Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (MAZINGIRA) na mwenyekiti wa kikao hicho Januari Makamba akizungumza na waandishi wa habari(hawapo pichani) kuhusu mkakati wa Serikali katika kupambana na uvuvi haramu nchini mara baada ya kumalizika kwa kikao kilichohusisha Wizara Saba kushoto ni Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi Charles Tizeba. .............................
Na Beatrice Lyimo-MAELEZO
Serikali imewaagiza wakurugenzi nchini hasa kwenye maeneo wanayojishughulisha na uvuvi kuwachukulia hatua maafisa uvuvi wanaoshindwa kutimiza wajibu kwa kushindwa kuzuia uvuvi haramu.
Akizungumza baada ya kikao cha kamati kilichohusisha Wizara saba za Maliasili, Ulinzi, Nishati na Madini Tamisemi, Kilimo, Mifugo na Uvivi pamoja na Mambo ya Ndani Naibu Waziri TAMISEMI Suleiman Jaffo aliwataka watendaji hao kutumia agenda ya kupambana na uvuvi haramu kuwa agenda ya kudumu katika vikao vyao.
Alisema kuwa maafisa uvuvi hao wanatakiwa kupimwa wajibu na utendaji kazi kwa kuangalia ni kiasi gani wanajihusisha na masuala mazima ya kupambana na uvuvi wa kutumia mabomu.
“Kuna baadhi ya mafisa uvuvi wanahusika na vitendo vya uvuvi haramu nchini hivyo kuanzia kesho wataanza kupimwa wajibu wao na kwa atakayeshindwa kutimiza wajibu atatolewa katika nyazifa hiyo”.
Kwa upande wake Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira Januari Makamba alisema kuwa nchi yetu inaeneo kubwa la bahari na kwa miaka kadhaa nchi yetu imekuwa na changamoto ya uvuvi haramu, hivyo tumeona kuna haja ya kuchukua hatua ya haraka katika kupambana na uharamia huo.
Akifafanua zaidi kuhusu hilo Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi Charels Tizeba alisema kuwa jambo la uvuvi haramu lisipochukuliwa kwa umakini litapelekea kuathiri uchumi wa nchi hivyo lengo la Serikali ni kukomesha uharibifu unaojitokeza sasa.
Alisema ni aibu kwa taifa letu la Tanzania kuendelea kuvua kwa njia haramu kwani nchi nyingi kwa sasa zimeondoka katika uvuvi wa namna hiyo.
Naye Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mwigulu Nchemba alitoa wito kwa watanzania wote kushirikiana na Serikali katika kufichuwa wale wanaohusika na uvuvi haramu.
Mwigulu Nchemba alisisitiza kuwa “kila mtanzania anawajibu wa kuwa makini katika kulinda rasilimali za majini tulizo nazo”.
Kikao hicho ni utekelezaji wa agizo la Makamu wa Rais la kupambana na uvuvi haramu ambapo maazimio hayo yatafanyiwa kazi na kuahidi kukutana baada ya miezi sita kwa ajili ya kutafakari hatua zilizochukuliwa pamoja na kurekebisha pale patakapoonekana pana changamoto.
|
Post a Comment