanakofanyia kazi kuhusu uanzishwaji na/au utekelezaji wa baadhi ya shughuli
wanazozifanya. Aidha pia katika baadhi ya maeneo, wadau hao wamekuwa
wakitekeleza shughuli ambazo ziko kinyume na makubaliano waliyoingia na Wizara
ya Afya.
Miongoni mwa shughuli zinazokinzana
na mila na desturi zetu ni pamoja na usambazaji wa vilainishi. Ni kweli kuwa
Wizara imezuia usambazaji wa vilainishi na tayari tumewasiliana na wadau hao
ambao wameahidi yafuatayo:
- Kukusanya
vilainishi vilivyokuwa vimesambazwa na kuhakikisha kuwa vinateketezwa
- Imekubalika
pia kuwa wadau kwa kushirikiana na Wizara watakaa pamoja na kuangalia
endapo pana fedha ambazo zingetumika kununua vilainishi, basi fedha hizo
ziweze kupangiwa matumizi stahiki kulingana na vipaumbele vya Wizara na
taifa kwa ujumla.
Wizara inawapongeza na kuwashukuru
wadau wote kwa jitihada za dhati zinazoendelea kutekelezwa na katika kusimamia
kikamilifu miongozo inayotolewa na Wizara yenye lengo la udhibiti wa ugonjwa wa
UKIMWI.
Imetolewa
na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
19
Julai 2016
Post a Comment