Utumikishwaji wa Watoto
bado ni tatizo kubwa nchini ambapo kati ya watoto watatu wenye umri wa miaka 5
- 17, mtoto mmoja anafanya kazi ambazo ni hatarishi katika maisha yake kiafya,
kimwili na kisaikolojia.
Akizungumza katika uzinduzi
wa Ripoti ya Matokeo ya Utafiti wa Utumikishwaji wa Watoto Tanzania wa Mwaka
2014, Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na
Walemavu, Dkt. Abdallah Posi amesema tatizo la utumikishwaji wa watoto bado ni
kubwa hapa nchini na hivyo ni wajibu wa jamii kuwekeza katika elimu badala ya
kuwaajiri au kuwatumikisha watoto.
“Utumikishwaji wa watoto
bado ni tatizo kubwa duniani kote si Tanzania pekee, kwani kwa mujibu wa
takwimu za Shirika la Kazi Duniani (ILO), asilimia 11 ya watoto wote duniani
(watoto milioni 264) wenye umri wa miaka 5 – 17 wanatumikishwa kwenye ajira za
aina mbalimbali,” amesema Dkt. Posi.
Dkt. Posi amesema kwa
mujibu wa ripoti ya utumikishwaji wa watoto Tanzania wa mwaka 2014/15, watoto
wenye umri wa miaka 5 – 17, watoto milioni 4.2 ambao ni sawa na asilimia 28.8
wanatumikishwa katika kazi mbalimbali za kiuchumi.
|
Post a Comment