Waziri wa Nishati na
Madini, Profesa Sospeter Muhongo ametoa agizo
la kupimwa tena kwa maji yanayotoka katika vyanzo vinavyozunguka mgodi
wa dhahabu wa Acacia North Mara ili kujiridhisha kuwa hayana athari kwa
binadamu, mifugo na mazingira.
Agizo hilo alilitoa
wilayani Tarime wakati akizungumza na
wananchi katika vijiji vya Matongo, Nyabichune, Mrwambe na Nyakungulu ambavyo
vinazunguka mgodi huo wa dhahabu.
Profesa Muhongo alitoa
agizo hilo baada ya Kamati iliyokuwa ikitathmini migogoro kati ya Mgodi huo na
wananchi kueleza kuwa matokeo ya vipimo vya
maabara vinaonyesha kuwa maji hayo yana viwango vinavyokubalika kwa
matumizi ya binadamu, mifugo na mazingira na kupendekeza kuwa wataalam wa afya
na mifugo wafanye utafiti zaidi ya suala hilo ili kujiridhisha zaidi.
“Viwango vinavyopaswa
kutumika katika upimaji wa maji haya lazima viwe vya Shirika la Afya Duniani
(WHO) hivyo zichukuliwe tena sampuli za maji wakati wa kiangazi na wakati wa
mvua na zipimwe tena. Sampuli hizo zigaiwe kwa makundi mbalimbali ikiwemo
wananchi, Mkuu wa wilaya, Kamati iliyofanya tathmini na mimi mwenyewe ili kila
kundi lipeleke katika maabara inayoaminika na baadaye kuwasilisha majibu ya
uchunguzi,” alisema Profesa Muhongo.
|
Post a Comment