Baadhi ya Wasimamizi wa Uchaguzi, Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi ngazi ya jimbo na Kata na Maafisa wa Uchaguzi wakifuatilia mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kutekeleza majukumu yao wakati wa Uchaguzi mdogo utakaofanyika Januari 22, 2017 leo mjini Dodoma.
................................... Tume ya Taifa ya Uchaguzi imewataka Wasimamizi wa Uchaguzi, Wasimamizi wa Uchaguzi mdogo wa Udiwani utakaofanyika katika Kata 20 za Tanzania Bara na Ubunge katika jimbo la Dimani Visiwani Zanzibar Januari 22, 2017 kuzingatia Sheria, Kanuni na Maadili ili Uchaguzi huo uwe Huru na wa Haki.
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Bw. Kailima Ramadhan wakati akifungua mafunzo ya siku 3 ya Wasimamizi wa Uchaguzi, Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi ngazi ya jimbo na Kata na Maafisa wa Uchaguzi leo mjini Dodoma.
Mkurugenzi Kailima amewataka Wasimamizi hao kuzingatia matakwa ya Katiba, Sheria, Kanuni na miongozo mbalimbali katika kushughulikia mambo yatakayojitokeza wakati wa uchaguzi huo.
Katika kutimiza majukumu yao wawe tayari kutoa ufafanuzi juu masuala mbalimbali kwa kuzingatia sheria na kutokuwa tayari kukubali kuyumbishwa na mtu yeyote atakayekiuka miongozo, sheria na kanuni za Uchaguzi.
Amewataka Wasimamizi hao watende mambo yote kwa kuzingatia kanuni na Sheria na kutoa maamuzi sahihi kwa mustakabali wa Taifa na kuwasisitiza kuepuka kutoa upendeleo katika maamuzi wanayoyafanya na wasikubali kuyumbishwa na matakwa ya baadhi ya watu. |
Post a Comment