TANZANIA imeeleza Kulani Vikali Matukio ya Uvunjifu wa Amani
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.
Samia Suluhu Hassan, akifuatilia kwa makini ufunguzi wa mkutano wa 27 kwa Wakuu
wa Nchi na Serikali wa Nchi Wanachama wa
Umoja wa Afrika AU ulioanza jana katika Ukumbu wa KCC mjini Kigali Rwanda.
Makamu wa Rais amemuwakilisha Rais John Magufuli kwenye mkutano huo.
..............................
Tanzania imeuhakikishia
Umoja wa Afrika (AU) kwamba itaendelea kufanya kazi kwa karibu na nchi
wanachama wa AU katika kujadili changamoto za kiusalama zinazolikabili Bara la
Afrika kwa njia ya mazungumzo na upatanishi kama inavyoelekeza Katiba ya umoja
huo.
Makamu wa Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ametoa kauli hiyo wakati
akichangia mada kuhusu Hali ya amani na usalama katika Bara la Afrika katika
Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (AU) uliofanyika hapa
Kigali, Rwanda.
Mheshimiwa Samia alisema
Tanzania inasikitishwa na inalaani vikali matukio ya uvunjifu wa amani
yanayoendelea kujitokeza katika baadhi ya nchi za Kiafrika kiasi cha kutishia
usalama wa raia.
Alielezea mauaji ya Hafsa
Mossi, aliyekuwa Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki na waziri wa zamani wa
Burundi na mapigano ya hivi karibuni Sudan ya Kusini ambapo mamia ya raia
wasiokuwa na hatia waliuwawa na wengine maelfu wameachwa bila makazi kwamba ni
muendelezo wa uvunjifu wa amani katika nchi hizo.
Aliwataka wadau husika katika
nchi za Burundi na Sudan ya Kusini kushiriki kikamilifu katika mazungumzo yanayoendelea
kwa kuwa hiyo ndiyo njia muafaka ya kuleta amani, usalama na utulivu wa kudumu katika nchi zao.
Aidha, Makamu wa Rais ambaye alimwakilisha Rais John Magufuli katika mkutano huo aliiomba Jumuiya ya
Kimataifa kuendelea kuisadia Sudan ya Kusini katika kutafuta ufumbuzi wa kudumu
katika mgogoro ulioikumba nchi hiyo.
Akichangia kuhusu mageuzi
ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa Makamu wa Rais alisema Tanzania kwa
ujumla inaunga mkono msimamo wa Afrika wa kuwa na viti viwili katika baraza
hilo na kura ya turufu bila ya masharti yoyote.
Wakati wa ufunguzi wa
mkutano huo viongozi walisisitiza suala la kuimarisha umoja baina ya nchi
wanachama na kusema hiyo ndiyo nguzo muhimu katika kukuza uchumi na ustawi wa
wananchi wa Bara la Afrika.
Katika mkutano huo kulikuwa
na uzinduzi wa pasi ya kusafiria ya Afrika ambayo ilitolewa kwa Mwenyekiti wa
AU, Rais Idris Deby wa Chad na nchi mwenyeji wa mkutano, Rais Paul Kagame wa
Rwanda.
Mkutano huo ambao
ulizungumzia pia gharama za kuendesha umoja huo na masuala ya haki za wanawake ulihudhuriwa
na Wakuu wa Nchi zaidi ya 35, Marais wastaafu, wake wa Marais pamoja na viongozi
wa serikali.
Post a Comment