Miji Sita ya Zanzibar Kufanyiwa Mipango ya Matumizi Bora ya Ardhi Ifikapo 2020
Na. Lilian Lundo – MAELEZO.
SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) inatarajia kukamilisha upangwaji wa matumizi ya ardhi kwa ajili ya maboresho ya Miji Sita ifikapo 2020.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira, Mhe. Salama Aboud Talib katika mahojiano na mwandishi wa habari hii kuhusu mafanikio ya Mkakati wa Matumizi ya Ardhi Zanzibar wa mwaka 2015.
Mhe. Salama amesema kuwa kumekuwa na mafanikio makubwa katika sekta ya ardhi mara baada ya kuanzishwa kwa Idara ya Mipango Miji na Vijiji ambayo ilipelekea kuanzishwa kwa mpango mkuu wa matumizi ya Ardhi uliosaidia kwenda kasi kwa shughuli za upangaji wa matumizi ya ardhi ukilinganisha na miaka ya nyuma.
“Malengo ya Awamu ya Saba katika kupanga Miji ni kutengeneza mipango ya matumizi ya Ardhi (Master Plan) ya miji Mikuu miwili ambayo ni Zanzibar na Mji wa Chake-Chake na kufanya Mipango ya Maendeleo (Local Area Plan) ya miji midogo 14,” alifafanua Mhe. Salama.
Aliongeza kuwa kati ya miji Mikuu miwili, Mji wa Zanzibar umeshafanyiwa mipango ya matumizi ya ardhi na kati ya Miji 14, Miji 3 ya Nungwi, Chwaka na Mkokotoni imeshafanyiwa mipango yake.
Aidha amesema kuwa hadi kufikia mwaka 2020, Miji 6 itakuwa imefanyiwa mpango wa matumizi ya Ardhi. Aliitaja Miji hiyo kuwa ni Chake-Chake, Wete, Mkoa, Mkunduchi, Dunga na Mahonda.
Mhe. Salama amesema kuwa tangu mwaka 1964 ni awamu hii ya saba ndiyo inayotoa kipaumbele katika masuala ya miji, ambapo taasisi maalum ya masuala ya miji imeundwa.
Pia kumekuwa na utekelezaji wa mipango ya matumizi ya ardhi ya mwaka 1968 ambayo imepata nguvu tena kwa kurudisha dhana adhimu iliyotungwa baada ya Mapinduzi ya kuwa na kitovu cha mji “Ngambo Tuitakayo”.
Post a Comment