Serikali
imehitimisha ubia kati ya Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL), na Kampuni ya Bhart
Airtel ya India kwa kuilipa kampuni hiyo Shilingi Bilioni 14.9 na hivyo
kuirudisha TTCL mikononi mwa Serikali kwa asilimia miamoja.
Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa amesema hatua hiyo ni mkakati wa
Serikali wa kuiwezesha TTCL kujitegemea ili kuzalisha faida, Kuimarisha
Miundombinu yake, na kutoa gawio Serikalini.
“Tunawataka TTCL
mjipange vizuri mjitangaze ili muwe kampuni kubwa na bora ya mawasiliano hapa
nchini”, amesema Prof. Mbarawa.
Waziri Prof. Mbarawa
amesema katika kuiongezea nguvu TTCL Serikali itawapa kituo cha Kutunza Taarifa cha Kijitonyama (Internet Data
Center) ili ikisimamie na hivyo kujipatia mapato kupitia gharama za uendeshaji
na usimamizi wa kituo hicho.
|
Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akiongea na wafanyakazi wa
Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL),Jijini Dar es salaam.
Amewataka wafanyakazi
wa TTCL kufanya kazi kwa bidii, kasi, uaminifu, ubunifu na kuulinda Mkongo wa
Taifa ili uwawezeshe kuwa na huduma bora na za uhakika wakati wote.
“Tumetumia fedha za
mkongo wa taifa kumlipa mbia mwenzenu bhart airtel ili kuiwezesha TTCL
kumilikiwa na Serikali kwa asilimia miamoja hivyo changamoto inayowakabili sasa
ni kufanya mabadiliko makubwa katika upande wa kutafuta masoko ili kuweza
kuongeza idadi ya wateja na kufanya kazi kwa faida”, amesisitiza Prof. Mbarawa.
Aidha Prof Mbarawa
amesema katika kuijali TTCL, Serikali imeipa masafa ya 1800 na masafa ya 2100
na itawaongezea masafa ya 800 yatakayowawezesha kuwa na huduma ya 4G LTE
yenye mtandao wenye kasi na hivyo
kuiongezea wateja hususani katika huduma za data.
|
|
Ofisa Mtendaji Mkuu wa
kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) Dkt .
Kamugisha Kazaura akifafanua jambo kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa wakati alipofanya mazungumzo na wafanyakazi
wa kampuni hiyo,jijini Dar es salaam.
Kwa upande wake,
Mwenyekiti wa Bodi ya TTCL, Profesa
Tolly Mbwete amesema TTCL imejipanga kutoa huduma zake katika maduka makubwa,
hospitali, stesheni za treni, mabasi ya mwendokasi na viwanja vya ndege katika
jiji la Dar es salaam na Miji mikubwa ili kuwawezesha wananchi kunufaika na
huduma za mtandao na data wakati wote.
Naye, Mtendaji Mkuu wa TTCL Dkt. Kamugisha Kazaura, ameishukuru
Serikali kwa fursa mbalimbali inazoipa kampuni hiyo na kumhakikishia Waziri
Prof Mbarawa kuwa katika kipindi cha miezi mitatu ijayo matokeo ya mkakati wa
mabadiliko ya kibiashara yataanza kuonekana.
Dkt. Kazaura amesema
kuwa tayari watumishi wenye mtazamo wa mabadiliko ya kiteknolojia wameajiriwa
na wengine watapewa mafunzo ili kuhimili soko la kibiashara na kuiwezesha TTCL
kunufaika na miundombinu yake iliyopo nchi nzima.
Waziri Prof. Mbarawa
alikuwa akizungumza na Menejimenti na wafanyakazi wa TTCL ikiwa ni utaratibu
aliojiwekea kuzungumza na wafanyakazi na taasisi zilizopo chini ya Wizara yake.
|
Post a Comment