( MAKALA ) Miaka 53 ya Mapinduzi ya Zanzibar Sekta ya Afya Imeimarika Zaidi
Na Beatrice Lyimo-
MAELEZO
Serikali ya Zanzibar imeipa kipaumbele sekta ya afya na kutoa huduma za afya zenye ubora kwa kuwafikia wananchi wote ili kuboresha afya zao kwa kuzingatia afya bora ni raslimali muhimu kwa maendeleo endelevu.
Afya ni hali ya ukamilifu kimwili, kiakili, kijamii na kutokuwepo kwa maradhi.
Afya bora ni nguzo na raslimali muhimu katika kuchangia maendeleo ya mtu binafsi, familia na nchi hususan katika kuleta maisha bora na kupunguza umaskini.
Kwa mantiki hii afya inalenga kuwa na ustawi endelevu wa jamii, kwa kuzingatia mchango wa mtu binafsi kulingana na nafasi, uwezo na fursa zilizopo katika kuleta maisha bora.
Uhakika wa upatikanaji wa huduma bora za afya wenye lengo la kuiwezesha jamii kuwa na uwezo wa kushiriki, kuamua, kupanga na kutekeleza mikakati yao ya kuwaletea maendeleo katika ngazi mbalimbali.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Afya imedhamiria kwa dhati kuimarisha huduma za afya za kinga na tiba na kuendeleza ustawi wa watu wa Zanzibar kwa kutilia mkazo zaidi wanawake, watoto pamoja na makundi mengine yanayoishi katika mazingira magumu.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Wizara ya afya yapo mafanikio kadhaa yaliyotekelezwa na Serikali katika sekta ya afya baada ya Mapinduzi 1964 ili kuimarisha sekta hiyo katika utoaji huduma kwa wananchi.
Baadhi ya mafanikio hayo ni pamoja na utoaji chanjo kwa watoto, Wizara kutekeleza mikakati mbali mbali ikiwemo mafunzo ya utoaji wa chanjo 172 katika wilaya zenye kiwango kidogo cha chanjo, uchapishaji na usambazaji wa vipeperushi 7,250 na mabango 7,500 kwa jamii na vituo vya afya.
Kwa upande wa Huduma za Uzazi, Miongoni mwa mbinu zinazotumika katika kuhakikisha mama wajawazito wanajifungua katika vituo vya afya na hospitali Wizara imeanzisha mpango maalumu katika wilaya ya Kaskazini B ili kufikia lengo hilo.
Mpango huu unatumia wafanyakazi wa jamii wa kujitolea ambao huwatembelea mama wajawazito majumbani mwao kwa lengo la kuwaelimisha juu ya masuala hayo ambapo Jumla ya wajawazito 674 wamekwishanufaika na mpango huo tangu mradi kuanzishwa kwake mwishoni mwa mwezi wa Machi, 2016.
Katika kutekeleza juhudi za kupunguza vifo vya uzazi na watoto wachanga, Serikali ilifanya mapitio ya muongozo wa kufanya tathmini ya vifo vya uzazi na watoto wachanga ili kuhakikisha inalinda afya ya mama na mtoto ambao ndio rasilimali ya taifa.
Huduma za uzazi wa mpango ziliendelea kutolewa kwa kununua dawa za uzazi wa mpango na kusambaza katika vituo vya afya Unguja na Pemba kwa msaada wa Shirika la Kushughulikia Idadi ya Watu Duniani.
Aidha, kupitia mradi huo, Serikali inaendelea na ujenzi wa mashimo ya kutupia taka za mazalio katika vituo vinane vya Nungwi, Pwani Mchangani, Uroa, Uzini na Selem kwa Unguja na Mkia wa Ng'ombe, Tundauwa na Fundo kwa Pemba. Vile ujenzi wa vinu vya kuchomea taka taka za hospitali vinajengwa katika hospitali za VItongoji, Micheweni na Wete.
Ili wananchi wawe na afya bora kwa kuwasogezea huduma za afya karibu na maeneo yao, Wizara ya Afya imeendelea kutekeleza mradi wa kupandisha hadhi hospitali za vijiji kuwa za wilaya na wilaya kuwa za mkoa kwa kuimarisha majengo na kuongeza huduma, vifaa na rasilimali watu ili kutoa huduma za afya stahiki kwa wananchi.
Katika hatua hiyo, katika ufunguzi wa hospitali ya Abdalla Mzee, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein aligiza Wizara ya Afya kujipanga na kuhakikisha uwepo wa nguvu kazi ya kutosha itakayowezesha kupatikana huduma masaa yote.
Sanjari na hilo, Dkt Shein aliwataka viongozi wa hospitali hiyo kusimamia vyema na kuilinda miundombinu iliyowekwa pamoja na utunzaji wa vifaa ili iweze kuwahudumia wananchi kulingana na malengo yaliyokusudiwa.
Aidha, Dkt Shein aliwataka wananchi kutumia kikamilifu fursa ziliopo za kupatiwa huduma za matibabu na uchunguzi katika hospitali hiyo wakati wote na kuondoa mazoea ya waweze kuhudumiwa kulingana na utaratibu utakaopangwa na Wizara ya Afya.
Ili kupunguza gharama za kusafirisha wagonjwa nje ya Zanzibar na nje ya nchi, Serikali imechukua hatua za makusudi kuipandisha hadhi Hospitali ya Mnazi Mmoja kuwa ya Rufaa ambapo Wizara imekarabati jengo la Wodi ya Watoto ulioanza Disemba 2014, na kutekelezwa na Kampuni ya Ujenzi ya Rans iliyopo hapa Zanzibar.
Ujenzi huo uliogharimu jumla ya Tsh bilioni 2.4 ambapo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imechangia Tsh 495,000,000 na fedha zilizobaki zimechangiwa na Serikali ya Norway kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Haukeland Bergen cha nchini humo.
Pia kumekuwa na mradi Shirikishi wa Kudhibiti Maambukizo ya Ukimwi, Kifua Kikuu na ambapo katika huduma za Uchunguzi wa VVU, Zanzibar ina vituo vya utoaji ushauri nasaha na upimaji wa VVU vipatavyo 98 vikiwemo 76 vya serikali, 10 vya Jumuiya zisizo za Serikali, vinne vya taasisi za dini na vinane vya binafsi.
Hatua hiyo imeifanya Zanzibar kwa mwaka 2015 kuwa na jumla ya watu 101,669 walipatiwa ushauri nasaha na upimaji wa vvu.
Kati yao 48,601 ambao ni sawa na asilimia 48 walikuwa wanawake na 53,068 sawa na asilimia 52 walikuwa wanaume. Kati ya waliopima asilmia 1.2 waligunduliwa na Virusi vya UKIMWI. Vile vile jumla ya watoa huduma za afya 32 walipatiwa mafunzo msasa juu ya ushauri nasaha na upimaji wa VVU pamoja na mafunzo msasa kwa watoa huduma 30 Unguja na Pemba juu ya upimaji na ushauri nasaha kwa watoa huduma hiyo.
Kwa upande wa huduma za Tiba, wizara imemarisha tiba na ushauri nasaha ambapo jumla ya kliniki 12 zinatoa huduma na tiba (8 Unguja na 4 Pemba) kwa wanaoishi na virusi vya Ukimwi (VVU).
Hadi kufikia mwisho wa mwezi Disemba 2015 jumla ya wagonjwa 8,721 walikuwa tayari wameshasajiliwa kwenye kliniki hizo, miongoni mwao ni wagonjwa 6,251 sawa na asilimia 71.7 walianzishwa dawa za kupunguza makali ya VVU (ARVs) wagonjwa waliobaki kwenye dawa mpaka kufikia Machi 2016 ni 3,978.
Kazi nyengine iliyofanya ni kukusanya sampuli za damu za watoto ambao mama zao wameambukizwa na virusi vya UKIMWI na kupelekwa Hospitali ya Muhimbili kwa ajili ya uchunguzi zaidi ambapo jumla ya sampuli 171 zimepelekwa katika hospitali hiyo, kati ya sampuli hizo 146 zimetolewa majibu watoto wawili kati yao waligundulika kuwa na maambukizi ya VVU.
Katika jitihada za kuimarisha nguvu kazi ya taifa, Serikali inaendelea kupambana na tatizo la madawa ya kulevya kwa kupunguza athari kwa vijana walioathirika na madawa hayo kwa kuwapatia dawa aina ya methadone ili kuachana na matumizi ya madawa ya kulevya.
Hatua hiyo imesaidia jumla ya vijana 168 kuendelea na matibabu hayo katika kituo maalumu kilichopo katika hospitali ya wagonjwa wa Akili Kidongo Chekundu ambapo masuala ya utawala Kamisheni inayohusiana na dawa za kulevya ipo chini ya Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais.
Kwa upande wa kifua kikuu jumla ya wagonjwa 457 waligundulika kuwa na ugonjwa huo ambapo wagonjwa 262 wapo Unguja na 195 wapo Pemba.
Sambamba na hilo, jumla ya wagonjwa 193 wamefuatiliwa katika familia zao, watu 667 walipata elimu juu ya kujikinga na maradhi hayo, kati yao wanne walikuwa na dalili na mmoja alithibitika kuwa na kifua kikuu.
Katika kupunguza ulemavu utokanao na Ukoma, zoezi la kuwafuatilia watu walioambukizwa na ugonjwa wa ukoma limefanyika Unguja na Pemba, kwa lengo la kuwatambua wale ambao wanaweza kufanyiwa urekebishaji wa viungo.
Katika zoezi hilo, jumla ya watu watano wamepatikana kutoka Wilaya ya Kusini Unguja na wanategemewa kufanyiwa upasuaji.
Aidha, uchunguzi ulifanyika katika Shehia 15 za Wilaya ya Kusini Unguja, ambako ugonjwa huu umeenea. Katika uchunguzi huo jumla ya watu 2,275 walichunguzwa, kati yao watu 215 walikuwa na maradhi ya ngozi na watu 40 waligundulika na maradhi ya Ukoma ambapo matibabu stahiki yalitolewa kwa wale wote waliogunduliwa na maradhi hayo.
WIZARA ya Afya imeeleza miongoni mwa juhudi zake inazoendelea kuzichukua katika kuhakikisha sekta hiyo inaimarika ni pamoja na kuwapeleka wataalamu wake wa fani mbali mbali masomoni ili kuendelea kujenga uwezo na kuelekea kwenye kujitegemea.
Hayo yameelezwa na uongozi wa Wizara hiyo, huko Ikulu mjini Zanzibar katika kikao maalum kati ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein na uongozi wa Wizara hiyo ilipokuwa ikiwasilisha Taarifa yake ya Utekelezaji wa Mpango Kazi wa Wizara kwa kipindi cha Julai hadi Septemba katika Bajeti ya mwaka 2016-2017.
Katika maelezo yake, Waziri wa Wizara hiyo Mahmod Thabit Kombo amesema kuwa Wizara bado inaendelea kupata mafanikio makubwa katika kuendeleza miundombinu yake hasa katika hospitali mpya ya Abdalla Mzee na kuweka vifaa vipya na vya maabara.
Waziri Kombo alitumia fursa hiyo kueleza majukumu Makuu ya Wizara hiyo ambapo pamoja na majukumu hayo Wizara imezingatia Sera, Mipango na mikakari mbali mbali ya Kitaifa na Kimataifa ikiwa ni pamoja na Malengo ya Maendeleo Endelevu 2030, Dira ya Zanzibar 2020, Sera ya Afya 2011, Mpango Mkakati wa III wa Sekta ya Afya pamoja na Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwak 2015-2020.Uongozi huo pia, ulizipongeza juhudi za Dk. Shein anazozichukua katika kuwapa maelekezo na ushauri ambao unaendelea kuwasaidia katika utendaji wao wa kazi.
Katika suala zima la upatikanaji wa dawa katika vituo vya afya, uongozi huo umezipongeza juhudi zilizochukuliwa na Serikali katika kuhakisha Bohari yake kuu inazo dawa za kutosha.Uongozi huo pia, ulieleza juhudi za makusudi zinazoendelea kuchukuliwa na Wizara hiyo katika uanzishwaji wa Bima ya Afya pamoja na hatua zilizofikiwa.
Mapema Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein alizipongeza juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na Wizara hiyo katika utoaji huduma ya afya kwa wananchi hapa nchini.
Dk. Shein alieleza haja ya kuendelea na utaratibu wa kuwapa mafunzo watendaji wa Wizara hiyo katika kada mbali mbali kwa lengo la kuja kutoa huduma kwa wananchi huku akisisitiza azma ya Serikali kupitia Wizara hiyo kuendelea kutoa huduma mbali mbali za upasuaji ambazo zitapunguza gharama za kuwapeleka wagonjwa nje ya nchi.
Aidha, Dk. Shein alisisitiza umuhimu wa kulipa kipaumbele suala zima la utafiti ndani ya Wizara hiyo huku akisisitiza suala zima la uzalendo na kueleza kuwa utaratibu wa kuwapeleka watendaji wa Serikali kufanya kazi Pemba sio adhabu bali ni taratibu za kiutumishi.
Dk. Shein aliyasema hayo katika hotuba yake iliyosomwa kwa niaba na Waziri wa Nchi Afisi ya Rais Ikulu na Utawala Bora Dk. Mwinyi Makame Mwadini, mara baada ya kulifungua jengo la wagonjwa wa nje katika Hospitali ya Kivunge, Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Katika hotuba hiyo, Dk. Shein alisema kuwa huduma bora za afya kwa wananchi wote bila ya ubaguzi ni miongoni mwa malengo ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964 ambapo Chama cha ASP kilichoongoza Mapinduzi hayo katika manifesto yake, kiliweka bayana azma yake ya kutoa huduma za afya bure bila ya ubaguzi wakati kitakaposhika hatamu za Serikali.
Dk. Shein alisema kuwa jitihada kubwa zimefanywa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kipindi cha miaka 52 ya Mapinduzi katika kuimarisha huduma za afya kwa kutambua kwamba afya bora ni muhimu kwa wananchi ili waweze kuishi vyema katika kazi ya kuleta maendeleo ya nchi yao.
Alisema kuwa mafanikio makubwa yamepatikana katika utekelezaji wa mipango na mikakati ya kuiendeleza sekta ya afya nchini kupitia vitengo na programu mbalimbali zinazoendeshwa na serikali kwa ushirikiano na washirika wa maendeleo.
“Nyote ni mashahidi wa kuimarika kwa huduma za afya katika hospitali na vituo vytetu vyote va afya... Aidha, kuna ongezeko kubwa la vituo vya afya vya daraja mbalimbali kiasi kwamba hivi sasa wananchi wa Zanzibar hawawezi kwenda zaidi ya kilomita tano bila ya kukuta kituo cha afya” alisema Dk. Shein.
Akieleza historia ya huduma za afya katika Mkoa wa Kaskani Unguja, Dk. Shein alisema kuwa kabla ya mapinduzi matukufu ya mwaka 1964 katika mkoa huo kulikuwa na vituo viwili tu vya afya ambavyo vilikuwepo Mkokotoni na Chaani.
Alisema kuwa katika kipindi cha miaka 52 ya Mapinduzi Mkoa huo hivi sasa una vituo vya afya 26 ambapo vituo 18 ni vya daraja la kwanza na 7 ni vya daraja la pili pia, kuna hospitali ya Koteji ya Kivunge ambayo lengo la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba ni kuipandisha daraja kuwa hospitali ya Wilaya.
Dk. Shein alisema kuwa lengo la mradi huo ulioanza mwaka 2012 ni kuziimarisha huduma za afya katika hospitali zote za Koteji ili kupunguza msongamano wa wagonjwa katika hospitali kuu ya Mnazi Mmoja.
Aidha, Dk. Shein alisema kuwa serikali imekusudia kuzisogeza huduma za afya kuwa karibu zaidi na wananchi ikiwa ni pamoja na huduma za upasuaji kwa kinamama wajawazito, huduma za uchunguzi kama vile za maabara, “X-ray” na “Ultra-sound”.
Pamoja na hayo, Dk. Shein alitumia fursa hiyo kutoa shukurani za dhati kwa shirika lisilokuwa la kiserikali la Uingereza HIPZ, UNICEF na ROTARY Club kwa kuiunga mkono serikali katika lengo la kuiimarisha hospitali hiyo.
Dk. Shein alisema kuwa huduma zinazotolewa katika hospitali hiyo zimeimarika sana baada ya serikali kupitia Wizara ya Afya kuongeza wafanyakazi, vifaa vya uchunguzi wa maradhi na kuongeza aina za huduma zinazotolewa katika hospitali hiyo.
Sambamba na hayo, Dk. Shein alitumia fursa hiyo kuwahimiza wazazi juu ya umuhimu wa kwenda kujifungulia hospitali na kuhudhuria kliniki ili kupima na kupatiwa ushauri pamoja na kuhakikisha watoto wanapelekwa vituoni kupatiwa chanjo kwa kuzingatia kampeni ya chanjo kwa watoto zinazoendeleshwa na Wizara ya Afya.
“Serikali itaendelea kuzipatia ufumbuzi changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya afya kwa lengo la kuwapatia huduma bora za afya wananchi wote mjini na vijijini”, alisema Dk. Shein.
Aidha, Dk. Shein alitoa wito kwa wananchi wote kuendelea kusherehekea maadhimisho ya miaka 52 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar kwa amani na utulivu.
Nae Waziri wa Wizara ya Afya Mahmoud Thabit Kombo aliwaeleza wananchi waliohudhuria uzinduzi wa hospitali hiyo kuwa hatua hizo ni miongoni mwa ahadi za Dk. Shein kupitia Ilani ya Uchaguzi ya CCM ambazo ameziahidi na sasa anaendelea kuzitekeleza huku akitoa shukurani kwa washirika wa maendeleo yakiwemo Mashirika ya Umoja wa Mataifa kwa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar.
Nae Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Mohemmed Saleh Jidawi amezitaja juhudi mbali mbali zinaendelea kuchukuliwa na Serikali chini ya uongozi wa Dk. Shein katika kuhakikisha Hospitali za Koteji kuwa za Wilaya na kueleza kuwa gharama za ujenzi huo ni milioni 461 chini ya ufadhili kutoka kwa Shirika la HIPZ.
Dk. Jidawi alisema kuwa lengo ni kuhakikisha hospitali hiyo inakuwa ya Wilaya na kulipongeza Shirika la HIPZ kwa kuendelea na juhudi zake katika kuiimarisha hospitali ya Kivunge kama ilivyofanya kwa hospitali ya Makunduchi.
Hospitali hiyo ina uwezo wa kupokea wagonjwa 120 hadi 140 kwa siku mbapo pia itafanya kazi kwa masaa 24 kwa kutumia mfumo wa kisasa wa kuwaorodhosha wagonjwa kwa njia ya Kompyuta kwa lengo la kutunza kumbukumbu za wagonjwa na muda wa kupanga foleni wakati wa kutoa na kupata huduma.
Nao washirika wa maendeleo wakiwemo wawakilishi wa HIPZ, UNICEF, ROTARY CLUB pamoja na uongozi wa Mfuko Taifa wa Bima za Afya wameahidi kuendelea kuiunga mkono Serikali ya Mapinduzi katika kuimarisha na kutoa huduma bora kwa wananchi.
Aidha, washirika hao walieleza kuwa kituo hicho kitakuwa ni mkombozi kwa akina mama na kutoa shukurani kwa ushirikiano wanayoyapata kutoka kwa uongozi wa Serikali ya Zanzibar.

Post a Comment