( MTAZAMO ) Ujenzi wa Uchumi wa Viwanda Kupitia Sekta ya Uvuvi Inawezekana
Na Ismail Ngayonga,
MAELEZO
DAR ES SALAAM.
KATIKA kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025, Serikali imekusudia kuweka mkazo katika ujenzi vya viwanda ili kuharakisha kasi ya ukuaji wa maendeleo kwa wananchi na taifa kwa ujumla.
Ili kufikia lengo hilo, Serikali imeanisha sekta kuu za kiuchumi ikiwemo mifugo, uvuvi, kilimo, ardhi, nishati, maji na kadhalika kuwa vipaumbele vikuu vya kimkakati vilivyojengewa uwezo wa kutumia rasilimali na malighafi ilizonazo hususani katika kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.
Idadi ya viwanda hapa nchini imeendelea kuongezeka kutoka viwanda 125 Mwaka 1961 hadi kufikia viwanda 54,422 mwaka 2016, Aidha, kati ya hivyo, viwanda vikubwa vinavyoajiri kuanzia watu 100 ni 247, viwanda vya kati vinavyoajiri kati ya watu 50 na 99 ni 170, viwanda vidogo vinavyoajiri kati ya watu watano na 49 ni 6,907.
Kulingana na takwimu hizo, ni dhahiri kuwa asilimia 99.15 ya viwanda vyote nchini ni viwanda vidogo sana na viwanda vidogo, ambavyo hutegemea sekta zisizo rasmi katika kutengeneza ajira za moja kwa moja kwa wananchi.
Uvuvi ni miongoni wa shughuli kuu ya kiuchumi kwa wananchi wengi wanaozunguka maeneo ya ukanda wa bahari, mito na maziwa, ambapo hutumia mazao ya rasilimali za maji kwa ajili ya lishe na kujiongezea kipato.
Akizungumza hivi karibuni Jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Yohana Budeba anasema Serikali imeanza mchakato wa kuwahamisha wananchi kuwekeza katika viwanda ili kuongeza thamani ya mazao ya uvuvi nchini.
Dkt. Budeba anasema hadi sasa jumla jumla ya viwanda vidogo vidogo 48 vya kuchakata samaki, ambapo 36 vipo katika ukanda wa pwani, 11 ukanda wa ziwa Victoria na 1 ukanda wa ziwa Tanganyika, ambapo vyote kwa pamoja vimekusudia kuongeza ajira na kuondoa umaskini kwa Watanzania.
“Mwaka 2015 jumla ya tani 42,000 za samaki ziliuzwa na jumla ya Tsh. Bilioni 1.6 ziliweza kukusanywa, hivyo tunaamini kuwa ujenzi wa viwanda utaweza kuiwezesha sekta hii kuongeza mchango wake katika pato la taifa kutoka asilimia 2.4 ya sasa” anasema Budeba.
Dkt. Budeba anasema Serikali imekusudia kujenga vituo vya kutotolesha samaki ili kuwezesha Tanzania kuwa kuzalisha tani 50,000 za samaki katika kipindi cha miaka mitano ijayo, ambapo kwa sasa Serikali ipo katika mazungumzo na Serikali ya Japan kwa ajili ya kujenga vituo katika mikoa ya Tanga, Morogoro na Rukwa.
Anaongeza kuwa kusudio la ujenzi wa vituo hivyo ni pamoja na kuanzisha mpango wa uzalishaji wa mbegu bora za samaki ikiwemo sato na sangara, ambao wamekuwa wakipendwa na wananchi kwa ajili ya matumizi ya kitoweo ili kuchangia lishe bora.
Kwa mujibu wa Dkt. Budeba anasema ili kuhakikisha wananchi wanafuga kwa kuzingatia kanuni za ufugaji bora, Serikali imekusudia kusambaza Wataalamu katika kila Kata nchini hatua inayolenga kuwajengea uwezo wafugaji kufuga kisasa zaidi.
Akifafanua zaidi Dkt. Budeba anasema Serikali itaendelea kuongeza idadi ya waatalamu wa uvuvi nchini, ambapo imepanga kuzalisha na maafisa ugani 5000 kupitia vyuo vya mafunzo ya uvuvi vya Mbegani- Bagamoyo, Nyegezi-Mwanza na Kigoma.
Aidha Budeba anasema Serikali inaendelea kuwahamisha wafugaji kujiunga katika vyama vya ushirika wa msingi vilivyopo katika Halmashauri, kwani kupitia vikundi huweza kutoa mikopo na ruzuku mbalimbali.
“Mwaka 2015/16 Serikali ilitoa kiasi cha Tsh. Milioni 440 kwa vikundi 73 vya ushirika wa wafugaji samaki, na pia ruzuku katika vifaa vya uvuvi na vyakula vya samaki, na mashirika ya hifadhi ya jamii ikiwemo NSSF nao wameanza utaratibu huu” anasema Budeba.
Akizungumzia kuhusu shirika la Uvuvi Nchini (TAFICO), Dkt. Budeba anasema Serikali imekusudia kurejesha hadhi ya shirika hilo, ambapo imepanga kununua meli tano kubwa za kisasa ili kuliwezesha shirika hilo kufanya shughuli za uvuvi katika maji ya kina kirefu.
Jitihada za Serikali zinazoendelea kuelekezwa katika kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara na kuendeleza viwanda vidogo, zitasaidia wananchi walio wengi zaidi kupata ajira, kuongeza kipato na kupunguza umasikini kupitia uvuvi.
Uchumi wa viwanda kupitia sekta ya uvuvi utaliweka taifa letu kuwa katika kundi la mataifa yanayozalisha bidhaa bora na zenye ushindani wa soko la kimataifa badala ya kuwa chanzo cha malighafi na soko la bidhaa kwa viwanda vya mataifa mengine.
Ili kufikia azma hiyo, ushirikiano na mchango wa mtu mmoja mmoja, makundi ya watu, taasisi za umma na taasisi za binafsi utahitajika, hiyo ni pamoja na kila mmoja wetu kwa uwezo wake kulenga kuwekeza katika viwanda vyetu na kupenda kununua mazao ya samaki yanayozalishwa nchini.
Post a Comment