Header Ads

Wajue Mabilionea wanane wanaomiliki mali Sawa na nusu ya Watu Duniani

Utafiti uliofanywa na shirika la Oxfam la Uingereza unaonesha mabilionea wanane wanamiliki mali sawa na mali ya watu 3.6 bilioni kwa pamoja.
Takwimu za shirika hilo, ambazo zimepingwa na baadhi ya wakosoaji, zinatokana na maelezo na habari za kina zilizokusanywa na shirika hilo, na zinaonesha pengo kati ya matajiri na maskini ni kubwa "kuliko ilivyodhaniwa awali".
Ripoti hiyo ya Oxfam imetolewa wakati mkutano mkubwa kuhusu uchumi wa dunia unaanza mjini Davos.
Mark Littlewood, wa Taasisi ya Masuala ya Uchumi, amesema Oxfam badala yake wanafaa kuangazia njia ya kusisimua ukuaji.
"Kama shirika linalopiga vita umaskini, Oxfam wanaonekana sana kuangazia zaidi matajiri," mkurugenzi mkuu huyo wa shirika hilo la ushauri amesema.
Kwa wale ambao wana malengo ya "kuangamiza kabisa umaskini uliokithiri", sana wanafaa kuangazia hatua za kusisimua ukuaji wa uchumi, ameongeza.
Ben Southwood, ambaye ni mkuu wa utafiri katika Taasisi ya Adam Smith, amesema la muhimu zaidi si kiasi cha mali inayomilikiwa na watu matajiri zaidi duniani, bali ni hali ya maisha ya watu maskini zaidi duniani, ambayo inaimarika mwaka baada ya mwaka.
"Kila mwaka, tunapotoshwa na takwimu za Oxfam. Takwimu ziko sawa - zinatoka kwa Credit Suisse - lakini ufasiri wa takwimu hizo si sahihi."
'Mkutano wa Davos'
Mkutano unaofanyika mjini Davis, Uswizi huwavutia viongozi wengi wa kisias ana kibiashara duniani.
Katy Wright, mkuu wa mambo ya nje wa Oxfam, anasema ripoti hiyo imesaidia shirika hilo kuwauliza maswali viongozi wa kisiasa na kiuchumi.
"Tuna uhakika kwamba Davos ni mkutano tu mwingine wa kupiga gumzo miongoni mwa viongozi na watu wenye ushawishi duniani, lakini tunahitaji kujaribu na kupata mwelekeo," aliongeza.

Mabilionea wanane matajiri zaidi duniani

1. Bill Gates (US): mwanzilishi wa Microsoft (utajiri wake $75bn)
2. Amancio Ortega (Spain): mwanzilishi wa Zara na mmiliki wa Inditex (utajiri wake $67bn)
3. Warren Buffett (US): mwenyehisa mkubwa Berkshire Hathaway (utajiri wake $60.8bn)
4. Carlos Slim Helu (Mexico): mmiliki wa Grupo Carso (utajiri wake $50bn)
5. Jeff Bezos (US): mwanzilishi na afisa mkuu mtendaji wa Amazon (utajiri wake $45.2bn)
6. Mark Zuckerberg (US): mwanzilishi mwenza na afisa mkuu mtendaji wa Facebook (utajiri wake $44.6bn)
7. Larry Ellison (US): mwanzilishi mwenza na afisa mkuu mtendaji wa Oracle (utajiri wake $43.6bn)
8. Michael Bloomberg (US): mmiliki wa Bloomberg LP (utajiri wake $40bn)
Chanzo: Orodha ya mabilionea ya Forbes, Machi 2016

No comments

Powered by Blogger.